Mbosso alivyowabeba wasanii WCB Wasafi
Muktasari:
- Mbosso ambaye kwa sasa anafanya muziki akiwa kama mwanamuziki huru chini ya lebo yake ya Khan Music, kwa sehemu ameshiriki kuwabeba Lava Lava na D Voice.
MARA nyingi ilizoeleka kuwa Diamond Platnumz ndiye alikuwa akiwabeba wanamuziki wa WCB Wasafi kupitia nyimbo walizoshirikiana, lakini hata Mbosso naye amefanya hivyo kwa baadhi ya wasanii wa lebo hiyo.
Mbosso ambaye kwa sasa anafanya muziki akiwa kama mwanamuziki huru chini ya lebo yake ya Khan Music, kwa sehemu ameshiriki kuwabeba Lava Lava na D Voice.
Utakumbuka Mbosso alitambulishwa rasmi WCB Wasafi mwaka 2018 ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu kusambaratika kwa kundi la Yamoto Band ambalo alifanya nalo kazi tangu 2013 akiwa na wenzake watatu.
Akiwa WCB Wasafi, Mbosso alitoa albamu moja, Definition of Love (2021), pamoja na Extended Playlist (EP) moja, Khan (2022) ambayo ilimpatia Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kwa mara ya kwanza akiwa kama solo.
Lakini, kwa namna gani Mbosso amewabeba kimuziki Lava Lava na Mbosso? Jibu ni kwamba nyimbo za wasanii hao wawili ambazo zimeuza zaidi mtandaoni ni zile ambazo wamemshirikisha na Mbosso.
Lava Lava & Mbosso
Hadi sasa wimbo wa Lava Lava uliofanya vizuri zaidi katika mtandao wa YouTube ambao ndio soko kuu la wasanii wa Bongofleva, ni ule ambao amemshirikisha Mbosso, Basi Tu (2021) ambao umetayarisha na Laizer.
Ikiwa ni miaka mitano imepita tangu video ya wimbo huo iliyoongozwa na Director Kenny imeachiwa, imeshatazamwa (views) zaidi ya mara milioni 30.2 YouTube, na hivyo kuwa kazi pekee ya Lava Lava yenye namba za juu zaidi katika jukwaa hilo.
Video hiyo ilikuja kuipiku ile ya wimbo uliomtoa Lava Lava kimuziki, Tuachane (2017) ambao ulikuwa namba moja kwa muda mrefu, na hadi anaondoka WCB Wasafi bado ilikuwa hivyo ila baada ya muda kolabo na Mbosso ikapindua meza.
Hiyo ni tofauti kidogo na Harmonize ambaye hadi sasa video yake yenye namba za juu zaidi ni ile ya wimbo aliyomshirikisha Diamond, Kwangwaru (2018) ambayo imeshatazamwa mara milioni 144.8, huku kazi yake inayofuatia ikiwa haifiki hata nusu ya namba hizo.
Hata hivyo, mbali na Harmonize, kuna wasanii wengi ambao nyimbo walizoshirikiana na Diamond zina rekodi ya kufanya vizuri zaidi kiasi kwamba wamekuja kupata ugumu kuzifikia rekodi za aina hiyo.
Baadhi yao ni Chege (Waache Waoane), Linex (Salima), Navy Kenzo (Katika), Jux (Enjoy), G Nako (Komando), Barnaba (Salama), na Mr. Flavour (Time To Party) kutokea Nigeria.
D Voice & Mbosso
Mara nyingi akijitambulisha kama mwanamuziki wa Singeli, ila bado D Voice ameendelea kufanya vizuri katika Bongofleva na kazi yake namba moja YouTube ni ya miondoko hiyo ambayo amemshirikisha Mbosso, Tunapendana (2024).
Licha ya D Voice kufanya kolabo nyingi na Zuchu na Diamond ambao wana nguvu kubwa ya ushawishi katika mtandao huo, lakini kolabo na Mbosso ndio imetokea kupendwa zaidi ikiwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 36.2 hadi sasa.
Baada ya hapo ndipo kolabo zake tatu na Zuchu zinafuatia ambazo ni BamBam (2023), Nani (2025) na Baridi (2026). Utakumbuka kwa ujumla D Voice na Zuchu wameshirikiana katika nyimbo sita ambazo zimetoka kati ya mwaka 2023 hadi 2026.
Kolabo yake na Zuchu (BamBam) ndio ilikuwa namba moja YouTube kwa upande wake D Voice kwa muda mrefu ila ikaja kupitwa na hiyo aliyofanya na Mbosso (Tunapendana), huku kolabo zake mbili na Diamond zikiwa na namba za chini sana.
Licha ya Zuchu kupoteza rekodi hiyo kwa D Voice, bado ana rekodi sawa na hiyo kwa Rayvanny ambaye wimbo wake namba moja YouTube ni Number One (2020) akimshirikisha Zuchu ambao video yake imeshatazamwa mara milioni 127.9.
Utakumbuka kuwa Zuchu anashikilia rekodi kama mwanamuziki wa kwanza solo [bila kushirikiana na msanii mwingine] kutoka Tanzania na Afrika Mashariki kwa video ya wimbo wake kutazamwa mara milioni 100 YouTube.
Zuchu aliweka rekodi hiyo mnamo Machi 2024 kupitia video ya wimbo wake 'Sukari' iliyotoka Januari 30, 2021 ikiwa imeongozwa na Director Kenny, huku ikiandika rekodi ya kuwa video iliyotazamwa zaidi YouTube Afrika kwa mwaka huo, rekodi ambayo hadi sasa hakuna msanii wa Bongofleva aliyeweza kuifikia.