KISIWA CHA UMAUTI -36
Muktasari:
- Wakati huo Yasmin alikuwa akitiriikwa na machozi kwa kumuona kaka yake.
ILIPOISHIA
Baada ya maofisa hao kumsalimia Yasmin walithibitisha kwamba alikuwa binti wa Rais Sharif Abdulatif aliyepotea nchini mwao katika mazingira ya kutatanisha.
Wakati huo Yasmin alikuwa akitiriikwa na machozi kwa kumuona kaka yake.
Yasmin aliwaeleza masahibu yaliyokuwa yamemtokea, maelezo ambayo yalimshitua kaka yake pamoja na maofisa hao.
SASA ENDELEA...
Baada ya kuthibitishwa kwamba Yasmin alikuwa binti wa Rais wa Comoro, aliitwa ikulu pamoja na kaka yake. Yasmin aliomba na mimi niwemo kwenye msafara huo. Ombi lake lilikubaliwa. Nilipatiwa mavazi mengine, tukapakiwa kwenye gari na kupelekwa ikulu, ambako tulikutana na Rais wa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar alimsikiliza Yasmin na kushangazwa na maelezo ya binti huyo wakati akimsimulia masahibu aliyokutana nayo.
“Hata hivyo, wewe ni shujaa kwa sababu hukukata tamaa,” Rais alimwambia Yasmin. Pia alinipongeza mimi kwa kunusurika kufa.
“Mkasa uliowakuta ni historia kubwa ya visiwa vyetu,” Rais aliendelea kutuambia.
Rais wa Zanzibar akawasiliana na Rais mwenzake wa Comoro na kuzungumza naye.
“Binti yako Yasmin ninaye hapa,” Rais wa Zanzibar alimwambia Rais wa Comoro.
“Nimepata habari zake na nimeshukuru sana kusikia kwamba mwanangu bado yuko hai. Sisi tulidhani ameshakufa,” Rais wa Comoro alisema kwenye simu.
“Ni kweli kwamba alipotea siku ya harusi yake mwaka mmoja uliopita?”
“Ni kweli. Lilikuwa tukio la kushangaza sana!”
“Ameniambia alikuwa akiishi katika kisiwa kimoja kisicho na watu na hajui alifikaje katika kisiwa hicho.”
“Binti yangu alipata masahibu makubwa, lakini nashukuru kuwa amenusurika.”
“Huyu hapa, ongea naye.”
Rais alimpa Yasmin mkono wa simu ili azungumze na baba yake.
“Asalam alaykum, baba!” Yasmin alimwamkia baba yake.
“Wa alaykum salam warahmatulahi wabarakat. Hujambo, mwanangu?”
“Sijambo, baba. Matatizo yaliyonitokea ni kama ulivyoyasikia.”
“Nimeyasikia na nimemtuma kaka yako Umar na maofisa wangu kuja kukuona. Nimeambiwa kuwa mmeshakutana.”
“Tumekutana na kaka ninaye hapa.”
“Nimefurahi kwamba uko naye kwa Rais mwenzangu. Je, wewe afya yako ikoje?”
“Afya yangu si nzuri, lakini pia si mbaya sana. Nikija huko mtaniona.”
“Ulikuwa unaishi vipi huko kisiwani ulikokuwa?”
“Nimeishi kwa taabu tu, baba. Nikija nitawaeleza vizuri.”
“Ningependa uzungumze na mama yako ili umtoe wasiwasi, lakini hatapatikana kwa sasa kwa sababu mimi bado niko ikulu.”
“Hakuna wasiwasi, baba. Mwambie mama mimi ni mzima. Ni masahibu tu yamenikuta na, ishallah, nitakutana naye.”
“Si mtakuja hii leo?”
“Kama tutaruhusiwa kuondoka, tutakuja leo.”
“Sawa. Sasa mpe simu Mheshimiwa Rais.”
Yasmin akampa simu Rais wa Zanzibar.
“Umeshazungumza na mwanao?” Rais wa Zanzibar akamuuliza Rais wa Comoro kimzaha.
“Tumezungumza kidogo. Unatarajia wataweza kuondoka leo hii kurudi Comoro?”
“Kwa vile ndege iko tayari, sioni cha kuwazuia kuondoka leo.”
“Basi ningependa uwaruhusu kuondoka na mtupatie taarifa muda ambao wanaondoka.”
Baada ya marais hao kumaliza kuzungumza, Rais wa Zanzibar alizungumza na maofisa wake.
“Nataka mhakikishe kuwa ugeni huu unaondoka leo kurudi Comoro. Na kwa upande wa huyu binti, apatiwe mahitaji yote ya kibinadamu kwa gharama ya serikali wakati akiwa hapa nchini kwetu, bila kumsahau kijana Zahrani aliyekuwa naye kule kisiwani.”
Zahrani ndilo jina nililozoewa kuitwa huko Zanzibar.
Baada ya Rais kutoa agizo hilo, aliagana na sisi na kututakia safari njema akina Yasmin.
Yasmin alimuahidi Rais wa Zanzibar kuwa hataisahau Zanzibar na atarudi kuitembelea tena atakapojaliwa.
Tulipotoka ikulu, tulipelekwa katika hoteli ya Bwawani, ambako tulipatiwa huduma mbalimbali kama vile chakula, nguo na mahali pa kupumzika. Hapo tulikutana na watu mbalimbali waliopata habari zetu na kututembelea. Walikuja maofisa wa serikali na pia mawaziri.
Kusema kweli, nilipata umaarufu mkubwa kutokana na Yasmin. Kwa vile mwenzangu alikuwa binti wa Rais na alikuwa akieleza mara kwa mara kuwa kama si mimi na yeye angeangamia, watu waliotutembelea walikuwa wakitupa pole pamoja na kunipongeza.
Maelezo yetu yalionekana kama kioja kikubwa kwa vile yalimuhusisha jini anayeitwa Harishi, ambaye alimteka Yasmin nchini Comoro na kumpeleka katika kile kisiwa cha mauti.
Taarifa zilipowafikia waandishi, nao walianza kumiminika katika hoteli ya Bwawani kutuhoji na kutupiga picha.
Baadhi ya waandishi hao, baada ya kupata maelezo kutoka kwangu na kwa Yasmin, walimuhoji Yasmin kutaka kujua jinsi tulivyoishi katika kisiwa hicho tukiwa peke yetu.
Mwandishi: “Mliishije na Zahrani mkiwa watu wawili wa jinsia tofauti katika kisiwa hicho?”
Yasmin: “Tuliishi kama marafiki.”
Mwandishi: “Mlitarajia kuwa mngeokoka?”
Yasmin: “Kusema kweli, hatukutarajia, ingawa tulikuwa tunaomba sana.”
Mwandishi: “Mlikuwa mnalalaje usiku?”
Yasmin: “Usiku wa jana ndio tulilala pamoja, lakini pia hatukulala usingizi kwa sababu tulijua kuwa tungeuawa.”
Mwandishi: “Sasa umeshaokoka. Unadhani utaendelea kuwa karibu na Zahrani?”
Yasmin: “Bila shaka. Tulipokuwa kule kisiwani, nilimpa ahadi Zahrani kuwa kama tutasalimika atanioa.”
Mwandishi: “Una maana kwamba umempenda Zahrani?”
Yasmin akacheka kabla ya kujibu. “Nimempenda sana.”
Mwandishi: “Je, sasa unadhani utatimiza ahadi uliyomuahidi?”
Yasmin: “Ndiyo, nitaitimiza.”
Mwandishi: “Kwa hiyo una mpango wa kuoana na Zahrani?”
Yasmin: “Mpango bado, ni mawazo tu ambayo naamini hayatabadilika.”
Mwandishi: “Umetuambia kuwa kabla ya kupotelea katika kisiwa mlichokuwa mnaishi ulikuwa unaolewa na mwana wa mkuu wa jeshi la ulinzi la Comoro. Je, kijana huyo akitaka muoane tena itakuwaje wakati umeshamuahidi Zahrani kuwa mtaoana?”
Yasmin: “Nadhani atakuwa ameshaoa.”
Kaka wa Yasmin, Umar Sharif Abdulatif, ambaye alikuwepo wakati Yasmin anahojiwa, alithibitisha kuwa aliyekuwa anamuoa Yasmin kabla ya Yasmin kupotea Comoro alishaoa mke mwingine na walikuwa wanaishi Ufaransa. Visiwa vya Comoro vilikuwa koloni la Ufaransa.
Mwandishi: “Kwa hiyo unatarajia kwenda Comoro na Zahrani?”
Yasmin: “Natarajia hivyo.”
Mwandishi: “Ndoa yenu itafanyika lini?”
Yasmin: “Siku yoyote wazazi wetu watakaponiruhusu kuolewa na Zahrani.”
Mwandishi aliyekuwa akimuhoji Yasmin alinigeukia mimi.
Mwandishi: “Je, umeyachukuliaje maelezo ya Yasmin?”
Zahrani: “Yamenifurahisha sana.”
Mwandishi: “Uko tayari kuoana na msichana ambaye baba yake ni Rais wa nchi?”
Zahrani: “Kama wazazi wake watakubali, niko tayari.”
Mwandishi: “Mtakuwa mnaishi wapi mtakapooana, Zanzibar au Comoro?”
Zahrani: “Popote tu tutakapokubaliana.”
Mara tu baada ya waandishi wa habari kuondoka, maofisa wa usalama kutoka ikulu ya Zanzibar walinitambulisha kwamba umefika wakati ambapo nitaachana na Yasmin, kwa vile muda wa safari yao ya kurudi Comoro ulikuwa umefika.
Kauli ile ilinivunja moyo, hasa kwa vile nilitegemea kuondoka na Yasmin. Yasmin akawaomba maofisa hao waniache niende naye Comoro.
“Hatumzuii mtu yeyote kwenda mahali popote anapotaka, ila Zahrani hana hati ya kusafiria,” afisa mmoja alimwambia Yasmin.
Ilikuwa kweli sikuwa na hati ya kusafiria na hata Yasmin hakuwa nayo, lakini kwa vile aliingia Zanzibar kidharura, alilazimika pia kuondoka kidharura.
Yasmin akanitazama kwa butwaa.
“Hivi huna hati ya kusafiria?” akaniuliza.
“Sina,” nikamjibu huku nikitikisa kichwa.
“Kuna kipindi ulikuja Comoro, ulifikaje bila ya hati?”
“Sina maana kwamba sina kabisa. Hati yangu ya kusafiria iko Pemba.”
“Kumbe unayo. Sasa tutafanyaje?”
“Amua wewe.”
“Sasa sikiliza,” Yasmin alitaka kusema kitu, lakini akasita na kumtazama kaka yake. “Kaka, kama una dola mia tano, mpatie Zahrani zimwezeshe kuja Comoro.”
Umar alitoa dola mia tano hapo hapo na kunipa.
“Hizo zitakuwezesha kwenda Pemba kuonana na ndugu zako na kujiandaa kwa safari ya kuja Comoro siku yoyote utakayopenda,” Yasmin akaniambia.
Umar akanipa namba za simu za kuwatambulisha wakati nitakapokwenda Comoro.
Nilikubaliana na Yasmin kwa shingo upande. Mwenyewe alijua kuwa sikuridhika kuniacha Zanzibar, ingawa nilipatiwa nauli ya kwenda Comoro siku nitakayopenda kuondoka.
Baada ya Yasmin kuniambia hivyo, aliishia kunitolea tabasamu lenye mchanganyiko wa furaha na majonzi.
Mimi sikuweza kutabasamu. Kwa siku chache nilizokuwa naye nilikuwa nimeshamzoea Yasmin. Kitu muhimu ambacho nitakikosa kwake ni ile hewa ya mwili wake.
Alikuwa na hewa tamu na ya kusisimua ambayo huisikia kila ninapokuwa karibu naye.
Hewa ile ilikuwa inaniliwaza kuliko manukato ambayo hujitia mwilini mwake.
“Nitasubiri. Sina la kufanya,” nikamwambia kwa sauti nzito ya huzuni.
“Tutakutana mahabuba wangu. Sitakuacha,” Yasmin akaniambia kwa sauti ya chini. Hakutaka isikiwe na wengine.
Sasa msafara ulikuwa unakwenda kiwanja cha ndege. Na mimi nililazimika kuwasindikiza nikiwa pamoja na maofisa usalama.