Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mo Salah, Kane watakavyochuana kubadili msimamo wa vinara wa mabao

Muktasari:

  • Na kinachoonekana ni kwamba, supastaa huyo wa kimataifa wa Misri anaweza kufikia kwenye namba nne kabla ya msimu huu wa Ligi Kuu England kufika tamati.

LONDON, ENGLAND: SUPASTAA wa Liverpool, Mohamed Salah amepanda kwa kasi kwenye orodha ya vinara wa mabao wa muda wote kwenye Ligi Kuu England, shukrani kwa kasi yake ya kutupia nyavuni karibu katika kila mechi msimu wa 2024-25.

Na kinachoonekana ni kwamba, supastaa huyo wa kimataifa wa Misri anaweza kufikia kwenye namba nne kabla ya msimu huu wa Ligi Kuu England kufika tamati.

Kwenye orodha ya wakali 10 waliofunika kwa kutupia nyavuni kwenye Ligi Kuu England ni wawili tu ndiyo wanaoendelea kukipiga hadi sasa ambao ni Mo Salah na straika wa Bayern Munich, Harry Kane.

Je, hao mastaa waliofanikiwa kutinga kwenye 10 bora ya vinara wa muda wote wa mabao kwenye Ligi Kuu England, wamepenya na kufika hapo baada ya kufikisha mabao mangapi?


10. Jermain Defoe – 162

Straika kiwembe kwenye kupasia mipira nyavuni kwenye nyakati za ubora wake. Defoe alicheza mechi nyingi kuliko mchezaji mwingine yeyote kwenye orodha hiyoo, lakini mabao yake aliyofunga akiwa na vikosi vya Tottenham Hotspur, West Ham United, Sunderland, Bournemouth na Portsmouth yamemfanya awe mmoja wa vinara wa muda wote kwenye Ligi Kuu England.

Akibarikiwa kasi, miguu yenye ufundi na mashuti ya kushtukiza, alifunga kila aina ya mabao na kuwamo kwenye orodha ya wachezaji watano tu waliowahi kufunga mabao matano kwenye mechi moja ya Ligi Kuu England, alipofanya hivyo kwenye mchezo dhidi ya Wigan katika msimu wa 2009-10.


9. Robbie Fowler – 163

Anatajwa kama mmoja wa wadunguaji asilia kabisa waliopata kutokea kwenye historia ya Ligi Kuu England kwa namna alivyokuwa akiwafanya makipa. Robbie Fowler aliibukia kama straika matata kabisa akitokea kwenye akademia ya Liverpool, ambapo alifunga mabao 30 katika michuano yote kwa misimu mitatu mfululizo, kuanzia akiwa na umri wa miaka 19 hadi 22. Fowler alikuwa na jicho la goli na alikuwa akifunga kwa miguu yote, huku msimu wake bora kabisa kwenye ligi ni ule aliofunga mabao 28 kwenye Ligi Kuu England katika msimu wa 1995-96, wakati akiwa na umri wa miaka 21. Fowler alifunga mabao 163 kwenye Ligi Kuu England na kuwamo kwenye orodha hiyo.



8. Thierry Henry – 175

Mfaransa Thierry Henry ameonekana kuwa chaguo la kila mtu kwenye orodha ya wachezaji bora zaidi waliowahi kutokea kwenye historia ya Ligi Kuu England, lakini kwenye orodha hii anashika namba nane. Hata hivyo, mabao yake 175 na asisti 73 alizofanya kwenye mechi 258, inamfanya kuwa mmoja wa wachezaji wenye wastani mzuri wa bao kwa mechi. Si tu, Henry alikuwa anafunga mabao makali, bali alikuwa akifanya hivyo kwa staili zote, huku nyingine zikishindwa kabisa kuigwa. Kingine ni kwamba staa huyo bado anabaki kuwa mwenyewe kwenye orodha ya wachezaji waliofikisha mabao 20 na asisti 20 ndani ya msimu, alipofanya hivyo 2002-03. Ni gwiji wa kweli kwenye Ligi Kuu England.


7. Frank Lampard – 177

Kama kuna mchezaji yeyote anayestahili pongezi kubwa kwenye orodha hii basi ni Frank Lampard. Akiwa ni kiungo pekee kwenye orodha hii ya mastaa 10 vinara wa mabao wa muda wote kwenye Ligi Kuu England, hilo limethibitisha juu ya ubora wa Mwingereza huyo katika kutikisa nyavu. Akijihakikishia kuwa mpiga penalti wa Chelsea kwa nyakati zake alizokuwa kwenye timu hiyo, kiungo huyo wa mabao alikuwa akifunga kutoka katika kila eneo na kwa staili zote. Mabao yake 22 na asisti 14 kwenye msimu wa ubingwa 2009-10 kinabaki kuwa kiwango chake bora kabisa ndani ya msimu moja, huku akiondoka kwenye Ligi Kuu England akiwa amefunga mabao 177.


6. Mohamed Salah – 184

Staa wa kizazi cha sasa, Mohamed Salah ameonyesha umahiri mkubwa wa kudumu kwenye kiwango bora cha soka kwa muda mfefu tangu alipotua kwenye kikosi cha Liverpool na kutamba Ligi Kuu England msimu wa 2017-18. Akisajiliwa kutoka AS Roma, msimu wake wa kwanza Anfield alivunja rekodi ya mabao katika msimu wa mechi 38. Mwanzoni akionekana kama mchezaji wa msimu mmoja, Mo Salah aliendelea kuwasha moto na kufanikiwa kufunga mabao 20 na kuendelea kwa misimu mitano, hivyo mechi tisa zilizobaki kumalizia msimu huu, atahitaji kufunga mara nne tu kufikia nafasi ya nne kwenye msimamo wa vinara wa mabao wa muda wote kwenye Ligi Kuu England. Sasa amefunga 184.


5. Sergio Aguero – 184

Hata muda mrefu, Sergio Aguero atashuka hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa vinara wa muda wote wa mabao kwenye Ligi Kuu England, lakini si jambo lenye kificho kwamba straika huyo wa Kiargentina ni mmoja wa wachezaji wa maana kabisa waliowahi kutokea kwenye ligi hiyo. Ni mfungaji wa mabao kwenye mechi kubwa, ikiwamo ile ya bao la mwisho lililoipa ubingwa Manchester City katika msimu waliochuana jino kwa jino na Manchester United. Aguero na mabao yake 184 kwenye Ligi Kuu England, yanamfanya kuwa kinara wa mabao kwenye kikosi cha Man City kwa upande wa ligi na hivyo kumpa mtihani wa kutosha Erling Haaland wa kwenda kuvunja rekodi yake.


4. Andrew Cole – 187

Straika wa zamani wa Manchester United pengine anaweza kuwa mchezaji asiyekubalika sana kwenye orodha hii, lakini Andy Cole alikuwapo pia kwenye enzi za Ligi Kuu England inacheza mechi 42 kwa msimu, ambapo alifunga mabao 34 katika msimu wa 1993-94, huku mabao yake ya jumla kwenye ligi ni 187 na la penalti ni moja tu. Pia ni mchezaji aliyefikisha kwa haraka mabao 50, alipofanya hivyo kwenye mechi 65 na kuwapiku wakali wa kutupia Alan Shearer na Ruud van Nistelrooy. Msimu wa 1993-94, alikuwa mchezaji wa kwanza kuwa kinara wa mabao na asisti na kuonyesha uhodari wake anapokuwa ndani ya uwanja.


3. Wayne Rooney – 208

Moja ya wachezaji bora kabisa waliopata kutokea kwenye Ligi Kuu England na Wayne Rooney anabaki kuwa mchezaji pekee aliyefunga zaidi ya mabao 200 na kuasisti 100 kwenye historia ya ligi hiyo. Ndiye kinara wa mabao kwenye klabu ya Manchester United na anabaki kuwa mchezaji aliyefikisha tarakimu mbili ya mabao mara nyingi kwenye Ligi Kuu England, akifanya hivyo kwa misimu 12. Rooney, ambaye ni mshindi mara tano wa Ligi Kuu England, ndiye mchezaji aliyecheza nafasi nyingi ndani ya uwanja kwenye ligi hiyo, ambapo alianza kama straika, kabla ya kutumika kwenye Namba 10 na baadaye, akamaliza soka lake akiwa kiungo wa chini. Amefunga mara 208 kwenye ligi.


2. Harry Kane – 213

Kwa mchezaji anayekupa uhakika wa mabao, hakuna straika mwenye uwezo wa kukuhakikishia hilo kumzidi Harry Kane. Kane amefikisha mabao 20 kwa msimu kwa misimu sita tofauti na alifikisha mabao 30 kwa msimu mara mbili tofauti kwenye Ligi Kuu England kabla ya kuondoka kwenda kujiunga na Bayern Munich kwa dili tamu kabisa. Ni mshindi mara tatu wa Kiatu cha Dhahabu, huku akiwa mmoja wa wachezaji watatu kwenye orodha ambao hawajaonja utamu wa kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England. Hata hivyo, taji la kuwa mfungaji mahiri haliwezi kumkosa akifunga mara 213 kwenye kikosi cha Tottenham, huku akiripotiwa kutaka kurudi kuvunja rekodi ya Alan Shearer.


1. Alan Shearer – 260

Kinara wa muda wote wa mabao Ligi Kuu England ni Alan Shearer. Katika kiwango chake bora alifunga mabao 260 katika mechi 441, huku akiasisti mara 64 na alifikisha idadi ya mabao 20 kwa msimu katika misimu saba tofauti. Alikuwa mfumania nyavuni mahiri kutokana na kushikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi ndani ya boksi, 227, huku akifunga penalti nyingi 56 na alitumia mechi chache za nyumbani kufikisha mabao 100, mechi 91. Alishinda ubingwa wa ligi mara moja wakati alipokuwa Blackburn Rovers na aligoma kwenda kujiunga na Manchester United, usajili ambao kama ungemfanyika basi angeenda kushinda mataji mengi, lakini aliamua kubaki Newcastle United.