Lionel Richie alazwa ICU
Muktasari:
- Kwa mujibu wa TMZ, mwimbaji huyo alipelekwa hospitali mjini St. Louis baada ya kuonekana akipata wakati mgumu kumaliza onyesho lake akiwa kwenye ziara ikielezwa kwamba amekuwa akitumbuiza bila kupumzika.
ST. LOUIS, MAREKANI: RIPOTI mpya imeeleza kuwa mwanamuziki maarufu Lionel Richie, mwenye umri wa miaka 77, Jumamosi iliyopita alikimbizwa hospitali baada ya kukumbwa na tatizo la kiafya katikati ya onyesho la muziki, ambapo alifikia kulazwa katika chumba cha wahonjwa mahututi (ICU).
Kwa mujibu wa TMZ, mwimbaji huyo alipelekwa hospitali mjini St. Louis baada ya kuonekana akipata wakati mgumu kumaliza onyesho lake akiwa kwenye ziara ikielezwa kwamba amekuwa akitumbuiza bila kupumzika.
Taarifa zinaeleza kwamba wakati akiimba wimbo wake maarufu “All Night Long,” Richie alimuomba mmoja wa wafanyakazi ampelekee kiti jukwaani, na baada ya hapo alilazimika kutumia muda mfupi uliobaki wa onyesho akiimba huku akiwa amekaa. Hata hivyo, alizidiwa na kukimbizwa hospitali baada ya kuonekana akiishiwa nguvu.
Hadi sasa, menejimenti ya mwanamuziki huyo haijatoa maelezo kuhusu tukio hilo. Lionel amekuwa ziarani pamoja na kundi la Earth, Wind & Fire. Kwa mujibu wa ripoti ya awali ya TMZ, madaktari wanachunguza uwezekano kwamba huenda alikumbwa na upungufu wa maji mwilini na alitarajiwa kuruhusiwa kutoka hospitalini, leo Jumanne.
Ziara yake ya “Sing A Song All Night Long”, akiwa pamoja na Earth, Wind & Fire, ilianza mwezi Juni, mwaka huu. Hata hivyo, baada ya Richie kuugua akiwa katikati ya onyesho la ufunguzi, waandaaji walilazimika kuahirisha maonyesho mawili yaliyofuata ili kumpa muda wa kupona.
Taarifa iliyotolewa na Live Nation wakati huo ilisema: “Kwa ushauri wa madaktari kwamba apumzike na kurejea katika afya yake kamili, Lionel Richie ameahirisha maonyesho yake mawili yanayofuata, Ijumaa, Juni 26 jijini Chicago, Illinois, na Jumamosi, Juni 27 jijini Columbus, Ohio.”
Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa yeye pamoja na Earth, Wind & Fire wangerejea jukwaani Jumanne, Juni 30, jijini Pittsburgh, Pennsylvania.
“Lionel amevunjika moyo kutokana na kuahirisha maonyesho haya mawili na hawezi kusubiri kurejea jukwaani kuwatumbuiza mashabiki wake. Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote ambao jambo hili limewasababishia mashabiki wenye tiketi za maonyesho hayo mawili. Tarehe mpya zitatangazwa hivi karibuni,” ilisema taarifa hiyo.
Muda mfupi baadaye, baada ya kurejea jukwaani, mwimbaji huyo wa “Dancing on the Ceiling” alirejea kwenye mitandao ya kijamii na kuwapa mashabiki wake taarifa kuhusu hali yake.
Aliandika: “Asanteni kwa kila ujumbe, kila neno la upendo na kwa upendo wenu wote. Ninaendelea vizuri, na ninawashukuru sana nyote.”
Richie aliwahi kueleza changamoto za kiafya za wasanii wanapokuwa kwenye ziara, ambapo mwaka 2017, nyota huyo ambaye pia ni jaji wa kipindi cha American Idol alizungumza na jarida la Forbes kuhusu baadhi ya changamoto ambazo hukabiliana nazo wanapokuwa kwenye ziara.
“Mbali na kupata usingizi mzuri, chakula kizuri na maji mengi, jambo lingine ambalo watu walio kwenye ziara hulisema mara nyingi kuliko kitu kingine chochote ni, ‘nahitaji daktari,’” alisema kwa mzaha.
Alieleza kuwa sababu ni kwamba wasanii wanaweza kukumbwa na mabadiliko ya mwinuko wa maeneo wanayokwenda, matatizo kama upungufu wa maji mwilini au hata sumu ya chakula.
“Kuna mambo mengi yanayotokea ukiwa kwenye ziara ambayo huwezi kuyatabiri. Tatizo ni kwamba hutaki kuhatarisha hali ambapo huna njia rahisi ya kumuona daktari, isipokuwa labda kupitia hoteli ambayo inaweza kukutafutia daktari,” alisema na kuongeza:
“Hata hivyo, kuna baadhi ya nyakati unaweza kuwa nyumbani kwa mtu ukiwa kwenye ziara. Haupo hotelini, na unatoa huduma.”