Mastaa waliookota dodo Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Katika timu tatu zilizoshuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Championship kwa msimu wa 2025-2026, zilikuwa ni KMC FC ya Kinondoni, jijini, Dar es Salaam, maafande wa Tanzania Prisons ya jijini, Mbeya na Mtibwa Sugar kutokea mkoani Morogoro.
WAKATI dirisha la usajili la Ligi Kuu na mashindano mengine ya ndani limefungwa rasmi Agosti 15, 2026, baada ya kudumu kwa mwezi mmoja tangu lilipofunguliwa Julai 6, 2026, wapo wachezaji waliookota dodo licha ya timu walizochezea kushuka.
Katika timu tatu zilizoshuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Championship kwa msimu wa 2025-2026, zilikuwa ni KMC FC ya Kinondoni, jijini, Dar es Salaam, maafande wa Tanzania Prisons ya jijini, Mbeya na Mtibwa Sugar kutokea mkoani Morogoro.
Hata hivyo, wakati KMC FC, Tanzania Prisons na Mtibwa Sugar zinashuka daraja hadi Ligi ya Championship kwa msimu huu wa 2026-2027, zipo timu mbalimbali zilizonasa saini ya nyota hao na kubakia Ligi Kuu Bara, kama Mwanaspoti linavyozielezea.
JKT TZ (5)
Kikosi hicho cha maafande wa JKT Tanzania, katika usajili wake wa msimu wa 2026-2027, kimenasa saini ya wachezaji watano kutokea kwenye timu zilizoshuka daraja, huku Mtibwa Sugar ikiongoza ikiwa na wanne na Tanzania Prisons ikisajili mmoja. Kwa wachezaji wa Mtibwa Sugar waliosajili ni wale waliofanya vizuri kwenye kikosi hicho, wakiwemo kiungo mshambuliaji, Fredrick Magata aliyefunga mabao matano ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026, akifuatiwa na Ismail Mhesa na Said Mkopi.
Mhesa na Mkopi kila mmoja wao alifunga mabao manne ya Ligi Kuu wakiwa na kikosi hicho cha Mtibwa Sugar, wakiungana na kipa Constantine Malimi, huku kwa upande wa Tanzania Prisons aliyesajiliwa ni kiungo mkabaji, Abdallah Masoud ‘Cabaye’.
GEITA GOLD (5)
Geita Gold iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, imerejea tena Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kuibuka mabingwa wa Ligi ya Championship msimu wa 2025-2026, huku ikisajili wachezaji watano kama ilivyokuwa kwa Prisons kutokea timu mbalimbali.
Timu hiyo imepanda daraja baada ya kuongoza na pointi 77, ikiungana na Kagera Sugar iliyomaliza nafasi ya pili na pointi zake 72, zikipanda moja kwa moja na maafande wa Polisi Tanzania iliyorejea kupitia mechi za mchujo kwa maana ‘Play-Off’.
Wachezaji waliosajiliwa ni Twalib Mhenga ‘Chicharo’ na Datius Peter wote kutoka Mtibwa Sugar, Neva Kaboma na Haji Mussa Gabi wakitokea kikosi cha maafande Tanzania Prisons, huku mwingine ni beki wa kati, Salum Athuman ‘Stopper’ kutokea KMC.
MASHUJAA FC (4)
Kikosi hicho cha maafande kimesajili wachezaji wanne waliotoka katika timu zilizoshuka daraja, huku miongoni mwa sajili za kuangaliwa zaidi ni ya aliyekuwa mshambuliaji nyota wa maafande wa Tanzania Prisons ya jijini, Mbeya, George Mpole.
Mshambuliaji huyo aliifungia Tanzania Prisons mabao saba ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026, huku akikumbukwa zaidi kwa msimu wa 2021-2022, alipoibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu baada ya kufunga mabao yake 17, akiwa na kikosi cha Geita Gold.
Nyota wengine waliosajiliwa na kikosi hicho cha maafande mbali na Mpole ni kiungo, Tariq Simba na winga, Haruna Chanongo na aliyekuwa nahodha wa Mtibwa Sugar, Haroun Lyawatwa aliyecheza kikosini kwa mafanikio makubwa kuanzia timu za vijana.
MBEYA CITY (4)
Mbeya City iliyonusurika kushuka daraja msimu wa 2025-2026, imefanya maboresho mbalimbali ikiwemo kumwongeza aliyekuwa mshambuliaji wa maafande wa Tanzania Prisons, Oscar Mwajanga ambaye tayari ameanza kuonyesha kiwango bora kikosini humo.
Mwajanga aliifungia Prisons mabao manne ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, japo tangu ajiunge na Mbeya City ikiwa ni raundi ya tano imechezwa tayari ameifungia mabao matatu, akionyesha kiwango bora chini ya Kocha Mkuu, Salum Mayanga.
Mbali na Mwajanga anayeendelea kuonyesha kiwango bora hadi sasa, ila nyota wengine waliosajiliwa ni kipa, Toba Kutisha mwenye clean sheets tatu za Ligi Kuu kwa msimu huu, akiungana na Omary Buzungu na George Chota wote kutoka Mtibwa Sugar.
NAMUNGO FC (4)
Kikosi hicho cha Namungo FC maarufu kwa jina la utani la ‘Wauaji wa Kusini’, katika usajili wa msimu huu wa 2026-2027, kimenasa saini ya nyota wanne wote kutoka KMC, wakiwemo, Hance Masoud, Juma Shemvuni, Redemtus Mussa na Rashid Chambo. Wachezaji wote wanne wamekuwa muhimili mkubwa katika kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, kinachonolewa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda, huku Chambo akiwa ndiye mchezaji aliyefanya vizuri na KMC FC, baada ya kuifungia mabao matatu ya Ligi Kuu.
POLISI TZ (3)
Polisi Tanzania iliyopanda daraja kupitia ‘Play-Off’, kwa kuitoa Tanzania Prisons kwa jumla ya mabao 4-1 na kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, imenasa saini ya wachezaji watatu kutoka katika timu zilizoshuka daraja.
Wachezaji hao wawili wametokea Mtibwa Sugar ambao ni beki wa kushoto, Evance Fabian na beki wa kati, Oscar Masai, huku pia ikimsajili kiungo, Kenny Ally Mwambungu kutoka KMC na wote wamekuwa chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Mbwana Makata.
DODOMA JIJI (3)
Katika wachezaji watatu waliosajiliwa na Dodoma Jiji, miongoni mwao ni aliyekuwa mshambuliaji wa KMC, Daruweshi Saliboko aliyeongoza kwa kukifungia kikosi hicho mabao mengi ya Ligi Kuu, baada ya nyota huyo kufunga manne msimu wa 2025-2026.
Wengine waliojiunga na kikosi hicho ni kipa, Mussa Mbisa na beki wa kulia, Marco Mhilu ambao wametokea kwa maafande wa Tanzania Prisons ya jijini, Mbeya, wakiwa ni chaguo la kwanza kwa timu hiyo ya Dodoma Jiji kwa msimu huu wa 2026-2027.
PAMBA JIJI (2)
Pamba Jiji maarufu kwa jina la utani la ‘TP Lindanda’ au ‘Wanakawekamo’, inayofundishwa na Kocha Mkuu, Mkenya Francis Baraza, imesajili nyota wawili ambao ni beki wa kulia, Omary Manga kutoka Mtibwa Sugar na winga, Frank Ernest wa KMC FC.
NYINGINEZO
Katika timu zilizosajili mchezaji mmoja mmoja ni Yanga iliyomsajili winga, Erick Mwijage kutoka KMC FC, huku kwa upande wa watani zao wa jadi hapa nchini, Klabu ya Simba ikinasa pia saini ya beki wa kati, Ibrahim Abbas ‘Nindi’ kutokea KMC.
Nyota wengine ni beki wa kulia, Nickson Mosha aliyejiunga na Singida Black Stars akitokea KMC FC, beki wa kati, Laurent Alfred aliyesajiliwa na kikosi cha Coastal Union maarufu kwa jina la ‘Wagosi wa Kaya’, baada ya kuondoka Mtibwa Sugar.
Kwa upande wa TRA United ilimsajili mshambuliaji Kassim Shaibu ‘Mayele’ kutoka Mtibwa Sugar aliyeifungia mabao mawili Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026, ili kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji la timu hiyo msimu huu.