KISIWA CHAMAUTI - 26
ILIPOISHIA
Pakapita kimya kifupi kabla ya Yasmin kuniambia.
“Kisiwa chote hiki kilikuwa kina watu.”
“Wewe uliwakuta hao watu?” nikamuuliza.
“Wakati Harishi ananileta hapa, alikuwa ameshamaliza watu wote. Wengine walihama wenyewe kukimbia kifo.”
“Na kama leo anakuja na kutukuta hivi, itakuwaje?”
“Atakukamata wewe. Atakufyonza damu na ndiyo ataniuliza wewe ni nani na ulifuata nini hapa.”
“Ina maana wewe hatakuadhibu?”
“Ananitisha tu pale ninapomuudhi, lakini kama atanikuta na mwanaume, nadhani ataniadhibu.”.
SASA ENDELEA...
“LAKINI hatakufyonza damu?”
“Hapo siwezi kujua”
“Inatisha. Ni kwa vile tu umenihakikishia kwamba hatarudi tena leo”
Tulipofika katika jumba la Yasmin. Tulikaa katika ule ukumbi tukaanza kuzungumza.
Yasmin akanieleza wazi kuwa alikuwa amenipenda.
“Wewe ndio ungefaa uwe mume wangu” akaniambia kiudhati.
“Tayari umeshakuwa mke wa jini, huwezi tena kuwa mke wangu”
“Jini amenioa wapi? Si ananibaka tu!”
“Lakini ndio mume wako na amekuleta huku kusudi aweze kukudhibiti”
“Hakuna kisichokuwa na mwisho. Mwisho wake utafika tu”
“Inshaallah!”
“Mimi na wewe tutakwenda kuoana Comoro!”
Nikatikisa kichwa changu. Niliona Yasmin alikuwa anaota ndoto ya mchana.
“Yasmin huoni kuwa tuko jela! Unawazia kwenda kuoana Comoro, hapa tutatoka vipi?”
“Tutatoka tu iko siku. Kila siku mimi naswali na kuomba”
“Angekuwa ni mwanaadamu aliyekuweka hapa tungepambana naye. Lakini jini aliyemaliza kisiwa kizima ni hatari”
“Usikate tamaa, usinivunje moyo. Wewe mwanaume!” Yasmin aliposema hivyo alinyanyuka.
“Ngoja nikapike sasa” akaniambia na kuelekea jikoni.
Wakati anatembea nilimtazama kwa nyuma. Nguo alizokuwa amevaa zilimpendeza. Kama alivyotueleza mwenyewe nguo hizo alikuwa analetewa na Harishi ambaye huziiba kwnye maduka ya miji mikuwa.
Yasmin alipofika kwenye mlango wa kuingilia ndani aligeuka na kunitazama. Alipoona nilikuwa namuangalia akatabasamu kabla ya kuingia ndani.
Nilikaa peke yangu nikiwaza hili na lile. Nilijiambia Yasmin alikuwa msichana mzuri, kikwazo kilikuwa ni lile jini. Kama nafanikiwa kumuoa binti wa rais ni heshima kubwa.
Baada ya muda kidogo niliondoka nikamfuata Yasmin jikoni.
“Umenifuata huku?” Yasmin akaniambia.
“Nataka tusaidiane kupika” nikamwambia kwa mzaha.
“Si ungekaa tu nikakupikia mume wangu mtarajiwa”
Nilijua Yasmin alikuwa anajifariji kuniita “mume wangu mtarajiwa” Na mimi sikutaka kumvunja moyo. Kwa upande mwingine mimi pia nilihitaji faraja kutoka kwa Yasmin.
“Hapana nataka nikusaidie mtarajiwa wangu”
“Haya nisaidie”
Nikamsaidia Yasmin kupika huku mizaha na dhihaka zikipita. Kwa mara ya kwanza niligundua Yasmin alikuwa mchangamfu na aliyependa mzaha. Alikuwa akicheka hadi sauti yake ilisikika nje. Alikuwa amesahau kabisa mateso yaliyokuwa yanatukabili sisi na yeye.
“Yasmin unacheka sana, sauti yako inasikika nje” nikamwambia.
“Kwani nani atatusikia, si tuko peke yetu?”
“Najua tuko peke yetu lakini usicheke sana”
“Acha nifurahishe moyo wangu nisife na kinyongo”
“Sikuwa nikijua kuwa umchangamfu kiasi hicho”
“Mimi ni mchangamfu sana, sema hili jinni ndilo limeniharibia maisha yangu. Ningeweza kuliua ningeliua”
“Hata ukiliua utaondoka vipi hapa kisiwani?”
“Hayo yatakuwa masuala mengine, bora nimeshaliua”
“Kama boti yetu ingekuwa nzima tungekutorosha tukaenda Zanzibar”
“Halafu ungenioa huko huko”
“Upendavyo”
“Mimi ningependa unioe Zanzibar. Gharama zote angetoa baba yangu”
“Mimi nisingekuwa na amri zaidi ya kukusikiliza wewe”
Nilipomwambia hivyo Yasmin alifurahi sana. Chakula kilipokuwa tayari alikipekua sehemu mbili. Sehemu moja ilikuwa yetu mimi na yeye. Sehemu ya pili ilikuwa ya wenzetu.
“Sasa wapelekee halafu urudi tuje tule” Yasmin akaniambia.
Alinitilia chakula kwenye kapu nikaondoka. Wakati nakaribia kufika kwenye mlango wa kutokea, nikawaona wenzangu wamenifuata.
“Tumeona unachelewa, tukapata wasiwasi” Masudi akaniambia.
“Nilikuwa nasubiri chakula na ndicho hiki ninawaletea” nikamwambia Masudi.
“Sasa na sisi tumeshakuja. Kuna haja ya kwenda tena kule”
“Tunaweza kula hapa hapa”
Masudi akawatazama wenzake.
“Jamani tuleni hapa hapa, au mnasemaje?’ akawauliza.
“Popote tu tunaweza kula”
Nikarudi ndani na kuliweka lile kapu la chakula.
Yasmin alikuwa amesikia sauti zetu akatufuata.
“Jamani mmekuja huku huku?” akawauliza.
“Tuliona mwenzetu anachelewa tukapata wasiwasi. Tulidhani labda ameshikwa na Harishi” Masudi akamjibu.
“Hapana. Alikuwa anasubiri chakula, lakini mnaweza kula hapa hapa”
Yasmin akaandaa kile chakula kwenye mswala. Kwa vile wenzetu walikuwa wamekuja, tuliona tule pamoja. Yasmin akaleta na kile chakula kingine.
Tulipomaliza kula tuliendelea kuzungumza pale pale tukiwa pamoja na Yasmin.
Masudi alikuwa akimtania sana Yasmin huku akimsifia kwa uzuri. Yasmin alikuwa akichekacheka tu na kuficha uso wake uliokuwa umejaa aibu.
Masudi akaeleza kisa ambacho nilihisi kilikuwa cha uongo kwamba zamani alipokuwa anakaa Mombasa alipendana na msichana mmoja wa Kilamu.
“Msichana. Alikuwa mzuri huyo. Alinipenda na mimi nilimpenda lakini wanawake wa Mombasa hawaoleki bwana!”
“Kwanini?” nikamuuliza.
Wana gharama sana. Huyo msichana wangu alikuwa anaitwa Nargisi. Kila siku alikuwa amechorwa piku, utadhania mwari wa harusi”
“Sasa huyo atapata kweli muda wa kupika ukimuoa?” nikamuuliza.
“Ndio maana nilishindwa kumuoa. Nilikuwa nikijiambia huyu msichana sijamuoa yuko hivi, je nikimuoa atakuwaje, piku kila siku…safari haziishi”
“Mapenzi ya kweli yana gharama” Yasmin akamwambia.
“Ni kweli lakini gharama ya mwanamke wa Mombasa ni kubwa. Kwanza kuna ile gharama ya miraa. Kila siku ni lazima umnunulie kilo moja ya miraa, tena ile miraa safi ya bei ghali”
“Wacha we!” Yasmin alimwambia kumtia jazba.
“Halafu wakati wa kula ile miraa ni lazima apate kokakola na chupa ya maji safi pamoja na mfuko mzima wa Big G. Zote ni pesa” Masudi aliendelea kueleza.
“Na wewe ulikuwa unakula?” nikamuuliza.
“Mimi nilikuwa nakula lakini si sana. Simalizi hata nusu lakini mwenzangu anaua kilo nzima. Akianza saa tisa hadi saa nne usiku hakuna kitu”
“Sasa akishakula hiyo miraa itamsaidia nini?” Yasmin akauliza.
“Anapata handasi” Masudi akamjibu.
“Handasi ni kitu gani?”
“Handasi ni kileo cha miraa. Wengine wanakiongezea na kungumanga. Wanasaga kungumanga, ule unga wake wanachanganya na kahawa. Ashiki yake ni hatari!”
Sote tukacheka. Yasmin ndio alicheka sana.
“Yaani mwanamke akitoka hapo ni lazima apate bwana!” Masudi aliendelea.
“Asipopata bwana inakuwaje?” Yasmin akamuuliza.
“Yaani anapokula miraa na kuchanganya na kahawa ya kungumanga tayari anakuwa na ahadi ya bwana”
“Kwa hiyo huyo mpenzi wako akishakula ndio mnakutana?’ Yasmin aliendelea kumuuliza. Maneno yalikuwa yamemkolea.
“Ndiyo maana yake”
“Unaonaje mapenzi yake?”
“Ni mapenzi adhimu. Sijapata kuona na sitamsahau yule msichana” Masudi kwa kutaka sifa aliongeza. “Na yeye pia hatanisahau kwani nilikuwa…mh!...hata havisemeki”
“Sema tu ulikuwaje?” Yasmin akamsisitizia.
“Mwenyewe alikuwa akiniambia penzi nililokuwa nikimpa hajalipata kwa mwanaume yeyote”
Hapo tulicheka tena. Lakini mimi nilicheka kwa kujua kuwa Masudi alikuwa akisema uongo kumfurahisha Yasmin. Na kwa kweli nilihisi alitaka kujipependekeza naye ili apendwe yeye.
“Sasa ilikuwaje mkaachana?’ nikamuuliza.
“Tuliachana baada ya mimi kurudi Unguja. Mama yangu aliniambia nirudi kwa sababu alikuwa akiishi peke yake”
“Baba yako alikuwa yuko wapi?” Yasmin akamuuliza.
“Alikuwa ameshakufa”
“Nani ambaye hajaoa katika nyinyi?”
Wenzangu wote walikuwa na wake zao isipokuwa mimi lakini Masudi alisema alioa kisha aliachana na mke wake. Nilichokuwa nakijua mimi ni kuwa Masudi alikuwa na mke wake.
Mimi nilioa nilipokuwa Dar Lakini mke wangu alifariki baada ya kuja Unguja. Na tangu wakati huo sijaoa tena.
Sikujua ni kwanini Yasmin alituuliza vile.
“Kwa hiyo wewe na Masudi ndio hamna wake?” Yasmin akaniuliza.
“Ninachojua mimi Masudi anaye mke” nilimwambia Yasmin.
Kauli ile ilimkera Masudi.
“Nina mke mimi?” Masudi akaniuliza kwa ukali kidogo.
“Unaye!” nikamwambia kwa mkazo.
“Mke si nilishamuacha?. Au wewe ulikuwa hujui?”
“Mimi najua watania tu lakini mke bado unaye”
“Basi na yaishe. Mimi niliuliza tu kutaka kujua. Kama unaye mke au huna hakuna tatizo” Yasmin akaingilia kati.
“Huyu bwana mdogo anapenda sana kuniingilia!” Masudi akaunguruma.
Nikaamua kunyamaza.
“Nimesema yaishe jamani. Ngoja tulete karata tucheze”
Yasmin alitumia hekima kuyageuza yale mazungumzo akaenda kuleta karata, tukawa tunacheza.
Nilimuona akiinama na kuushika mguu wa mwenzetu aliyemuua, akamburuza kuelekea kwenye mlango wa kutokea.
Mwenzangu alikuwa amebaki mvunguni akinitazama. Nikaufunga mlango taratibu, kisha nikarudi mle mvunguni.
“Mwenzetu ameuawa,” nikamwambia mwenzangu. “Harishi amemburuza na kutoka naye.”
“Alimuona wapi?”
“Mara ya kwanza aliingia ndani, wewe ulikuwa umelala. Akamsomba pale kwenye godoro na kutoka naye kwenda kumuua. Ndiyo pale ulipoamka.”
“Kumbe Yasmin alitaka tufe alipotuambia tulale?”
“Ni makosa yetu sisi. Yasmin alituambia tutoke alfajiri, sisi tumelala hadi sasa kumekucha.”
“Lakini ni kweli.”
Wakati tunazungumza kwenye mvungu, Yasmin akaingia.
Tulipoona miguu yake, tulitoka mvunguni.
“Jamani, niliwambia nini?” akatuuliza kwa kutaharuki.
Hakukuwa na aliyemjibu. Sote tulikuwa tumeshikwa na fadhaa.
“Si niliwambia mtoke alfajiri, mmelala hadi sasa wakati niliwambia kuwa Harishi atakuja leo?”
“Ni kweli ulituambia,” nikamkubalia.
“Sasa mbona hamkutoka alfajiri?”
“Tumepitiwa.”
“Mtanilaumu mimi bure, jamani!”
“Hatutakulaumu hata kidogo. Umetufanyia wema sana.”
“Harishi alikuja mapema sana, akaniambia anasikia harufu ya kimtuntu. Nikamwambia mtu ni mimi. Akaniambia, ‘Hebu ngoja.’ Akatoka kuja kuwatafuta.”
“Siku hizi atakuwa anakuja kila siku kwa sababu ameona anapata mlo anaoutaka. Ni lazima mjihadhari.”
“Mimi naona tuondoke tu humu ndani,” mwenzangu akasema kwa woga.
“Lakini amekwisha kwenda zake. Kwa leo hatarudi tena,” Yasmin akatuambia.
“Itabidi tuondoke tu,” mwenzangu alizidi kusisitiza.
“Kwani wenzenu wengine wako wapi?”
“Bado wamelala hadi sasa?” Yasmin akauliza kwa mshangao.
“Naona bado wamelala,” nikamjibu.
“Kumbe nyinyi hamuwezi kuamka alfajiri?”
“Tatizo ni kuwa usingizi wenyewe unakuja wakati wa alfajiri,” nikamwambia Yasmin.
“Basi ni balaa. Sasa itabidi usiku mwende mkalale sehemu nyingine, mjaribu bahati yenu.”
“Tutafanya hivyo.”
“Kuna nyumba nyingi hazina watu. Mnaweza kutafuta nyumba nzuri yenye vitanda, mfanye makazi yenu. Hapa mtakuwa mnakuja mchana tu, muda ambao nitawambia mimi.”
“Tumekuelewa, ngoja niwaamshe hawa mabwana.”
Tukatoka pamoja mle chumbani. Tulipotoka tukawaona wenzetu nao wametoka.
“Hivi ndivyo mnaamka, jamani?” Yasmin akawauliza.
“Dada yetu, si unajua usingizi hautabiriki?” Mtu mmoja akamjibu.
“Hamkumbuki jana niliwambiaje? Si niliwambia muamke alfajiri muondoke?” Yasmin akawauliza.
“Ni kweli ulituambia, lakini ndiyo tumepitiwa.”
“Shakiri ameuliwa leo na Harishi!” nikawaambia.
“Unasema kweli?” wakaniuliza kwa pamoja kwa mshangao.
“Ni kwa sababu ya kuchelewa kuamka. Sisi tumeponea chupuchupu baada ya kuingia mvunguni mwa kitanda.”
“Basi tutakwisha!”
“Yasmin ametupa wazo. Badala ya kulala hapa, tutafute nyumba nyingine tuweke makazi yetu. Hapa tutakuwa tunakuja kula chakula mchana, katika muda atakaotuambia Yasmin.”
“Hivyo itakuwa vizuri,” mmoja wa wenzetu hao akasema.
“Sasa mjitayarishe, ninaenda kuwaandalia chai,” Yasmin akatuambia.
Wakati Yasmin anakwenda jikoni, wenzetu wawili waliokuwa wamelala chumba cha pili, walivyokuwa hadi mwenzetu akauliwa, tukawaeleza.
Kwa kweli walipata hofu.
“Sasa tukishakunywa chai tutoke tukatafute hiyo nyumba,” nikawambia wenzangu.
Ilipofika saa nne, tayari tulikuwa tumeoga na kunywa chai. Tukamwambia Yasmin tunataka kwenda kutafuta nyumba ya kukaa kwa maana tayari tulishakuwa wakazi wa kisiwa kile na hatukuwa na matumaini ya kuondoka.
“Kwani mpaka mwende nyote?” Yasmin akaniuliza.
“Unataka twende wangapi?” nikamuuliza.
“Mnaweza kwenda wawili, wawili wabaki.”
Mimi na wenzangu tukatazamana, lakini sote tulionekana kutoliafiki wazo la Yasmin.
“Acha tu twende sote,” nikamwambia Yasmin.
“Basi ngoja niwasindikize, msiniache peke yangu.”
“Tukizunguka na wewe itakuwa vizuri,” nikamwambia.
“Kwanini?”
“Kwa sababu wewe ndiye mwenyeji wetu, utaweza kutuongoza vizuri.”
“Haya basi, twendeni.”
Tukatoka na Yasmin. Yasmin alikuwa akikijua vyema kisiwa hicho. Alituzungusha mitaa mbalimbali tukiangalia nyumba. Mwisho alitupeleka katika nyumba moja ambayo alituambia ilikuwa ya mtu mmoja tajiri wa kisiwa kile ambaye naye aliuawa na Harishi.
Ilikuwa nyumba nzuri, lakini ilikuwa imechakaa kwa vile haikuwa ikiishi watu. Tulipoingia ndani tulikuta mavumbi yalikuwa yameenea nyumba nzima.
Tukaanza kazi ya kuisafisha nyumba. Yasmin alitusaidia kufanya usafi. Ilikuwa kazi iliyotuchukua saa kadhaa.
Tulipomaliza, tulichota maji kwenye kisima, tukaoga, kisha tukapumzika. Hapo ndipo tulipoanza kugawana vyumba.
Nyumba yenyewe ilikuwa na vyumba vinne na sisi wenyewe tulikuwa wanne. Kila mmoja alijichagulia chumba chake alichokipenda. Tulifungua makabati, tukatoa mashuka na kutandika vitanda tulivyovikuta humo ndani.
Wakati ninatandika kitanda, Yasmin aliniambia nimpe shuka atandike yeye. Nikampa.
“Natamani sana ningekuwa hapa pamoja na nyinyi,” Yasmin akaniambia wakati anatandika.
“Ukiwa hapa utatuponza sote.”
“Ninasema tu, lakini najua haitawezekana. Unajua katika nyinyi nyote nimekupenda wewe zaidi. Ninatamani ungekuwa mume wangu.”
“Hata mimi natamani ungekuwa mke wangu, lakini ndiyo tupo jela. Uhai wetu unahisabika.”
“Ni kweli. Tusikumbushie hayo. Tuswali tuombe nusura itufikie.”
“Wewe unaswali?” nikamuuliza Yasmin.
“Ninaswali, lakini kwa siri sana. Harishi hataki niswali. Swala ndiyo inayonipa matumaini ya kuishi.”
“Umenikumbusha jambo zuri sana na sisi tutaanza kuswali.”
“Kila mara ninaota kuna mtu atakuja kumwangamiza Harishi na mtu huyo atakuwa mume wangu.”
“Mtu huyo atatokea wapi?”
“Sijui.”
“Mtu huyo atastahili kuwa mume wako kwa sababu atakuwa jabari sana atakayeweza kupambana na jini na kumwangamiza.”
“Usisahau kwamba majini yameumbwa kama sisi!”
“Ni kweli, Yasmin, sema tu yamepewa uwezo wa kutudhuru.”
Yasmin alikuwa amemaliza kutandika, akakaa kitandani na kuniita.
“Njoo tukae kidogo.”
Nikaenda kuketi naye.
“Kwa kweli, wewe ni mzuri na unapendeza sana. Sina la kusema,” nilimwambia Yasmin ambaye alitabasamu. Alipotabasamu, mashavu yake yaliunda vidimbwi.
Mara moja akainuka pale kwenye kitanda.
“Sasa ninaenda kupika. Tunaweza kwenda sote?”
“Twende na wenzetu?” nikamuuliza.
“Hapana. Wao waache hapa hapa. Twende mimi na wewe.”
“Una hakika kuwa nitakuwa salama?”
“Harishi hatakuja leo. Ameshakuja asubuhi, ni mpaka kesho.”
“Ngoja niwaage wenzangu.”
Tukatoka ukumbini. Wenzangu walikuwa wameketi wakizungumza. Nikawambia kuwa namsindikiza Yasmin.
“Ninakwenda kupika, nitampa chakula awaletee,” Yasmin akawambia.
“Yaani utasubiri chakula huko huko?” Mmoja akaniuliza, lakini uso wake haukuonesha furaha.
“Ndiyo, atakisubiri,” Yasmin akamjibu.
Masudi akawatazama wenzake kabla ya kuniambia.
“Sawa. Sisi tutasubiri.”
Jina lake lilikuwa Masudi. Katika sisi watu wanne tuliobaki, yeye alikuwa ndiye mkubwa kwetu kiumri.
Wakati mimi na Yasmin tunatoka kwenye ile nyumba tukirudi nyumbani kwa Yasmin, Yasmin aliniambia, “Yule kaka uliyezungumza naye anaitwa nani?”
“Anaitwa Masudi.”
“Naona kama hakufurahi ulivyomwambia tunatoka mimi na wewe.”
“Inawezekana, ni binadamu. Labda ameona tumewabagua.”
“Mbona wengine hawakusema kitu?”
“Kila mtu ana mawazo yake. Yule amezoea kutuamrisha kwa sababu kwenye kundi letu yeye ndiye mkubwa kiumri na amekuwa kama kiongozi wetu.”
“Kwa hiyo alitaka anisindikize yeye?”
Yasmin aliposema hivyo nilicheka, na yeye akacheka.
“Unafikiri nakutania?” aliponiuliza hivyo, alitaja jina langu.
“Hunitanii, unaniambia ukweli. Najua Masudi hakufurahi,” nikamwambia.
Pakapita kimya kifupi kabla ya Yasmin kuniambia.
“Kisiwa chote hiki kilikuwa kina watu.”
“Wewe uliwakuta hao watu?” nikamuuliza.
“Wakati Harishi ananileta hapa, alikuwa ameshamaliza watu wote. Wengine walihama wenyewe kukimbia kifo.”
“Na kama leo anakuja na kutukuta hivi, itakuwaje?”
“Atakukamata wewe. Atakufyonza damu na ndiyo ataniuliza wewe ni nani na ulifuata nini hapa.”
“Ina maana wewe hatakuadhibu?”
“Ananitisha tu pale ninapomuudhi, lakini kama atanikuta na mwanaume, nadhani ataniadhibu.”