El Clasico; Real Madrid ilivyoifunua Barcelona sebuleni
Muktasari:
- Awali, Barcelona ilitarajiwa kutawala mchezo huo kwa kiwango kikubwa Badala yake, Real Madrid ilikuwa timu bora kuanzia mwanzo katika pambano hilo ilkidhibiti mchezo na kupata bao la kuongoza mwishoni mwa kipindi cha kwanza, wakati Kylian Mbappa alipokuwa mahali sahihi kwa wakati sahihi. Mpira uliotolewa ovyo na Gerard Martín ulimpiga Mfaransa huyo na kuingia wavuni.
BARCELONA, HISPANIA:JANA, ule mfululizo wa ushindi wa Barcelona katika Ligi Kuu Hispania (La Laga) msimu huu ulimalizwa na wapinzani wao, Barcelona, baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 nyumbani kupitia supastaa wa kimataifa wa Ufaransa, Kylian Mbappe aliyetupia yote mawili ilhali moja la wenyeji likifungwa na Raphinha Dias.
Lakini, wakati na baada ya kipute hicho kuna mambo kibao yalijiri na haya hapa ni matano yaliyofichua udhaifu wa Barcelona. Kimsingi Real Madrid ilipuuza utabiri wa kabla ya mchezo na kuibuka na ushindi wa haki kwenye Uwanja wa Camp Nou ukiwa ni wa kwanza wa El Clasico msimu huu.
Awali, Barcelona ilitarajiwa kutawala mchezo huo kwa kiwango kikubwa Badala yake, Real Madrid ilikuwa timu bora kuanzia mwanzo katika pambano hilo ilkidhibiti mchezo na kupata bao la kuongoza mwishoni mwa kipindi cha kwanza, wakati Kylian Mbappa alipokuwa mahali sahihi kwa wakati sahihi. Mpira uliotolewa ovyo na Gerard Martín ulimpiga Mfaransa huyo na kuingia wavuni.
Ingawa Barcelona iliboresha mchezo kipindi cha pili na kusawazisha kupitia Raphinha, aliyefunga bao lake la 13 la msimu katika La Liga kwa pasi nzuri ya Pedri, kikosi cha Hansi Flick kilikuwa mbali na kiwango chake bora. Wakati ilipoonekana El Clasico ingeisha kwa sare, Eduardo Camavinga alifanya shambulizi zuri na kumpasia Mbappe aliyefunga bao la pili likiwa lake la 100 akiwa na Real Madrid.
Huo ulikuwa ushindi wenye ujumbe mzito kutoka kwa kikosi cha Jose Mourinho. Real Madrid ilistahili ushindi huo, ikiwa ni timu inayozidi kuimarika, huku Barcelona ikipata kipigo cha ajabu. Haya hapa mambo matano kutokana na matokeo hayo yasiyotarajiwa.
JOSE AONYESHA UMAHIRI, MBINU
Real Madrid ilicheza mchezo wake bora zaidi msimu huu, na Mourinho alipanga kikosi vyema sambamba na jinsi wachezaji wake walivyoonekana kujiandaa kwa kiwango cha juu.
Kwa waliotarajia kwamba angerejea katika mbinu za zamani kujilinda kwa nguvu na kuzuia mashambulizi ya wapinzani kwenye Uwanja wa Camp Nou walikosea.
Kama ilivyokuwa kwa PSG katikati ya wiki, Real Madrid ilicheza vyema na mara nyingi iliwasukuma Barcelona katika eneo lao la ulinzi ikiwalazimisha kufanya makosa.
Zaidi ya hapo, Real Madrid ilipanga wachezaji wake kumfuatilia kila mchezaji wa Barcelona katika maeneo mbalimbali ya uwanja. Kila mchezaji alikuwa tayari kumkaba mpinzani wake kwa kasi na bila kuchoka.
Barcelona ilipofanikiwa kumiliki mpira kwa muda mrefu, Los Blancos ilishuka na kutumia mfumo wa ulinzi wa 4-1-4-1 katika eneo la katikati.
Jude Bellingham alipewa jukumu la kumuwekea presha Rodri, jambo lililomfanya kiungo huyo ambaye kwa kawaida huwa mahiri katika kupanga mashambulizi akiwa nyuma ashindwe kucheza kwa uhuru.
Kuchezeshwa kwa Bernardo Silva katika eneo la kiungo pia kulionyesha kuwa Madrid ilitaka kuongeza udhibiti wa mpira ilipokuwa ikishambulia.
Nyota huyo wa Ureno alikumbana na changamoto wakati timu yake ilipokuwa haina mpira, lakini alipoupata alicheza vizuri. Vilevile uwepo wake ulipunguza majukumu ya Aurelien Tchouameni wakati Madrid ilipomiliki mpira.
Mfaransa huyo naye alicheza kwa kiwango cha juu, lakini Silva alikuwa muhimu katika kutekeleza mpango wa mashambulizi wa Madrid akitumia haraka nafasi zinazopatikana baada ya kupora mpira kutoka kwa wapinzani.
Pasi ndefu nzuri ya Silva ndiyo iliyoanzisha shambulizi lililozaa bao la kwanza, baada ya Los Blancos kumiliki mpira kwa muda mrefu. Tangu mwanzo, Real Madrid ilikuwa na kasi kubwa zaidi kuliko Barcelona, ikiikimbiza na kuizidi nguvu timu hiyo.
Hiyo ni sifa inayotambulika katika mbinu za zamani za Mourinho. Kwa mpango mzuri wa kiufundi na ari ya kupambana, El Clasico ilichezwa kwa namna Mourinho alivyotaka.
Katika kurejea kwake kwenye El Clasico iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa, Mourinho alimzidi maarifa Hans Flick na kumpa kocha huyo Mjerumani kipigo chake cha kwanza cha nyumbani katika pambano hili la kihistoria.
Rekodi ya Mourinho ya kutopoteza katika mechi za El Clasico iliyoanzia kipindi chake cha awali cha kuinoa Real Madrid, sasa imefikia mechi sita mfululizo, akiwa ameshinda nne na kutoka sare mbili.
Mourinho ni kocha wa tatu wa Los Blancos kufikia rekodi hiyo, baada ya Miguel Munoz aliyefanya hivyo kati ya 1962 na 1965, na Vicente del Bosque 2001 na 2003. Makocha hao wawili kila mmoja aliweka rekodi ya mechi saba mfululizo bila kupoteza katika El Clasico.
MBAPPE AMEIGEUZA BARCA MTEJA WAKE
Hakuna namna nyingine ya kulieleza jambo hili; Kylian Mbappa ameifanya Barcelona kuwa mmoja wa wapinzani anaowatesa zaidi, kwani akiwa kwenye Uwanja wa Camp Nou, Mfaransa huyo ni kama amehakikisha kuwa atafunga mabao. Bao lake la kwanza huenda lilipatikana kwa bahati, na la ushindi lilikuwa mguso rahisi kwa kuingiza mpira wavuni, lakini mabao yote yana thamani sawa.
Mbappe sasa amefunga mabao 14 dhidi ya Barcelona katika maisha yake ya soka, huku 11 kati ya hayo akifunga kwenye Uwanja wa Camp Nou. Pia amefunga manane katika mechi saba za kwanza za El Clasico. Mfaransa huyo sasa amefunga mabao mawili katika mechi moja mara mbili ndani ya mechi zake tano za El Clasico katika La Liga.
Tayari amefanya hivyo mara nyingi zaidi kuliko Cristiano Ronaldo na Karim Benzema walivyofanya katika maisha yao ya soka. Awali, ubora wa Mbappe haukuwa ukitosha kuipa Real Madrid ushindi, kwani Los Blancos ilikuwa ikitawaliwa na Barcelona katika mechi za hivi karibuni.
Kwa upande mwingine, winga wa Barcelona na mpinzani wa Mbappe katika La Liga, Lamine Yamal alishindwa kutengeneza nafasi hata moja ya kufunga kwa wenzake na alikamilisha asilimia 76.6 ya pasi akifanikiwa kupiga 47 kati ya 76.
CUCURELLA, WENZAKE WALIMNYAMAZISHA
“Nitammeza mzima,” hayo ndiyo maneno ambayo Yamal alitumia kueleza alichopanga kumfanyia Marc Cucurella kabla ya beki huyo wa pembeni kucheza El Clasico yake ya kwanza. Lakini mwishoni ni beki huyo mwenye nywele za kujikunja aliyemzidi Yamal na kumdhibiti kabisa.
Katika moja ya mapambano ya ana kwa ana yaliyokuwa na mvuto mkubwa uwanjani, Cucurella alimuwekea Yamal presha kwa kiwango ambacho mabeki wachache wa kushoto wameweza kufanya. Tangu mchezo ulipoanza alihakikisha anakuwa karibu na Yamal akitumia nguvu kumzuia, akimgusa mara kwa mara na hata kumchezea faulo ili kumvuruga.
Yamal alionekana kukerwa na hali hiyo na kukosa uhuru wa kucheza tangu mwanzo, Cucurella akimzidi katika karibu kila hatua ya mchezo.
Baada ya kipindi cha kwanza kibovu, kilichofikia kilele pale Yamal alipokosa nafasi ya wazi akiwa karibu na lango, nyota huyo alitumia sehemu kubwa ya kipindi cha pili akihama kuelekea katikati ya uwanja ili kujiepusha na udhibiti wa Cucurella. Ingawa alionyesha dalili chache za ubora kwa ujumla ilikuwa El Clasico isiyovutia kutoka kwake.
Kwa upande mwingine, Cucurella alimaliza mchezo akiwa amefanya vitendo 12 muhimu vya ulinzi, huku akipitwa na mpinzani katika kumiliki mpira kwa chenga mara moja pekee.
Msimu uliopita, Cucurella alimnyamazisha Yamal wakati Chelsea ilipoichakaza Barcelona kwa mabao 3-0 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Takribani miezi 11 baadaye, beki huyo wa kushoto amerudia jambo hilo na kudhibiti kwa kiwango cha juu tishio kubwa zaidi la Barcelona.
BARCA IIMARISHE SAFU YA ULINZI
Kuna mambo mengi yaliyoiathiri Barcelona katika mchezo ambao bila shaka ulikuwa mbaya zaidi kwake msimu huu. Mtiririko wa pasi ulikuwa wa polepole, washambuliaji wake walidhibitiwa kwa kiasi kikubwa huku wakipoteza nafasi za kufunga ilhali timu nzima ilionekana kutokuwa na mpangilio na mara kwa mara ilipoteza mpira katika maeneo hatari.
Lakini, jambo kubwa lililosababisha anguko lilikuwa, kwa mara nyingine tena, safu yake ya ulinzi yenye upungufu ambayo imekuwa ikianikwa hadharani mara nyingi katika misimu mitatu iliyopita.
Hata Barcelona ilipoonekana kuanza kuudhibiti mchezo baada ya kupata bao la kusawazisha, bado kulikuwa na hisia kwamba Real Madrid ingeweza kufunga wakati wowote.
Camavinga alimpita Pau Cubarsi katika hatua iliyozaa bao la ushindi la Madrid kana kwamba beki huyo hakuwepo uwanjani.
Cubarsi amekuwa akicheza vizuri tangu Kombe la Dunia 2026, lakini alikumbana na matatizo makubwa dhidi ya PSG na tena katika El Clasico. Hata hivyo, kama Cubarsi alivyokuwa na wakati mgumu swahiba wake, Gerard Martin, alikuwa mbaya zaidi.
Martín, ambaye alibadilishwa kutoka nafasi yake ya awali na kuanza kucheza beki wa kushoto, amekuwa akionyesha kiwango kizuri. Lakini, ni wazi kwa karibu kila mtu isipokuwa Flick kwamba Barcelona inahitaji mchezaji bora zaidi katika nafasi hiyo.
Jaribio lake la kuondoa mpira lililoishia kwa Mbappe kufunga bao la kwanza lilikuwa kosa kubwa na la aibu. Mbali na mabeki hao wawili wa kati, safu nzima ya ulinzi ya Barcelona inaonekana kuyumba, inaweza kupenywa kwa urahisi na imeshindwa kuleta hali ya kujiamini.
Kwa hiyo, haipaswi kushangaza kuona Barcelona ikiwa na udhaifu uleule wa ulinzi iliokuwa nao msimu uliopita, kwa sababu ni kundi lilelile la wachezaji. Kipigo cha juzi na kile cha PSG katika wiki hiyo kinaibua maswali makubwa kuhusu Flick na mipango ya usajili ya Barcelona katika kipindi cha majira ya joto.
Kwa msimu wa pili mfululizo, klabu hiyo imeamua kupuuza kabisa juhudi za kutatua matatizo ya ulinzi ambayo yamekuwa yakiisumbua kwa miaka miwili iliyopita. Isiporekebisha makosa yake na au kusajili beki wa kiwango cha juu katika dirisha la usajili la Januari, ni vigumu kuona tatizo hilo likiisha.
Barcelona itaendelea kuanikwa udhaifu wake kila inapokutana na wapinzani wenye nguvu.
MBIO ZA UBINGWA LA LIGA MBICHI
Kama Barcelona ingeshinda, Real Madrid ingebaki nyuma kwa pointi tisa kwenye msimamo wa ligi na hilo lisingemaliza moja kwa moja matumaini ya Madrid ya kutwaa ubingwa wa La Liga, lakini bila shaka lingeyafanya kuwa madogo sana, hasa ikizingatiwa kuwa msimu haujafikisha hata miezi mitatu.
Hata hivyo, Real Madrid iliharibu rekodi nzuri ya Barcelona ya kutopoteza pointi katika La Liga na kupunguza pengo kati yao hadi tatu sawa na mechi moja.
Na sasa mbio za ubingwa wa La Liga zimefunguka zaidi, hasa kwa kuzingatia kwamba Atletico Madrid iko pointi mbili tu nyuma ya Barcelona, ambayo inashika nafasi ya pili.
Baada ya wiki mbili, Atletico na Barcelona zitakutana kwenye Uwanja wa Metropolitano, huku kikosi cha Diego Simeone kikiwa na lengo la kupigania nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi.
Barcelona ilikuwa imeanza msimu kwa kiwango cha kuvutia sana, lakini kipigo cha El Clásico cha Jumapili kimekuwa na gharama kubwa kwao. Kwa maana ya ushindani wa pointi, matokeo hayo yanaweza kuchukuliwa kuwa mabadiliko ya pointi sita.
Mabingwa hao watetezi wa Hispania wanapaswa kufanya kazi haraka kurekebisha mambo, kwa sababu hawajaonyesha tena ubora waliokuwa nao mwanzoni mwa msimu tangu waanze kukutana na wapinzani wa kiwango cha juu.
Kwa upande mwingine, Los Blancos sasa imeshinda mechi tano mfululizo tangu mapumziko ya mechi za kimataifa kati ya Septemba na Oktoba. Inaonekana kuimarika kadiri kila mchezo unavyopita.
Kikosi cha Mourinho kinapaswa kuchukuliwa kuwa mpinzani wa kweli katika mbio za ubingwa wa La Liga na pia katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.