Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Baby mama wa Henry, Rajacic ni nani hasa?

Muktasari:

  • Henry ambaye aliifungia timu ya taifa ya Ufaransa magoli 51 katika michezo 123, uhusiano wake na Rajacic ulikuja baada ya kuvunjika kwa ndoa yake na aliyekuwa mkewe mwanamitindo Claire Merry.

Mchezaji wa zamani wa Arsenal na Barcelona, Thierry Henry tayari ni baba wa watoto wanne kutoka kwa wanawake wawili tofauti akiwemo mpenzi wake wa sasa, Andrea Rajacic ambaye wamekuwa pamoja kwa muda mrefu.


Henry ambaye aliifungia timu ya taifa ya Ufaransa magoli 51 katika michezo 123, uhusiano wake na Rajacic ulikuja baada ya kuvunjika kwa ndoa yake na aliyekuwa mkewe mwanamitindo Claire Merry.

Ndoa kati ya Henry na Claire ilifungwa Julai 5, 2003 katika kasri la Highclere Castle, na kufikia Mei 2005 wakajaliwa mtoto wao wa kwanza, Tea, mrembo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 21.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya Henry kuhamia Barcelona, ripoti zilitoka zikieleza kuwa wawili hao wapo katika mchakato wa kupeana talaka, mchakato uliokamilika Desemba 2008, huku mchezaji huyo akimlipa mtalaka wake takribani Pauni 10 milioni.

Kuanzia hapo, Henry akawa ameufunga ukurasa wa Claire, na ukawa mwanzo wa penzi la Rajacic, uhusiano ambao leo tunaenda kuutazama kwa mapana yake kama ifuatavyo.

Uhusiano wa Henry na Rajacic umekuwepo kwa miaka zaidi ya 16 ambapo moja ya matukio yao ya awali kuonekana hadharani pamoja ilikuwa Februari 2010 walipohudhuria majaribio ya magari ya Formula One jijini Barcelona.

Miezi michache baadaye, Rajacic alisafiri hadi Afrika Kusini kwa ajili ya kumsapoti Henry na timu ya taifa ya Ufaransa katika michuano ya Kombe la Dunia la FIFA ambayo ilifanyika Afrika kwa mara ya kwanza.

Kwa mujibu wa taarifa zake katika mtandao wa LinkedIn, Rajacic ambaye ni raia wa Bosnia alisomea Usimamizi wa Biashara katika Chuo Kikuu cha Mary Washington huko Fredericksburg, Virginia kati ya mwaka 2003 hadi 2007 alipohitimu ngazi ya shahada.

Baadaye kuanzia mwaka 2009 hadi 2010, alisoma lugha ya Kihispania katika shule ya biashara na sheria iliyopo Barcelona, Esade. Hata hivyo, kabla ya kujiunga na Esade, Rajacic aliishi New York ambako alifanya kazi ya mauzo katika kampuni ya Milk Studios.

Kwa miaka mingi Henry amekuwa akiposti baadhi ya picha na taarifa kuhusu uhusiano wao kwenye mitandao ya kijamii, kwa mfano Januari 2026 kupitia Instagram alimuita Rajacic 'partner in crime', akimaanisha mwenza wake wa karibu zaidi katika maisha.

Wawili hao walijaliwa kupata mtoto wao wa kwanza Agosti 2012, na kumpa jina la Tristan, kisha walifuata wengine wawili ambao ni Tatiana aliyezaliwa Agosti 2015, na Gabriel aliyezaliwa Novemba 2016.

Miezi michache baada ya kuzaliwa kwa Tristan, Rajacic alizungumza na kampuni inayotoa huduma ya malezi kwa watoto ya Romy and the Bunnies na kumtaja mtoto huyo kama mwanga wa maisha yake.

“Kuishi kila siku nikimsaidia kugundua dunia inayomzunguka na kuiona kupitia macho yake, kunaifanya siku yangu kuwa nzuri. Anajifunza vitu kwa haraka sana, na ni jambo la kushangaza kuona furaha yake katika vitu vya kawaida kabisa,” alisema Rajacic.

Kwa upande wa Henry, katika mahojiano na Podcast ya The Diary of a C.E.O hapo Januari 2024, alisema watoto wake ndio huwa wanamfanya ajisikie vizuri pale anapokuwa na msongo wa mawazo.

“Watoto wangu wananiokoa na msongo wa mawazo. Wananiokoa kwa sababu kila siku naona kitu kipya kwao. Wananifundisha kuwa baba bora... Wananifungulia milango ambayo sikujua namna ya kuifungua," alisema Henry.

Naye Rajacic alizungumzia namna ambavyo Henry amekuwa akimsaidia katika malezi ya watoto wao akisema ni bahati kuwa na mtu wa namna hiyo.

“Nina bahati sana kuwa na mtu ambaye ni baba anayeshiriki kikamilifu katika malezi, na anayeniunga mkono kwa kunisaidia katika kila hali," alisema Rajacic wakati akizungumza na Romy and the Bunnies.

Katika mahojiano na gazeti la Uingereza la The Times mnamo Juni 2024, Henry ambaye kwa sasa ni mchambuzi soka alisema baada ya kuishi miji mbalimbali kutokana na kazi yake, sasa nyumbani kwake ni pale familia yake ilipo - hana mji maalum.

“Mtazamo wangu ulibadilika baada ya kupata watoto. Unajua unapoanzisha familia, nyumbani kwako ni pale familia yako ilipo. Nina watoto watatu waliozaliwa London, mmoja alizaliwa New York, hivyo sasa familia yangu ndiyo itakayoamua nyumbani ni wapi,” alisema Henry.

Mei 10, 2026, katika siku ya kina mama duniani, Henry aliposti picha kadhaa za familia yake Instagram akimtakia Rajacic heri ya siku hiyo pamoja na kumshukuru.

“Heri ya siku ya kina mama, asante kwa sapoti, mwongozo na upendo wako usio na masharti. wewe ndiye nguzo yetu!” aliandika Henry katika post hiyo katika ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi (followers) zaidi ya milioni 6.

Na licha ya Rajacic kupenda kuishi maisha ya faragha, hilo halimzuii kuongozana na Henry katika matukio muhimu, mathalani alikuwa naye katika hafla ya tuzo za GQ Men of the Year mnamo Novemba 2024, na takribani miezi miwili baadaye walipita wote juu ya zulia jekundu la tuzo za Joy zilizofanyika mjini Riyadh, Saudi Arabia.