Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kibu afichua tamu, chungu za Libya

Muktasari:

  • Kibu, ambaye ni sehemu ya kikosi cha Taifa Stars, amekuwa mmoja wa wachezaji wanaotumia uzoefu wa kucheza nje ya Tanzania kuongeza thamani yao katika timu ya taifa huku akifichua kuwa tangu alipokwenda Libya amejifunza mengi ndani na nje ya uwanja.

MSHAMBULIAJI wa Al-Nasr ya Libya, Kibu Denis, amefichua namna maisha ya soka la kulipwa nje ya Tanzania yanavyomjenga zaidi, akisema ushindani mkubwa anaokutana nao nchini humo umemfanya ajisukume kufikia kiwango cha juu zaidi.

Kibu, ambaye ni sehemu ya kikosi cha Taifa Stars, amekuwa mmoja wa wachezaji wanaotumia uzoefu wa kucheza nje ya Tanzania kuongeza thamani yao katika timu ya taifa huku akifichua kuwa tangu alipokwenda Libya amejifunza mengi ndani na nje ya uwanja.

Mshambuliaji huyo, ambaye hadi sasa amefunga mabao saba katika mashindano yote akiwa na Al-Nasr na kutoa asisti tano, anasema kiwango cha ushindani alichokikuta Libya ni kikubwa kuliko alichokizoea Tanzania.

Anasema mazingira hayo yamemlazimisha kutoridhika na kiwango alichofikia, bali kila mchezo kujitafuta upya na kuongeza kitu katika uchezaji wake.


USHINDANI UMEONGEZA KIWANGO

Kibu anasema moja ya vitu vikubwa alivyovuna tangu alipohamia Libya ni ushindani unaomlazimisha kufanya zaidi ya alichokuwa akikifanya Tanzania.

“Ushindani ni mkubwa sana kule. Kile nilichokuwa nakifanya hapa Tanzania, kule ni zaidi ya mara mbili au mara tatu. Kwa hiyo ukubwa wa ushindani na uzoefu ninaoupata kule, namshukuru Mungu, ninaendelea kuutumia kuja kusaidia timu yangu ya taifa," anasema na kuongeza;

“Unapokuwa kwenye mazingira kama yale, huwezi kusema nimefanya vizuri leo basi nimefika. Kila siku unatakiwa kuonyesha kitu kipya, unatakiwa kupambana ili ubaki kwenye kiwango kilekile au ukipandishe zaidi. Hilo limenisaidia sana mimi kama mchezaji.”

FURAHA YA KWELI

Kibu anasema taarifa ya kuitwa Taifa Stars miaka mitano iliyopita imekuwa moja ya matukio muhimu katika safari yake ya soka, hasa kwa sababu hakutarajia kama angepata nafasi hiyo wakati huo.

Anakumbuka kuwa akiwa Mbeya City, taarifa hiyo ilifika kwake kwa njia ambayo haikutarajiwa, baada ya mdogo wake kumtumia picha kupitia WhatsApp.

“Kwa mara ya kwanza kusema ukweli nilipokea kwa furaha kubwa sana kwa sababu sikuwahi kutegemea. Ijapokuwa nilikuwa nacheza mpira, sikuwahi kusema kwa kiwango ninachocheza naweza nikaja kupata nafasi ya kuitwa timu ya taifa," anasema kiungo huyo na kuongeza;

“Mdogo wangu ndiye aliyenitumia picha WhatsApp akaniambia, ‘Kaka umeitwa timu ya taifa.’ Sikuamini. Tulikuwa mazoezini, wachezaji wenzangu wakawa wananiambia, ‘Bana umeitwa huko.’ Baadaye tulipofika kambini kwenye klabu yangu nikapata taarifa rasmi kwamba kweli nimeitwa."

Anaendelea kwa kusema; “Nilifurahi sana kwa sababu kuitwa timu ya taifa ni jambo la faraja sana kwenye maisha ya soka kwa kila mchezaji, hususani kijana ambaye bado anapambania ndoto zake. Kwangu ilikuwa kama uthibitisho kwamba kile ninachokifanya kinaonekana na kimenipa nguvu ya kupambana zaidi.”


KUFUNGA HAITOSHI

Kwa Kibu, furaha kubwa akiwa Taifa Stars haipo tu kwenye kufunga bao, bali kwenye kuona mchango wake unaisaidia timu kupata matokeo.

Anasema anaweza kufunga lakini kama timu ikapoteza, hisia zake haziwezi kuwa sawa na pale anapofunga au kutoa asisti na Taifa Stars ikaondoka na ushindi.

“Furaha inakuwa kubwa sana ninapofunga au ninapoasisti, lakini zaidi sana tunaposhinda. Unaweza ukafunga lakini timu ikawa inapoteza, kwa hiyo ile furaha inakuwa haipo kabisa kwa hiyo ninapopata nafasi ya ku-asisti na kufunga kwenye timu yangu ya taifa na kupata ushindi, inakuwa na faraja kubwa kwangu. Sio kwangu tu, hata kwa mashabiki, Watanzania wote na familia yangu. Unajua unapokuwa umeisaidia nchi yako kupata matokeo, ile hisia yake ni tofauti kabisa,” anasema.

MAISHA YA LIBYA

Licha ya kuondoka Tanzania na kwenda kucheza Libya, Kibu anasema hakukutana na ugumu mkubwa wa kuzoea maisha ya soka la nje ya nchi kama ambavyo watu wengi wanaweza kufikiria.

Anasema jambo lililorahisisha safari hiyo ni mapokezi aliyoyapata Al-Nasr, ambako wachezaji wenzake walimfanya ajisikie kama mtu ambaye alikuwa amekaa nao kwa muda mrefu.

“Nikienda kucheza nje ya nchi sioni kama kuna ugumu mkubwa uliopo. Naweza kusema ni mazingira tu tofauti, lakini sioni kama kuna ugumu wote,"

“Namshukuru Mungu kwa sababu malezi na mapokezi kule yalikuwa mazuri. Ukienda sehemu mpya halafu watu wakakupokea vizuri, inakusaidia sana. Wachezaji wenzangu walinipokea kwa furaha, walikuwa wachangamfu na walinifanya nijisikie kama tumeshaishi muda mrefu pamoja,” anasema.


WIKI TATU ZILITOSHA

Kibu anasema hakuhitaji muda mrefu kuingia kwenye mfumo wa Al-Nasr, akitaja mapokezi mazuri na mazingira ya timu kama sababu zilizomsaidia kuzoea haraka.

“Nilivyofika kuchukua muda kama wiki tatu hivi. Nilivyofika ilikuwa baada ya wiki mbili mechi zikaanza, kwa hiyo nilivyoanza kucheza mechi ya kwanza moja kwa moja nikaingia kwenye mfumo," anasema na kuongeza;

“Niliona wenzangu wananielewa na mimi nawaelewa. Kocha pia alikuwa anataka nijue mfumo wao na mimi nilikuwa tayari kujifunza. Kwa hiyo haikuwa changamoto kubwa sana kwangu kuingia kwenye mfumo.”


BARIDI ILIKUWA MTIHANI

Kama kuna jambo moja lililompa wakati mgumu mwanzoni, Kibu anasema ni hali ya hewa, hasa baridi kali ya Libya wakati wa Januari.

Akiwa ametoka Tanzania ambako amezoea hali ya joto, anasema mabadiliko hayo yalikuwa tofauti kwake, lakini baada ya muda aliweza kuzoea.

“Kwanza nilifika Januari, Libya kunakuwa na baridi kali sana. Baridi ilinipa ugumu kwa sababu ukiangalia huku Tanzania nimetoka kwenye joto muda wote.

“Kwa hiyo mwanzoni ilikuwa tofauti kwangu, lakini namshukuru Mungu haikuchukua muda mrefu sana ku-adapt. Mwili nao unaanza kuzoea na unaendelea na maisha yako ya kawaida,” anasema.

KUWA MBALI NA FAMILIA

Licha ya kusema Libya ameiweka kwenye nafasi ya nyumbani, Kibu anakiri kuwa kuna kitu kimoja ambacho hawezi kukificha kuwakosa watu wake wa karibu.

Anasema umbali na familia yake ndiyo sehemu inayomfanya wakati mwingine ajisikie mpweke akiwa nchini humo.

“Familia yangu tu ndiyo ninayowamisi kwa sababu kule nakuwa mpweke sana. Hakuna rafiki mwingine ninayemmisi zaidi ya mke wangu, watoto, mama na wadogo zangu. Unapokuwa mbali na familia kuna wakati unahitaji tu kuwa nao, kuongea nao na kuona wanaendeleaje. Lakini hilo ni sehemu ya maisha ya mchezaji anayekwenda kucheza nje. Lazima ukubali kwamba kuna vitu utavikosa, lakini unapaswa kuendelea kupambana kwa ajili ya kazi yako na maisha ya familia yako,” anasema.


LIBYA NI NYUMBANI PIA

Pamoja na kuwa mbali na Tanzania, Kibu anasema mazingira ya Al-Nasr yamemfanya asihisi kama yuko ugenini.

Anasema mapokezi aliyoyapata na namna anavyoishi ndani ya timu vimefanya Libya kuwa kama nyumbani kwake.

“Mimi nikiwa Libya nahisi tu kama nipo nyumbani. Kwa hiyo hakuna changamoto yoyote ambayo nimeipata kule mbaya ikanifanya nijisikie nirudi nyumbani. Hapana, kwa sababu kule pia ni kama nyumbani.

“Unapopokelewa vizuri, ukawa na watu wanaokuelewa na ukaweza kufanya kazi yako vizuri, hauwezi kujisikia kama uko sehemu ambayo si yako. Mimi nimezoea na naendelea na maisha yangu kule,” anasema.


ANAJISHINDANISHA MWENYEWE

Kibu anasema tofauti kubwa na alichokizoea Tanzania ni namna anavyotazamwa ndani ya Al-Nasr, ambako anahisi wachezaji wenzake wanamtegemea zaidi kutokana na uzoefu na uwezo wake.

Hali hiyo, badala ya kumweka kwenye presha, imemfanya ajitengenezee ushindani binafsi wa kutaka kufanya vizuri kila mchezo.

“Kwenye timu ile mimi nachukuliwa kama mchezaji mkubwa sana. Kwa hiyo ushindani wa kule ni kwamba najishindanisha mwenyewe. Nataka nifanye kikubwa zaidi kila mechi. Sitaki nikacheza vizuri leo halafu kesho nikaona imetosha. Nataka kila mechi niingie nikiwa na kitu cha kuongeza," anasema.

Anaongeza; “Wachezaji wenzangu wananipa thamani kubwa na wananitegemea kwamba kwenye uwezo wangu naweza kufanya kitu kikubwa cha kuisaidia timu. Hilo linanipa nguvu zaidi kwa sababu najua kuna watu wananiamini. Kwa hiyo unatakiwa urudishe ile imani kwa kufanya kitu kizuri uwanjani.”

UZOEFU WAKE STARS

Kibu anasema uzoefu anaoupata Libya hauishii Al-Nasr pekee, bali anaupeleka pia Taifa Stars, ambako anakutana na wachezaji wenye malengo yanayofanana ya kuipeleka Tanzania kwenye mafanikio.

Anasema ushindani wa nje umemsaidia kuwa na mtazamo mpana zaidi kuhusu soka na namna mchezaji anavyopaswa kujiandaa.

“Uzoefu ninaopata kule ninakuja kuutumia hapa Taifa Stars. Unapokuwa kwenye ushindani mkubwa unajifunza kuwa tayari muda wote, unajifunza kupambana na hali tofauti na unajifunza pia kuwaheshimu wapinzani," anasema na kuongeza;

“Kwa hiyo mimi kile ninachokipata Libya nataka nikitumie kusaidia Taifa Stars. Nchi yangu ndiyo inanipa nafasi ya kuonyesha uwezo wangu, kwa hiyo nikija hapa nataka nitoe kile nilichojifunza kule ili kiwe na faida kwa timu yangu ya taifa.”