Manula afunguka kibao cha Erasto, AFCON na figisu za soka
Muktasari:
- Manula anasema tukio hilo lilitokea akiwa bado kijana, lakini halikuzaa ugomvi wala chuki, kwani baada ya kumpiga kibao, Erasto alitekeleza alichokuwa amemwelekeza na mchezo ukaendelea kama kawaida.
KIPA wa Azam FC, Aishi Manula ‘Tanzania One’ amefichua kwa mara ya kwanza alivyowahi kumpiga kibao Erasto Nyoni wakiwa uwanjani, akisema alifanya hivyo baada ya mchezaji huyo kuchelewa kutekeleza majukumu yake.
Manula anasema tukio hilo lilitokea akiwa bado kijana, lakini halikuzaa ugomvi wala chuki, kwani baada ya kumpiga kibao, Erasto alitekeleza alichokuwa amemwelekeza na mchezo ukaendelea kama kawaida.
Katika mahojiano maalum na Mwanaspoti, Manula pia anafunguka kuhusu deni kubwa walilopewa wachezaji wa Tanzania kuelekea AFCON 2027, akisema kucheza mashindano hayo nyumbani mbele ya Watanzania kunaongeza presha na wajibu wa Taifa Stars kufanya vizuri zaidi.
An asema kiwango kilichoonyeshwa na Taifa Stars katika AFCON iliyopita kimepandisha matarajio ya Watanzania, ambao sasa wanaamini timu hiyo inaweza kwenda mbali zaidi huku akitaja maandalizi yake binafsi kuwa ni kuhakikisha anakuwa fiti, anapata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye klabu yake na kumpa kocha wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, sababu ya kumjumuisha kwenye kikosi cha AFCON 2027.
KIBAO CHA ERASTO
Kama ilivyo kwenye soka, Manula anasema jazba ni sehemu ya mchezo, hasa wakati wa presha ambapo mapigo ya moyo huwa juu na mawasiliano ya wachezaji ni makali.
Anakumbuka tukio moja la akiwa bado kijana anacheza Simba, alipowahi kumpiga kibao Erasto Nyoni wakati wa mpira wa kona baada ya kuona mchezaji huyo alikuwa anachelewa kutekeleza maelekezo aliyokuwa akimpa.
“Nakumbuka nilipokuwa kijana mdogo, tuko kwenye kona na namuelekeza Erasto afanye kitu. Alikuwa kama anachelewa, nikampiga kibao,” anasema.
Kinachoshangaza anasema baada ya tukio Erasto aliendelea kuwa mchezoni na kutekeleza alichoagizwa huku suala hilo likiishia hapo.
“Baada ya kumpiga kibao akaenda akafanya kile kitu. Maisha mengine yakaendelea. Hakuna kitu kingine kilichotokea,” anasema.
Manula anasema matukio kama hayo yanaweza kutokea kutokana na presha ya mchezo, lakini hayapaswi kubeba chuki baada ya mchezo kumalizika.
DENI AFCON
Manula anasema jambo linalomzunguka kichwani ni ukubwa wa deni ambalo wachezaji wamepewa na Watanzania kutokana na Tanzania kuwa miongoni mwa wenyeji wa AFCON 2027.
Anasema kucheza mashindano makubwa nyumbani kunamaanisha wachezaji hawatakuwa na nafasi ya kujificha nyuma ya mazingira, kwani mashabiki watakuwa kwenye viwanja, wakifuatilia kila hatua na kutarajia matokeo mazuri.
“Ni deni kubwa ambalo tumepewa wachezaji wa Kitanzania. Mashindano yako nyumbani na matarajio tukiwa katika uwanja wa nyumbani ni makubwa zaidi kwa sababu tuko nyumbani, tuna mashabiki wetu na haya mashindano yako barazani,” anasema Manula.
Anaongeza kuwa wachezaji wanapaswa kulibeba jukumu hilo kwa heshima kwa kuhakikisha wanafanya kila linalowezekana kuipa Tanzania matokeo yatakayowafanya Watanzania wajivunie kuwa wenyeji wa mashindano hayo.
“Tunatakiwa tuwaheshimishe Watanzania kwa kile ambacho Serikali imeamua kutuletea AFCON. Sisi sasa tunatakiwa tulibebe hilo na tuwape sababu ya wao kuleta tena mashindano makubwa kama haya,” anasema.
IMEONGEZA PRESHA
Manula anasema kiwango cha Taifa Stars katika AFCON iliyopita ndicho kinachofanya matarajio ya mashabiki kuwa makubwa zaidi kuelekea ya 2027.
Anasema Watanzania sasa hawaangalii tena Taifa Stars kama timu inayoenda kushiriki tu, bali wanaamini inaweza kushindana na timu kubwa na kufika hatua za juu.
“Deni kubwa zaidi ambalo tunalo ni namna bora ambavyo timu ya Taifa imefanya kule Morocco. Kila Mtanzania sasa kichwani kwake anafikiria kile kiwango ambacho tuliifanya Morocco,” anasema.
Kwa mujibu wa Manula, kiwango kilichoonyeshwa dhidi ya baadhi ya vigogo barani Afrika ikiwemo Tunisia na wenyeji, Morocco kimewafanya Watanzania waanze kuamini kuwa robo fainali ya AFCON si ndoto tena. “Kama tuliweza kufanya vile Morocco, tukatoa kiwango kizuri dhidi ya Tunisia na tukatoa kiwango kizuri dhidi ya Morocco, vipi tukiwa kwenye uwanja wa nyumbani? Tafsiri yake kila mtu anaamini hapa robo fainali tunayo,” anasema.
Hapo ndipo anapoona ukubwa wa jukumu lililo mbele akisisitiza wachezaji wanapaswa kuwa makini katika kila hatua ya maandalizi ili wasije wakashindwa kufikia matarajio hayo.
“Namna gani bora ambayo tutafanya? Namna gani tunapaswa kufanya? Namna gani tusifanye makosa ili kile ambacho kila mtu kiko kichwani mwake tukakifikie? hilo ni deni kubwa ambalo mimi huwa naliwaza na nalifikiria siku zote.”
ANAITAKA AFCON
Pamoja na kuangalia mbali kuelekea AFCON, Manula anasema anajua safari ya kufika Stars inaanza na kufanya vizuri klabuni.
Anasema anahitaji kupata nafasi ya kucheza, kuwa na afya njema na kuendelea kujenga kiwango kitakachompa kocha wa Taifa Stars sababu ya kumchagua.
“Matarajio yangu kama mchezaji ni makubwa ni kuhakikisha kwamba napata nafasi ya kucheza kwenye klabu yangu lakini pia nakuwa na afya njema ili kuendelea kumpa mwalimu nafasi ya kuweza kunichagua na kuniweka kwenye kikosi ambacho kitaenda AFCON,” anasema.
NYAKATI NGUMU
“Mambo magumu zaidi ambayo nimekumbana nayo kwenye mpira ni pamoja na kukosa kile ambacho mmekitarajia au ambacho mlihisi kwamba mngestahili kukipata,” anasema.
Anataja kupoteza fainali au kushindwa kuvuka hatua fulani katika mashindano ya CAF kuwa miongoni mwa nyakati zinazoweza kumuathiri mchezaji hata baada ya mchezo kumalizika.
“Unakuta mna tarajia kwamba labda mnaenda mechi ya fainali au kufuzu hatua ya makundi ama kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa au Kombe la Shirikisho. Kila mmoja anajua leo tunaenda kumaliza hii kazi na tunavuka hiki kikwazo, lakini pale ambapo mnafeli, unakuta hata mtu unashindwa kulala,” anasema.
MAJERAHA, KUREJEA
Kwa upande wa majeraha, Manula anasema kuumia ni sehemu ya kazi ya mchezaji na si jambo la kumshangaza kwa mwanasoka.
Anasema jeraha linaweza kutokea kwenye mechi, mazoezini au hata nje ya uwanja, lakini changamoto kubwa huanza pale mchezaji anapolazimika kuanza safari ya kurejea baada ya kuumia.
“Kupata majeraha sio kitu kigumu kwa sababu unajua kazi tunayoifanya, muda wowote unaweza kuumia. Kitu kigumu ni pale ambapo unatoka kwenye majeraha na kuweza kurejea uwanjani,” anasema Manula ambaye wakati akiwa Simba aliwahi kukumbana na majeraha ya ngonga yaliyomweka nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi mitano.
“Kuna zile hatua za kupona ambazo unafanya na ‘physio’, hasa pale ambapo umetoka kufanya upasuaji. Kwenye zile nyakati za kurudi uwanjani ndipo inakuwa ngumu kwa sababu kuna maumivu. Unatakiwa uendelee nayo mpaka yaishe.”
Manula anasema kuvumilia hatua hiyo ni muhimu ya safari ya kurejea uwanjani, kwani mchezaji akishindwa kukabiliana na maumivu anaweza kurejea akiwa hajawa tayari.
Anasema pia uzito wa mwili baada ya kupona ni changamoto nyingine kwa mchezaji na kuongeza hatari ya kupata jeraha jipya.
“Lazima upambane na hayo maumivu na hicho kidonda ili uweze kurudi. Kuna wengine unakuta kweli umepona vizuri lakini umerudi ukiwa umenenepa na ukiwa umenenepa muda mwingine inaweza kusababisha ukapata majeraha,” anasema.
MATCH-FIXING? KELELE TU
Kuhusu tuhuma za upangaji matokeo ambazo zimekuwa zikizunguka katika soka la Tanzania, Manula anasema amewahi kukutana na mazingira yanayohusishwa na mijadala hiyo, lakini hataki kuingia kwenye tetesi ambazo hazina ushahidi.
Anasema kwake, jambo lisilo na ushahidi halistahili kupewa nafasi kubwa katika mjadala wa soka.
“Ni vitu ambavyo huwa siwezi kuvizungumzia kwa sababu kwangu sio vitu vya kuzungumzia. Mara zote zinakuwa ni kelele tu za watu ambazo hazina ushahidi,” anasema na kuongeza:
“Vitu ambavyo havina ushahidi sio vitu vya kuzungumzia.”
MAKIPA WA KIGENI
Katika miaka ya karibuni, ushindani kwenye nafasi ya makipa umeongezeka kutokana na klabu za Tanzania kusajili makipa wa kigeni, jambo ambalo Manula anasema ni sehemu ya mabadiliko ya soka la nchini.
Anasema ligi imekua, fedha zimeongezeka na matarajio ya klabu yamekuwa makubwa, hivyo kila timu ina uhuru kusajili mchezaji anayehisi anaweza kuisaidia kufikia malengo yake.
Anasema hali hiyo inawalazimisha makipa wazawa kupambana zaidi na kuonyesha thamani yao uwanjani badala ya kulalamikia uwepo wa wageni.
“Kitu ambacho kitakutofautisha na mwingine ni kile ambacho utakionyesha uwanjani. Soka ni mchezo wa wazi, watu wanaona. Sio wa kujificha,” anasema.
Manula anasema uzoefu wake unaonyesha kuwa pale alipokuwa akifanya vizuri na kuwa chaguo la kwanza, klabu hazikuwa na sababu ya kutafuta kipa mwingine wa kigeni kwa sababu alikuwa akifikia kiwango walichokuwa wanahitaji. “Miongoni mwa makipa ambao nimehudumu kwenye timu zote ambazo nimeweza kuhudumu nilikuwa chaguo la kwanza. Hakukuwa na hao magolikipa wa kigeni kwa namna ambavyo nilikuwa nacheza,” anasema.
TANZANIA IMEBADILIKA
Manula anasema ukuaji wa soka la Tanzania unaonekana pia katika namna ambavyo mashabiki wanavyotazama matokeo ya klabu na Taifa Stars kwenye mashindano ya kimataifa.
Anasema zamani timu za Tanzania zilipokwenda nje na kupoteza kwa tofauti ndogo, matokeo hayo yalionekana kama mafanikio na wachezaji walirudi wakiwa wamepongezwa. “Zamani tulikuwa tunashuhudia hizi timu zetu tukawa tunapongezwa kwa kufungwa magoli machache. Taifa Stars ikienda Misri ikafungwa tatu wanasema imejitahidi, ikienda Algeria ikafungwa tatu wanasema imejitahidi,” anasema.
Lakini kwa sasa, Manula anasema hali hiyo imebadilika kwa sababu kiwango cha Tanzania kimepanda na mashabiki wameanza kutaka zaidi. “Leo hii tukienda Congo tukacheza tukafungwa moja kutakuwa na malalamiko kwa nini tumefungwa. Kwa sababu wanaona levo tulivyofika na namna ambavyo wachezaji wetu tulivyo, tunastahili zaidi,” anasema.
DILI LA AFRIKA KUSINI
Manula pia anafichua kuwa wakati akiwa Simba aliwahi kuhusishwa na klabu kadhaa za Afrika Kusini ikiwemo Kaizer Chiefs, lakini anasema hakuwahi kuwa muumini wa kuondoka Tanzania kwa sababu tu klabu ya nje inamhitaji. Anasema kulikuwa na mawasiliano na hizo klabu, lakini ofa zilizokuwepo hazikufikia kiwango ambacho yeye aliona kinaweza kumshawishi kuondoka.
“Mara zote hata kwenye mahojiano ambayo nilikuwa nafanya nyuma, mimi sio muumini wa kutoka kwamba klabu inakutaka basi kwa sababu ni Afrika Kusini basi niende,” anasema.
Anasema moja ya mambo aliyokuwa akiyatazama ni kifurushi ambacho angekipata pamoja na gharama za maisha katika nchi hiyo.
“Kama Tanzania napata kiwango kizuri kuliko Afrika Kusini nikaona hakuna sababu ya kwenda kucheza nje. Tanzania ni rahisi maisha kwa sababu najua nitaenda kununua nyanya sehemu fulani au kula kwa mama ntilie, lakini nikishakuwa Afrika Kusini maisha yatakuwa ghari sana,” anasema.
Mbali na masuala ya kifedha, Manula anasema wakati huo aliona pia kiwango cha Simba katika mashindano ya kimataifa kilikuwa kikubwa kiasi cha kumfanya asiwe na sababu ya kukimbilia kuondoka.
FIGISU VYA AFRIKA
Manula anasema mwanzoni mwa safari yake kwenye mashindano ya kimataifa alikutana na mazingira ambayo kwake yalikuwa magumu na ya kushangaza.
Anataja kusubiri muda mrefu katika viwanja vya ndege, kuchelewa kwa visa, usumbufu wa usafiri na hata kuchelewa kufunguliwa kwa viwanja vya mazoezi kuwa miongoni mwa mambo aliyokuwa anayakutana nayo.
“Mwanzoni kipindi tunaanza kushiriki mashindano ya kimataifa ndipo nilikuwa naona vitu vya ajabu. Mnafika airport mnakaa saa tatu, watu wanachelewesha viza mnawekwa sehemu au mnaenda kwenye uwanja wa mazoezi kufunguliwa mnachelewa,” anasema.
Lakini anasema kadiri alivyozidi kupata uzoefu ndivyo alivyogundua kuwa sehemu kubwa ya changamoto hizo ni mazingira ya kawaida katika soka la Afrika. “Baadaye nikaona kumbe ni mazingira ambayo ni ya kawaida kabisa kwenye soka letu la Afrika.
Hata tukienda airport tukakaa masaa sita, sasa hivi unaagiza chakula, unakula, unakaa na unajua tutachelewa lakini tutatoka.”