Video za Bongofleva zilizofanyika nje ya Afrika
Muktasari:
- Kuanzia Alikiba hadi Diamond Platnumz, bila kuwasahau Navy Kenzo na Country Wizzy, ni miongoni mwa wanamuziki wengi wa Bongofleva waliofanya hivyo. Fahamu zaidi hapa.
BAADHI ya wanamuziki wa Bongofleva siyo tu wamevuka mipaka ya Tanzania kwenda kushuti video za nyimbo zao, bali wametoka nje kabisa ya Bara la Afrika kwa lengo la kujaribu vitu vipya na kuleta utofauti wa kazi.
Kuanzia Alikiba hadi Diamond Platnumz, bila kuwasahau Navy Kenzo na Country Wizzy, ni miongoni mwa wanamuziki wengi wa Bongofleva waliofanya hivyo. Fahamu zaidi hapa.
1. Ommy Dimpoz (Vacation - 2022) Ulaya: Ni video ambayo ilifanyika katika kisiwa maarufu nchini Hispania cha Ibiza. Kwa mujibu wa Dimpoz, yeye ndiye mwanamuziki wa kwanza wa Bongofleva kushuti video katika eneo hilo ambalo hupokea watalii wengi.
2. Alikiba (Mbio - 2019) Asia: Video ya wimbo huu ambayo imeongozwa na Director Kevin Bosco Jnr, imefanyika katika eneo la Jebel Sifah, ambalo ni miongoni mwa vivutio vizuri vya utalii vilivyopo Muscat nchini Oman. Inaelezwa kuwa Alikiba alianza kuandika wimbo huo miaka 10 iliyopita akiwa Oman kabla ya kurejea tena nchini humo kwa ajili ya kushuti video hiyo, na kufanya show katika Hoteli ya Intercontinenta.
3. Jux (Sexy & Bad - 2026) Ulaya: Wimbo huu mpya wa Jux ambao amemshirikisha Stonebwoy kutokea Ghana, video yake yote imefanyika jijini London, Uingereza huku ikipambwa na mastaa wakubwa Afrika kama Davido, Tiwa Savage na Mr. P wa kundi la P-Square.
4. AY (Touch Me - 2014) Amerika Kaskazini: Wimbo huu ambao AY amewashirikisha Sean Kingston na Ms Triniti, imefanyika Marekani katika maeneo mawili tofauti ambayo California na Miami.
5. Navy Kenzo (Morning - 2017) Asia: Kundi hili linaloundwa na Aika na Nahreel, walipoenda Tel Aviv nchini Israel kwa ajili ya ziara yao ya dunia, AIM World Tour, ndipo walishuti na video ya wimbo huo uliojumuishwa katika albamu yao ya kwanza chini ya The Industry.
6. Country Wizzy (Let It Go - 2023) Ulaya: Rapa huyu aliweka kambi ya muda huko Vienna nchini Austria, na ndipo aliposhuti video ya wimbo huu ikiongozwa na Director Chris VMC.
7. Shilole (Malele - 2015) Ulaya: Miaka 10 iliyopita, staa huyu alienda Ubelgiji kufanya show ndipo akaaanza kushuti video ya wimbo huo kabla ya kwenda kumalizika vipande vinginne huko nchini Uholanzi. Ni video ambayo ukiitazama inaonyesha kabisa mazingira ya bara la Ulaya.
8. Ommy Dimpoz (You Are The Best - 2019) Asia: Ikiwa imeongozwa na Director Hanscana kutokea Bongo, chupa hili limefanyika huko Muscat Bay nchini Oman, katika eneo la Jebel Sifah ambalo ni maarufu kwa utalii. Vilevile video ya wimbo wa Ommy Dimpoz, Cheed na Alikiba, RockStar (2019), imefanikiwa katika eneo hilo hilo.
9. Jux (Uzuri wako - 2014) Asia: Kipindi anasoma nchini China, ndipo Jux alishuti video ya wimbo huu jijini Beijing ambapo iliongozwa na Zed Benson.
10. Diamond (Marry You - 2017) Amerika Kaskazini: Vipande vyote ambavyo Ne-Yo na Diamond wanaonekana katika video ya wimbo huu vimeshutia Los Angeles, Marekani, eneo la Beverly Hills ambalo ni maarufu kwa mastaa wa Hollywood. Hata hivyo, video hiyo yote haikufanyika Marekani, kuna baadhi ya vipande vichache vimeshutiwa Johannesburg, Afrika Kusini, na ndio vile ambavyo kina Rich Mavoko na Q Boy Msafi wameonekana.