Prime
Kuwatetea Azam FC na Doumbia ni kazi ngumu, nimechoka
MIONGONI mwa kazi ngumu duniani ni kuitetea Azam FC. Namaanisha timu yao ya mpira. Sio viwanda, sio bidhaa zao. Timu yao ya mpira. Unahitaji kuwa na roho ngumu kuwatetea hawa rafiki zetu.
Wameanza ligi kama wale wakubwa wa Kariakoo, Simba na Yanga. Wakati wenzao wakiwa wameshinda mechi zote Azam tayari ana sare mbili. Sio sare tu, bali ni sare dhidi ya timu zilizopanda daraja msimu huu.
Polisi Tanzania na Geita Gold. Unawezaje kuchukua ubingwa kwa namna hii? Kama tunatamani kumpata bingwa mwingine wa Ligi Kuu Bara nje ya Simba na Yanga mawazo yetu huwa yanakwenda kwa Azam.
Hata hivyo, msimu umeanza tu tayari wameshajiweka nyuma kwa wakubwa. Wameanza kwa kurudia tabia yao ya misimu yote. Azam huwa hawasumbuliwi sana na mechi za Simba na Yanga. Huwa wanapata matokeo wanayoyahitaji.
Mara chache sana wanakosa matokeo wanayoyahitaji pindi wakicheza na wakubwa. Lakini limekuwa jambo la kawaida kwao kutopata matokeo mazuri dhidi ya timu ndogo.
Bahati mbaya kwa Azam ni kwamba timu ndogo zipo nyingi kuliko timu kubwa. Timu kubwa zipo mbili tu. Simba na Yanga. Hawa kina Polisi Tanzania na Geita wapo wengi.
Na hawa ndio ambao mara nyingi wanainyima ubingwa Azam na kuwapa mataji Simba na Yanga. Wanafungwa sana na Simba na Yanga halafu wanawavimbia Azam. Na Azam mpaka leo hajawahi kupata dawa yao. Ni ngumu kuwatetea Azam.
Zamani kulikuwa na utetezi kwamba Azam inanyongwa na waamuzi. TFF wameamua kutuletea kitu kinaitwa Football Video Support (FVS).
Uamuzi umekwenda kwa haki kwa kiasi kikubwa. Tayari Simba wamecheza mechi tatu wakiwa pungufu na bado wameshinda mechi zao. Azam tayari wamepoteza pointi nne dhidi ya timu zilizopanda daraja huku mechi zilichezwa kwa haki. Napata shida kuwatetea Azam.
Majuzi nilikuwa nawatetea Azam mitandaoni kwamba na wao wana haki ya kuwa na Fei Toto ambaye kila dirisha kubwa amekuwa akihusishwa na Simba na Yanga.
Kabla hatujafika mbali wale ambao wanasema Fei Toto aende timu za mataji Simba na Yanga wameanza kuninyima pumzi na kudai nilikuwa nafanya utetezi wa kijinga. Kwamba tayari Fei anaelekea kukosa taji la ubingwa ndani ya siku chache tu tangu msimu uanze.
Lakini, ni jambo gani Azam hawajafanya? Wana kocha wa viwango kabisa Florent Ibenge. Wamembakisha Fei Toto. Kila msimu wanaleta wachezaji wa maana. Wafanye nini zaidi? Unapowapambania mitandaoni wao wanakuangusha uwanjani.
Msimu huu wameleta watu wa maana kwa mujibu wa tafiti zao za usajili. Wamekuja watu wa maana kuungana na kina Fei, lakini tayari wana sare mbili zisizoeleweka. Ni kazi ngumu kuwatetea rafiki zetu wa Azam.
Tuwasubiri katika mechi za kimataifa? Labda, lakini kumbukumbu hazitupi sapoti tukiamua kuwaamini huko. Azam walishawahi kutolewa katika michuano mikubwa ya CAF na timu moja ya kipuuzi kutoka Ethiopia. Huwa tunasema kwamba Azam inanyongwa sana katika ligi ya ndani, vipi kuhusu mechi za nje za kimataifa.
Sasa hivi wana kocha wa viwango vya CAF labda tuwasubiri Azam huko. Tatizo rekodi zao katika michuano ya kimataifa huwa zinatutesa pia.
Inakuwa ngumu kuwatetea. Labda msimu huu wanaweza kufanya kitu, lakini kwa sare hizi za Polisi na Geita wameanza kuninyima pumzi mapema dhidi ya watesi wao ambao wanapambana na mimi nikiwa nawatetea.
Azam pesa ipo. Wachezaji wapo. Makocha wa maana wanakuja na kuondoka. Tatizo nini? Sielewi. Wakati mwingine huwa nahisi kwamba labda sio timu ya wananchi. Labda hakuna shinikizo kubwa la wao kushinda mechi zao.
Mfano ni kwamba hizi sare zao mbili zinaonekana kama jambo la kawaida tu. Fikiria kama hizi sare mbili wangetoa Simba na Yanga. Nchi isingekalika. Kuna watu wangetaka rafiki yangu Murtaza Mangungu ajiuzulu na kule kwa Yanga wangetaka kocha aondoke.
Kuitetea Azam ni sawa na kumtetea rafiki yangu Ibrahim Doumbia pale Msimbazi. Mshambuliaji fulani hivi ambaye niliingia vitani kumtetea, lakini naelekea kushindwa.
Alifunga bao zuri la kichwa katika mechi za michuano ya Kagame pale Rwanda. Nikaamini kwamba pamoja na upungufu wake mwingi lakini labda ni mzuri hewani.
Kuanzia hapo sijaona ubora wake chini wala juu. Mipira ya juu amekuwa akiokoa zaidi kuliko kufunga. Kumtetea Doumbia ni kazi ngumu hasa unapokumbuka kwamba yeye ni mshambuliaji tegemeo katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Kwamba, Ismail Mgunda amechukuliwa kuwa msaidizi wa Doumbia. Inanyong’onyesha mashabiki wa Msimbazi wakati huu ambao wanapambana kuiondoa Yanga katika kilele cha mafanikio.
Doumbia ananipa wakati mgumu kumtetea kwa sababu hata mashabiki wa Simba yake pia hawamtetei. Kama ni dakika za kucheza basi yeye ni miongoni mwa wachezaji wanaopewa dakika nyingi na kocha Steve Barker.
Mtu mmoja amenipenyezea kwamba aliyemleta Doumbia anashinikiza mchezaji wake apate dakika nyingi uwanjani kwa ajili ya kuhalalisha uhamisho huu.
Bahati nzuri kwa Doumbia ni kwamba mtu mwingine anayetumika katika nafasi yake haonyeshi kwanini Simba hawahitaji kuanza na Doumbia. Huyu anaitwa Ellie Mpanzu. Anatumika kama mshambuliaji feki pale mbele, lakini Mpanzu hana mwendelezo wa ubora. Mpanzu ana ubinafsi mwingi katika mchezo wake.
Ukweli ni kwamba nafasi ya mshambuliaji pale Simba inahitaji mtu wa maana. Hawahitaji mtu wa kubahatisha. Tulitoka na kina John Bocco, Meddie Kagere na Chris Mugalu leo tuna Doumbia.
Kuna mahala watu wanaofanya usajili Simba wanawakosea sana mashabiki wao. Nadhani katika uhamisho wa Doumbia ziliangaliwa namba zake tu, lakini hakukuwa na uchunguzi zaidi.
Umefika muda sasa tuanze kuangalia ubora wa ligi mbalimbali za Afrika Magharibi. Ligi kama ya Mali itupiwe jicho la pili. Wachezaji wengi waliotoka Ligi Kuu Mali kuja ligi yetu wanafeli. Aliyeweza zaidi ni Djigui Diarra.
Pande zote mbili wachezaji waliotoka Mali hawakuwa na maajabu. Doumbia anaongezeka katika orodha hii. Sidhani kama anaweza kunifanya nitambe mtaani.
Napata kazi kumtetea. Kuwatetea Azam ni kama kumtetea Doumbia. Kumtetea Doumbia ni kama kuwatetea Azam. Ni kazi ngumu huku mtaani.
Sijui lini wanaweza kutufanya tutoke kifua mbele. Kila unapodhani wanakaribia kukupa kiburi ndipo wanapokuangusha. Baadaye unaishia kuziba sura tu kwa aibu. Labda tuendelee kusubiri.