KAIBEBA! Kwa nini Harry Kane amevuta Ballon d’Or
Muktasari:
- Kufunga mabao 73 katika msimu mmoja siyo jambo dogo hata kwa timu nzima. Lakini, mchezaji mmoja kufunga mabao mengi kiasi hicho ni mafanikio ya kushangaza.
LONDON, ENGLAND: HARRY Kane huenda asiwe mshindi mwenye mvuto mkubwa zaidi wa tuzo ya Ballon d’Or 2026, lakini ushindi wake umethibitisha kuwa kudumisha kiwango cha juu cha uchezaji ni jambo linaloweza kumfikisha mchezaji kileleni mwa soka la maisha yake.
Kufunga mabao 73 katika msimu mmoja siyo jambo dogo hata kwa timu nzima. Lakini, mchezaji mmoja kufunga mabao mengi kiasi hicho ni mafanikio ya kushangaza.
Hilo ndilo alilolifanya Kane msimu uliopita, alipofunga mabao 61 akiwa na Bayern Munich na mengine 12 timu ya taifa ya England. Cha kushangaza zaidi, mabao hayo 73 aliyafunga katika mechi 65 pekee.
Kane alitarajiwa kwa kiasi kikubwa kutwaa tuzo ya Ballon d’Or 2026 na juzi, Jumatatu, alifanya hivyo, na kuwa mchezaji wa kwanza kutoka England kushinda tuzo hiyo tangu Michael Owen 2001.
Tuzo hiyo aliipokea jijini London ambako amefunga mabao yake mengi. Hata hivyo, nafasi yake ya kufikia mafanikio hayo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na uamuzi wake wa kuhamia Munich.
KUONDOKA SPURS
Baada ya miaka 19 akiwa Tottenham Hotspur, safari iliyoanza akiwa na umri wa miaka 11 katika akademi ya klabu hiyo na kuishia akiwa nahodha na mfungaji bora wa muda wote wa timu, Kane alifanya uamuzi ambao wengi hawakutarajia wa kuhamia Ujerumani Agosti 2023, alikojiunga na Bayern Munich.
Kilichoufanya uamuzi huo kuwa wa kushangaza ni kwamba alikuwa amebakiza mabao 47 pekee kufikia rekodi ya mabao mengi zaidi katika historia ya Ligi Kuu England iliyowekwa na Alan Shearer, huku akiwa bado na miaka mingi ya kucheza soka.
Uamuzi wa Kane kuondoka Spurs ulichochewa zaidi na hamu ya kubadilisha rekodi binafsi na kuelekea mafanikio ya timu, baada ya miaka mingi bila kutwaa taji kubwa akiwa na klabu.
Nyota huyo ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 30, alitaka kushinda mataji, na Bayern ilionekana kuwa mahali sahihi pa kutimiza lengo hilo. Hata hivyo, kinachovutia ni kwamba kwa kufanya uamuzi huo, sasa yuko katwaa tuzo ambayo huenda ndiyo heshima kubwa zaidi ya mtu binafsi ambayo mchezaji wa soka anaweza kupata.
Safari ya Kane kuelekea kuwa mshindi wa Ballon d’Or imejengwa zaidi katika kutegemewa na kudumisha kiwango cha juu kuliko kung’ara kwa vipindi vifupi na kushuka kwa kiwango.
Pamoja na hilo, uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao akiwa Bayern umempandisha katika kiwango kingine tangu alipoondoka katika klabu aliyokulia, na kumuweka miongoni mwa wafungaji bora wa mabao katika historia ya soka.
NAMBA ZA MOTO
Kane alifunga mabao 61 katika mashindano yote msimu uliopita, ambao ndio kipindi kilichotumika kutathmini waliowania Ballon d’Or mwaka huu. Alifunga mabao 19 zaidi ya mchezaji mwingine yeyote katika ligi tano bora za Ulaya.
Hiyo ilikuwa idadi kubwa zaidi ya mabao yaliyofungwa na mchezaji mmoja katika msimu mmoja akiwa na klabu inayoshiriki ligi hizo tano bora tangu Cristiano Ronaldo alipofunga mabao 61 akiwa na Real Madrid 2014/15.
Hata ukiondoa mabao 17 ya penalti, Kane angebaki na 44 ambayo bado ni mengi kuliko mfungaji aliyemfuatia, Kylian Mbappe aliyefunga mabao 42 yakiwamo 12 ya penalti.
Kane alifunga mabao 36 katika Bundesliga, idadi aliyofikia pia katika msimu wake wa kwanza Bayern 2023/24. Pia, alitwaa kiatu cha dhahabu cha Bundesliga kwa mara ya tatu mfululizo.
Mchezaji mwingine pekee katika historia ya Bundesliga kutwaa tuzo hiyo kwa misimu mitatu au zaidi mfululizo ni Robert Lewandowski aliyefanya hivyo misimu mitano kuanzia 2017/18 hadi 2021/22.
Mabao 36 ya Kane Bundesliga 2025/26 yamezidiwa mara tatu tu katika historia ya mashindano hayo tangu yalipoanza 1963. Lewandowski alifunga 41 msimu wa 2020/21, huku Gerd Muller akifunga 40 msimu wa 1971/72 na 38 ule wa 1969/70.
Kane pia alifunga hat-trick tano akiwa na Bayern msimu uliopita, zaidi ya mara mbili ya mchezaji mwingine yeyote katika klabu zinazoshiriki ligi tano bora za Ulaya. Hat-trick nne kati ya hizo alifunga Bundesliga, idadi aliyofikia pia 2023/24, ambao ulikuwa wa kwanza kwake Ujerumani.
Katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kane alifunga mabao 14, ikiwa ndiyo idadi kubwa zaidi aliyowahi kufunga katika kampeni moja ya mashindano hayo, akimaliza akiwa bao moja nyuma ya Mbappe aliyefunga mabao 15 na kuwa mfungaji bora wa mashindano hayo.
Pamoja na hilo, Kane alijiunga na kundi dogo la wachezaji sita pekee katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kufunga mabao 14 au zaidi ndani ya msimu mmoja.
Katika kipindi kilichotumika kutathmini Ballon d’Or 2026, kuanzia Agosti 3, 2025 hadi Julai 19, 2026, ni Erling Haaland aliyefunga mabao 20, Mbappe 16 na Mikel Oyarzabal 14 pekee waliokuwa na mabao mengi zaidi ya Kane, aliyefunga 12 kwa timu za taifa zinazoshiriki mashindano ya Ulaya (UEFA).
Mabao sita aliyofunga katika Kombe la Dunia 2026 akiwa na England yalimwezesha Kane kumpita Gary Lineker na kuwa mfungaji bora wa England katika historia ya mashindano hayo.
Na sasa ana mabao 14 katika Kombe la Dunia, manne zaidi ya Lineker. Pia amekuwa mchezaji wa kwanza wa kiume wa England kufunga katika mashindano makubwa matano tofauti ya kimataifa.
KIWANGO CHA KUSHANGAZA
Katika ngazi ya klabu, mabao 61 ya Kane akiwa na Bayern Munich ndiyo idadi kubwa zaidi aliyowahi kufunga katika msimu mmoja kwenye mashindano yote. Alivunja rekodi yake ya awali ya mabao 44, aliyofunga katika msimu wake wa kwanza klabuni hapo 2023/24.
Tangu alipoingia katika kikosi cha kwanza cha Tottenham na kuwa mchezaji wa kudumu 2014/15, Kane alifunga mabao 20 au zaidi katika soka la klabu kwa misimu yote 12 iliyotangulia msimu wa 2026/27. Katika misimu minane kati ya hiyo, alifikisha mabao 30 au zaidi.
Kuanzia 2014/15 hadi mwisho wa 2025/26, mchezaji pekee aliyefunga mabao mengi zaidi katika mashindano yote ya ligi tano bora za Ulaya kuliko Kane, aliyefunga 421 alikuwa Lewandowski mabao 464.
Kane alifunga katika mechi 47 tofauti msimu uliopita akiwa na Bayern na timu ya taifa ya England. Hakuwahi kucheza zaidi ya mechi mbili mfululizo bila kufunga bao. Mara ya mwisho alipokaa zaidi ya mechi mbili bila kufunga katika msimu mmoja kwa klabu na timu ya taifa ilikuwa Februari 2025.
Kinachovutia siyo idadi ya mabao anayofunga au mechi anazofunga, bali pia uwezo wake wa kutumia nafasi anazopata. Msimu uliopita, asilimia 24.1 ya mashuti yake yasiyotokana na penalti akiwa na klabu na timu ya taifa yaligeuka kuwa mabao.
Kiwango hicho kilikuwa cha juu zaidi ya cha wachezaji kama Mbappe aliyekuwa na asilimia 15.8, Oyarzabal 16.3 na Ferran Torres 18.8. Kane alikuwa nyuma kidogo tu ya Haaland, aliyekuwa na asilimia 25.2.
Miongoni mwa wachezaji kutoka Ulaya na Amerika Kusini waliochezea klabu katika ligi tano bora za Ulaya 2025/26, hakuna aliyezidi makadirio ya mabao yasiyotokana na penalti kwa kiwango kikubwa kuliko Kane, aliyekuwa juu kwa mabao 20.3 akiwa na klabu na timu ya taifa. Huo ulikuwa msimu wa kipekee kwa Kane, lakini uwezo wake wa kufunga mabao mengi kuliko yanavyotarajiwa kulingana na nafasi anazopata siyo jambo lililoanza msimu huo pekee.
Kutumia takwimu za mabao yaliyotarajiwa kupima uwezo wa mchezaji kumalizia nafasi kwa usahihi kwa kuangalia kipindi kifupi kunaweza kupotosha. Hata wachezaji bora hupitia vipindi ambavyo wanashindwa kutumia nafasi, huku wengine wakipata vipindi vifupi vya kufunga mabao mengi.
Hata hivyo, mchezaji anayeendelea kufunga mabao mengi kuliko kiwango chake tarajiwa kwa muda mrefu huonyesha uwezo wa kumalizia nafasi kwa kiwango kilicho juu ya wastani.
Katika kipindi cha misimu mitano kuanzia mwanzo wa 2021/22 hadi mwisho wa 2025/26, wachezaji 12 tofauti walipiga mashuti yasiyotokana na penalti 400 au zaidi katika ligi tano bora za Ulaya.
Mbappe alikuwa na mashuti mengi zaidi (688) akifuatiwa na Kane (607). Pamoja na kupiga mashuti mengi kiasi hicho, Kane aliendelea kuonyesha uthabiti mkubwa katika kutumia nafasi zake.
Katika kipindi hicho cha misimu mitano, Kane alifunga mabao 112 kutokana na mabao tarajiwa ya 90.2, hivyo kufunga mabao 22.8 zaidi ya makadirio. Hicho kilikuwa kiwango kikubwa zaidi cha kuzidi mabao tarajiwa kuliko mchezaji mwingine yeyote katika ligi tano bora za Ulaya.
Kuzidi makadirio kwa muda mrefu kiasi hicho kunaonyesha jinsi alivyo mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kumalizia nafasi.
Uchambuzi wa wastani unaohusisha mashuti 50 katika vipindi vinavyofuatana katika misimu mitano unaonyesha wazi zaidi uwezo wake wa kufunga mabao.
Wachezaji wengine wengi kati ya 11 waliochambuliwa walipitia vipindi vya kufunga mabao mengi au machache kuliko ilivyotarajiwa kwa kuzingatia matarajio yao. Kane, kwa upande mwingine, mara chache sana alishuka chini ya kiwango kilichotarajiwa.
Bila shaka, Kane ananufaika na wachezaji wenzake kama Michael Olise na Luis Díaz wanaomtengenezea nafasi za kufunga akiwa Bayern. Hata hivyo, pia amekuwa sababu muhimu iliyowafanya wachezaji hao wawili kufanya vizuri.
Msimu uliopita, Olise alikuwa wa kwanza kwa asisti katika mashindano yote miongoni mwa wachezaji wa klabu za ligi tano bora za Ulaya akiwa nazo 26, huku Díaz akiwa wa tatu na 19.
ZAIDI YA STRAIKA LA MABAO
Jambo ambalo mara nyingi huzungumziwa kuhusu Kane ni tabia yake ya kushuka nyuma kutoka eneo la ushambuliaji na kushiriki katika kujenga mashambulizi, tofauti na washambuliaji wengi.
Hilo siyo jipya kwake, lakini linavutia zaidi linapozingatiwa pamoja na idadi kubwa ya mabao anayofunga. Msimu uliopita aligusa mpira ndani ya eneo la hatari la wapinzani kwa asilimia 14.8 pekee ya miguso yake yote katika mashindano yote.
Kiwango hicho kilikuwa chini ya kile cha washambuliaji wengine wanaofunga mabao mengi, wakiwamo Mbappe mwenye asilimia 17.6, Haaland 26.8, Deniz Undav 15.3, Lautaro Martínez 15.4 na Vinicius Junior 17.0.
Tofauti kati ya Kane na Haaland ilikuwa kubwa zaidi. Haaland ni mshambuliaji anayependa kukaa ndani ya eneo la hatari la wapinzani, wakati Kane hutumia muda mwingi zaidi nje ya eneo hilo, akisaidia kujenga mashambulizi kabla ya kuingia ndani ya eneo la hatari.
Msimu wa 2025/26, Kane alikuwa na wastani wa kugusa mpira nje ya eneo la hatari la wapinzani mara 37.1 kwa mechi katika mashindano yote, zaidi ya mara mbili ya Haaland aliyekuwa na wastani wa miguso 16.4.
Hii ndiyo sababu Kane ni tishio kubwa kwa safu za ulinzi za wapinzani. Akiwa na umri wa miaka 33, mara nyingi hushuka nyuma na kutumia nafasi ambazo mabeki wa kati hawapendi kuingia kuzifunika. Timu ya taifa ya England na Bayern zimejenga mifumo ya uchezaji kwa kuzingatia uwezo huo wa Kane, huku wachezaji wenye kasi na nguvu wakitumia haraka nafasi zinazofunguka kutokana na mwendo wake.
Takwimu za Kane katika kutengeneza nafasi msimu uliopita hazikuwa kubwa sana, akiwa na asisti sita na nafasi 67 alizotengeneza kupitia mashambulizi ya wazi. Hata hivyo, takwimu hizo zilimuweka katika kundi la juu ikilinganishwa na wachezaji wengine wa nafasi yake, akiwa na asilimia ya 82.
MAFANIKIO YANAYOSTAHILI
Kwa sehemu kubwa ya msimu uliopita, ilionekana kuwa Lamine Yamal ndiye angekuwa mpinzani mkubwa zaidi wa Kane katika kuwania Ballon d’Or 2026. Takwimu za Yamal 2025/26 zilimpa hoja nzito kutwaa tuzo hiyo.
Akiwa na Barcelona, alifunga mabao 24 na asisti 17 katika mashindano ya klabu. Jumla ya mabao na asisti alizohusika nazo ilikuwa 41, ikiwa nyuma ya Kane aliyekuwa na 68, Olise na Mbappe waliokuwa na 48 kila mmoja, Haaland mwenye 47 na Diaz aliyekuwa na 45 miongoni mwa wachezaji wa ligi tano bora za Ulaya.
Jambo la kushangaza zaidi kuhusu Yamal ni kwamba alimaliza msimu wa 2025/26 akiwa na umri wa miaka 19 na siku sita tu, huku akiwa tayari ameshinda Kombe la Dunia. Kwa mujibu wa makala hii, ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutwaa taji hilo.
Katika miaka ya Kombe la Dunia tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990, ni mara mbili tu ambapo mchezaji hakushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya au Kombe la Dunia, lakini alitwaa Ballon d’Or. Hiyo ilikuwa kwa Hristo Stoichkov 1994 na Lionel Messi 2010.
Hata hivyo, muda wa Yamal wa kutwaa tuzo hiyo bado utakuja. Kwa sasa, Kane anaweza kufurahia mafanikio ya kutimiza kile alichokusudia alipokubali kutoka katika mazingira aliyoyazoea na kujipa changamoto mpya ili kutwaa mataji yaliyohitajika kuimarisha nafasi yake miongoni mwa wanasoka wakubwa wa wakati wote.