Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kipa Azam: Kwa mashuti  moto kwanini usivurugwe?

Muktasari:

  • Akizungumzia ushindani wa namba dhidi ya makipa wenzake klabuni hapo kama Aishi Manula na Zuberi Foba, Hamisi amebainisha kuwa wanaishi katika mtindo wa kifamilia wenye upendo na kusaidiana kwa kila namna.

BAADA ya msimu mmoja wa kuitumikia KMC kwa mkopo, mlinda mlango Hamisi Athuman amerejea rasmi kwenye klabu ya Azam FC, akiwa na kiu ya kutumia fursa hiyo kujijenga zaidi na kutimiza ndoto zake za kimataifa. Kipa huyo amefunguka mambo mbalimbali kuhusu kurejea Chamazi, ushindani wa namba na Aishi Manula pamoja na Zuberi Foba, maisha yake ya soka, ugumu wa nafasi ya golikipa na malengo yake.


MANULA, FOBA

Akizungumzia ushindani wa namba dhidi ya makipa wenzake klabuni hapo kama Aishi Manula na Zuberi Foba, Hamisi amebainisha kuwa wanaishi katika mtindo wa kifamilia wenye upendo na kusaidiana kwa kila namna.

Anaeleza kuwa kocha Florente Ibenge ana mfumo wa mzunguko unaotoa fursa kwa kila golikipa kucheza.

“Mwalimu wetu anampa kila mtu nafasi kulingana na mchezo husika. Nilicheza mchezo wa kwanza, nikapumzika wa pili, nikacheza wa tatu na wa nne kabla ya Foba kurudi na kuendelea,” alisema Hamisi, akisisitiza kuwa mzunguko huo unawasaidia wachezaji wote kukua na kuwa na utayari pindi dharura inapojitokeza.

AZAM CHUO CHA SOKA

Hamisi ameitaja Azam FC kama sehemu sahihi inayojenga misingi sahihi ya mpira nchini, akibainisha kuwa asilimia kubwa ya wachezaji wanaocheza Ligi Kuu hivi sasa wamepita kwenye mfumo wa vijana wa Azam.

“Wewe angalia tu ligi kuu utagundua kila timu lazima utakuta wachezaji wawili watatu waliopita Azam hapa mchezaji anaandaliwa kwa ajili ya ushindani na anaweza kucheza sehemu yoyote ndio maana nilisema ni chuo.”

Kipa huyo anamtaja Aishi Manula kama mmoja wa makipa anaowafuatilia ligi kuu kutokana na uzoefu wake na mchango alioutoa kwenye timu ya taifa.

Kuhusu uwepo wa magolikipa wa kigeni kwenye ligi, kipa huyo alisema iwapo kipa mgeni ana uwezo mkubwa uliowazidi wazawa, inakuwa ni fursa nzuri kwao kujifunza vitu vipya, lakini akiwa amezidiwa uwezo na wazawa inakuwa haina maana yoyote.


FOBA TANZANIA ONE

Alipoulizwa kuwataja magolikipa wa Kitanzania wanaoweza kuwa na kiwango bora na chenye mwendelezo katika miaka mitano ijayo, Hamisi alimweka Foba pamoja na yeye mwenyewe. Alieleza kuwa Foba ana uwezo mkubwa na uzoefu uliomfanya acheze mechi nyingi kubwa pamoja na michuano ya AFCON, huku akiamini kuwa yeye pia anajiona akifika mbali kupitia fursa za kucheza anazozipata.

“Kumpata Tanzania One kama Manula ni ngumu kwa sababu yeye alifanya kitu kikubwa kwa nchi lakini naamini Foba ni miongoni mwa makipa ambao wanakuja vizuri na mashabiki wakiendelea kumpa sapoti anaweza kutusaidia timu ya taifa miaka mitano ijayo.”

KIPA NAFASI NGUMU

Katika uchambuzi wake wa kiufundi, Hamisi anasisitiza kuwa nafasi ya golikipa ndiyo ngumu zaidi katika soka. “Kiungo akikosea, nyuma yake wapo mabeki wa kusawazisha makosa; beki akikosea, nyuma yake yupo kipa. Lakini golikipa akikosea mara moja au mbili, hakuna wa kumsaidia na inakuwa goli,” alieleza Hamisi.

Anaongeza kuwa kipa anafanya kazi katika eneo la mita nane peke yake, akiwa amevaa jezi tofauti na analazimika kupiga mahesabu na kufanya maamuzi sahihi ndani ya sekunde chache wakati mpira ukiwa kwenye spidi kubwa.

“Kwangu nadhani kipa ni nafasi ngumu ndio maana unaona wakati mwingine kama makipa akili zao haziko sawa kwa sababu ya kazi ngumu iliyopo mbele yao yaani mpira unarushwa na washambuliaji haijalishi usoni au mwilini.”

Anaongeza kuwa kigezo cha golikipa bora kinabaki kuwa ‘clean sheets’ nyingi, ingawa ubora pia unapimwa kwa mawasiliano, uongozi uwanjani na uwezo wa kuokoa hatari.

NJE YA SOKA

Anasema yeye tangu udogoni hakuwa na kitu cha kufanya zaidi ya mpira ambao akijifunza kwa kuwatazama wachezaji wa mtaani kwa kuwa hakuwa na fursa ya kuangalia TV au kwenda viwanjani wakati huo.

“Wakati huo nyumbani hakuna TV wala nafasi ya kwenda uwanjani kwa hiyo mimi nilikuwa nawatazama tu wale makipa waliokuwa wanacheza Ndondo basi.”