Momanyi apiga hat trick, Singida ikifanya kweli CAF
Muktasari:
- Momanyi alifanya kazi hiyo mapema ndani ya kipindi cha kwanza, akifunga mabao yake dakika za 20, 23 na 32, kabla ya Sheikhan Khamis kuongeza bao lingine dakika ya 41 na kuifanya Singida kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 4-0.
SINGIDA Black Stars imeanza kampeni yake ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Al Ghazala ya Sudan Kusini, huku mshambuliaji wake, Mathew Tegisi Momanyi akiweka historia kwa kufunga mabao matatu 'hat-trick'.
Momanyi alifanya kazi hiyo mapema ndani ya kipindi cha kwanza, akifunga mabao yake dakika za 20, 23 na 32, kabla ya Sheikhan Khamis kuongeza bao lingine dakika ya 41 na kuifanya Singida kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 4-0.
Mwanzo huo uliifanya Singida kuonyesha mapema kwamba ilikwenda Juba ikiwa na mpango wa kuondoka na matokeo mazuri ugenini, huku Al Ghazala ikishindwa kuhimili mashambulizi ya kikosi hicho cha kocha Papy Kimoto.
Momanyi alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya wenyeji hao, akitumia vizuri nafasi zilizopatikana mbele ya lango na kukamilisha hat-trick yake ya kwanza akiwa na kikosi hicho ndani ya dakika 32 pekee.
Baada ya mapumziko, Singida iliendelea kushambulia na kuongeza bao lingine kupitia Jonathan Sowah dakika ya 63 na 90 na lile la Henry David dakika ya 85, huku Al Ghazala ikifanikiwa kupata bao la kufutia machozi dakika ya 70.
Ushindi huo ni hatua muhimu kwa Singida katika safari yake ya kimataifa, ikizingatiwa imepata matokeo mazuri na tofauti kubwa ya mabao ugenini kabla ya mchezo wa marudiano Septemba 13, 2026.
Kinachovutia zaidi ni namna Momanyi alivyoanza mashindano kwa kishindo, akifunga mabao matatu katika kipindi ambacho Singida ilitawala mchezo na kuweka msingi wa ushindi mkubwa.
Huu ni msimu wa pili kwa Singida kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, endapo timu hiyo itafanikiwa kufika hatua ya makundi, basi itakuwa moja ya timu changa ambazo zimefanya vizuri zaidi kwenye michuano ya CAF kwa miaka ya hivi karibuni.
Hata hivyo, kuvuka na kwenda hatua ya makundi ni mtihani kwa Singida kwani ikiitoa Al Ghazala itakutana na mshindi kati ya Al Ahli Madani ya Sudan na Tusker ya Kenya.