Arsenal haijasajili mashine ya kushoto, lakini kulia pa moto
Muktasari:
- Ni timu chache zitakazowahurumia. Wapinzani waliotumia mamia ya mamilioni ya shilingi msimu huu wakijaribu kurejea kwenye ushindani wa juu hawatataka kusikia malalamiko kuhusu jinsi mabingwa hao walivyopata shida kupata wachezaji ambao wangeboresha kikosi cha kwanza.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL kwa mbali ndiyo timu inayotegemea zaidi upande wa kulia inapofika kwenye namna inavyoshambulia katika Ligi Kuu England.
Je? Ni kweli wanahitaji kusajili winga wa kushoto wa kiwango cha dunia? Tatizo la kuwa bora kama Arsenal ni kwamba inapofika kwenye soko la usajili inakuwa vigumu kuimarika zaidi.
Ni timu chache zitakazowahurumia. Wapinzani waliotumia mamia ya mamilioni ya shilingi msimu huu wakijaribu kurejea kwenye ushindani wa juu hawatataka kusikia malalamiko kuhusu jinsi mabingwa hao walivyopata shida kupata wachezaji ambao wangeboresha kikosi cha kwanza.
Arsenal ilimsajili Christos Tzolis, Ezri Konsa na Bruno Guimaraes, ambao kila mmoja tayari amechangia kwa namna kubwa tangu walipotua msimu huu. Hata hivyo, wakati Tzolis ameingia vizuri kwenye nafasi ya winga wa kushoto, alikuwa mchezaji asiyejulikana sana alipowasili, na bado hajathibitisha uwezo wake kwa kipindi cha kutosha katika kiwango cha Ligi Kuu England, ingawa dalili za awali zinaonyesha mambo mazuri.
Hilo lilimaanisha kwamba Leandro Trossard na Gabriel Martinelli walipoondoka, sehemu kubwa ya simulizi vijiweni kuhusu usajili wa Arsenal ilikuwa ni kuhusu kushindwa kwao kumpata nyota bora wa kucheza upande wa kushoto.
HAWA WALIPEPERUKA, LAKINI...
Kulikuwa na taarifa kuhusu mpango wa kumsajili Vinicius Junior; kuhusu kushindwa kumudu gharama za Morgan Rogers na Bradley Barcola ambao wote walihamia kwa wapinzani wao Ligi Kuu England, na kuhusu kuendelea kwa muda mrefu na matumaini ya kumsajili Julian Álvarez, ingawa siyo winga wa kushoto na huenda hata asingekuwa amecheza nafasi hiyo Arsenal kama angesajiliwa.
Mwishowe, kwa mtazamo wa wengi, Arsenal ilibaki bila mchezaji mkali katika eneo hilo, na kama ingeyumba msimu huu, kushindwa kusajili mshambuliaji wa kiwango cha dunia upande wa kushoto ingekuwa miongoni mwa sababu zinazotajwa katika tathmini mbalimbali mitandaoni.
Lakini, Arsenal ilikuwa imetwaa ubingwa bila, na pengine unaweza kukubaliana kuwa na mshambuliaji wa kiwango cha dunia upande wa kushoto. Martinelli na Trossard ni washambuliaji wazuri, wanaostahili kupewa majukumu makubwa na kutoa mchango muhimu kwa mabingwa hao, lakini hawakuwa kiini cha mashambulizi ya Arsenal.
KULIA PA MOTO
Lakini, Arsenal ilishambulia kupitia upande wa kushoto kwa kiwango kidogo msimu uliopita kuliko timu nyingine yoyote katika Ligi Kuu England, huku asilimia 31.8 pekee ya miguso katika nusu ya uwanja ya wapinzani ikitokea kwenye theluthi ya kushoto ya uwanja.
Upande mwingine, tayari wana nyota matata Bukayo Saka, ambaye wamejenga mashambulizi yao kumzunguka kwa miaka kadhaa. Haikuwa jambo la kushangaza kwamba msimu uliopita walikuwa na asilimia 41.7 ya miguso katika nusu ya uwanja ya mashambulizi kupitia upande wa kulia. Ni West Ham pekee iliyotumia zaidi upande huo, na yenyewe ilikuwa na mchezaji muhimu wa aina hiyo katika upande huo, Jarrod Bowen.
Hata hivyo, jambo hili halikutokana na Saka pekee, kwani alikosa sehemu ya msimu uliopita kutokana na majeraha na Arsenal haikubadilisha namna ilivyocheza alipokuwa nje. Upande wa kulia ukiwa na Noni Madueke au Max Dowman akicheza winga, bado ulikuwa kiini cha mashambulizi ya timu.
Lakini kwa Saka kuwa fiti kwa asilimia 100 tena na kuonekana kurejea katika kiwango chake bora msimu huu, Arsenal imezidisha zaidi matumizi ya upande wa kulia. Katika mechi tatu za Ligi Kuu England hadi sasa, wamekuwa na asilimia 47.5 ya miguso yao ya mashambulizi kupitia upande wa kulia, huku asilimia 27.4 pekee ikiwa upande wa kushoto. Labda bila ya kushangaza, hizo ndizo asilimia za juu na za chini zaidi kwa mtiririko huo miongoni mwa timu zote za Ligi Kuu England msimu huu, na tofauti ni kubwa.
Na sasa ni dhahiri kwamba wanategemea zaidi upande huo. Katika mchezo dhidi ya Chelsea wiki iliyopita, Kai Havertz alihamia mara kwa mara upande wa kulia kusaidia kuongeza idadi ya wachezaji katika eneo hilo, mara nyingi akichukua nafasi iliyokuwa pana zaidi hata kuliko Saka. Ilikuwa ni kutoka eneo hilo alipohamia katikati na kufunga bao la kusawazisha la Arsenal.
Na katika ushindi wa Jumatano usiku dhidi ya Napoli katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Martin Odegaard wakati mwingine alionekana kama anacheza winga wa kulia; yeye na Saka walipokezana pasi mara nyingi zaidi kuliko walivyofanya na mchezaji mwenzao mwingine yeyote.
Mtandao wa pasi wa Arsenal katika mchezo huo unaonyesha wazi ni kwa kiasi gani walihamisha mpira kwenda upande wao wa kulia, na walikuwa na ufanisi mkubwa wakizalisha jumla yao kubwa zaidi ya mabao yanayotarajiwa (xG), 4.05, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu rekodi hizo zianze kutunzwa msimu wa 2012-13. Walistahili kushinda kwa tofauti kubwa zaidi ya bao moja.
Hata Tzolis, aliyeingia kutoka benchi, alijitokeza upande wa kulia, akihamia huko kusaidia kukamilisha mfululizo wa pasi 29 kwa kutoa pasi ya mwisho iliyomwezesha Odegaard kufunga bao la ushindi.
Ni muhimu kutambua kwamba, Saka alikuwa angalau sehemu ya sababu iliyofanya Arsenal ishambulie sana kupitia upande wa kulia, lakini bao hilo lilifungwa baada ya kutolewa uwanjani. Kama ilivyokuwa alipokosekana msimu uliopita, Arsenal haikubadilisha mfumo wake bila yeye.
KUSHOTO PIA
Siyo kwamba Arsenal hawana tishio pia upande wa kushoto, kwani Tzolis sasa ana pasi nne za mabao katika mechi zake tano za kwanza za mashindano akiwa Arsenal, huku beki wa kushoto Riccardo Calafiori akiwa kivutio kikubwa kutokana na jukumu lake jipya la kushambulia.
Mara nyingi anaingia ndani ya Tzolis ili kushambulia eneo la hatari na karibu kuwa kama mshambuliaji wa kati pale Havertz anapotoka kwenye nafasi yake. Ni Havertz na Saka pekee waliokimbia bila mpira kwa kasi kubwa na kufikia eneo la penalti mara nyingi zaidi ya Calafiori (mara nane) katika mechi za Ligi Kuu England akiwa Arsenal msimu huu.
NAMBA SASA
Muitaliano huyo pia ana pasi mbili za mabao, maana yake Tzolis na Calafiori, wanaounda upande wa kushoto wa Arsenal wamechangia pasi sita kati ya tisa za mabao ambazo wachezaji wa Arsenal wamezitoa katika mashindano yote msimu huu.
Lakini, wao siyo kiini cha ubora wa Arsenal. Calafiori ana wastani wa miguso 39.6 kwa kila dakika 90 katika mashindano yote msimu huu, ikiwa ni idadi ya nne kwa uchache miongoni mwa wachezaji wote wa Arsenal, nyuma ya kipa David Raya (38.8) na washambuliaji Havertz (35.7) na Viktor Gyokeres (15.3). Tzolis yupo mbele kidogo akiwa na wastani wa miguso 52.9 kwa kila dakika 90.
Wakati huohuo, beki wa kulia Ben White amekuwa bora sana, baada ya msimu uliokuwa na taarifa mbalimbali kuhusu uwezekano wa Arsenal kutaka kumsajili mbadala wake. Amekuwa akihusika sana kwenye matukio akiwa mmoja wa wachezaji wanne pekee walioanza mechi zote tano hadi sasa, huku akiwa na wastani wa miguso 68.4 kwa kila dakika 90 ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuliko Calafiori upande wa kushoto.
Sehemu kubwa zaidi ya mashambulizi ya Arsenal inatokea upande wa kulia ikilinganishwa na upande wa kushoto. Na mfumo huo umekuwa na ufanisi mkubwa, kwani Arsenal imeshinda mechi zote tano ilizocheza kwa jumla ya mabao 10-1. Chelsea ndiyo timu pekee ambayo imewasumbua au kuonekana wakati wowote kuwa inaweza kuwafunga.
HAYA HAPA MASWALI
Lakini, mkazo wa Arsenal kwenye upande wa kulia unazua maswali. Kwanza, je, kuna dalili za kuwategemea zaidi waliopo huko? Ikiwa mpinzani akiufunga upande huo, Arsenal itapata shida kutafuta njia ya kupenya? Hilo bado halijaonekana kwa sababu wamekuwa bora dhidi ya kila mpinzani, jambo ambalo linaonyesha kuwa mfumo huo unaweza kutosha kuwasaidia kutimiza malengo yao yote msimu huu.
Pili, nini kitatokea ikiwa au pale mchezaji muhimu wa upande wao wa kulia atakosekana kwa muda kutokana na majeraha? Arsenal ilionekana kuwa na ufanisi mdogo katika mchezo wa wazi Saka alipokosekana msimu uliopita, wakati Odegaard anaonekana kuwa sehemu muhimu na amekuwa na changamoto ya majeraha katika miaka michache iliyopita. Hilo ni jambo ambalo halijibiki sasa, ingawa linaweza kuwaletea matatizo.
Lakini mwisho, na labda jambo muhimu zaidi kutokana na usajili wa msimu huu, je, wangekuwa bora zaidi ikiwa wangekuwa na winga matata mwenye jina kubwa upande wa kushoto? Mchezaji kama Vinícius, kwa mfano, asingefurahia kucheza pembeni asiyepewa kipaumbele. Angetaka kucheza kushoto na angehitaji mpira umfikie kila anapopata nafasi. Uwepo wake bila shaka ungebadilisha namna Arsenal inavyocheza.
Na mbali na kuwa wa gharama nafuu zaidi, Tzolis anafanya kazi nzuri hadi sasa, akiutendea haki upana wa uwanja ili kuinyosha safu ya ulinzi ya wapinzani, huku akitoa pasi za mwisho zenye madhara pale anapohusika kwa ufanisi zaidi kuliko mchezaji mwingine yeyote katika timu.
Je atadumisha kiwango chake cha sasa kwa msimu mzima na kikosi kinapokuwa na mzigo mkubwa wa mechi? Hilo huenda asionekane kuwa nalo na hasa kuwa na utulivu huohuo kadri miezi inavyosonga.
Lakini bahati nzuri ni kwamba Arsenal ina ubora upande mwingine, hivyo huenda hilo lisiwe tatizo. Kwa baadhi ya watu, dirisha la usajili la Arsenal lilionekana kuwa la kukatisha tamaa kwa sababu hawakutumia kiasi kikubwa cha fedha kusajili winga nyota wa kushoto, lakini kutokana na ushahidi wa awali wa mwanzo wao wa msimu unaoegemea zaidi upande wa kulia, huenda Arsenal ikawa katika nafasi nzuri zaidi kwa kufanya kweli.