Prime
Mtihani mwingine kwa Jabaar Simba
KLABU ya Simba inaendelea na maboresho ya kikosi hicho kwa ajili ya msimu wa 2026-2027, ambapo wachezaji sita hadi sasa tayari wametambulishwa, huku 10, wakipewa mkono wa kwaheri, ili wakatafute changamoto sehemu nyingine nje ya timu hiyo.
Wachezaji wapya waliosajiliwa ni Kelvin Nashon kutokea Pamba Jiji, Nathaniel Chilambo (Azam FC), Bakari Msimu (Coastal Union), Ibrahim Doumbia (AS Korofina), Keletso Makgalwa (Sekhukhune United FC) na Ibraheem Jabaar aliyetoka Stellenbosch FC.
Walioachwa ni Jonathan Sowah, Ladack Chasambi, Omary Omary waliojiunga Singida Black Stars, Mzamiru Yassin (TRA United), Awesu Awesu (Namungo FC), Chamou Karaboue (Al-Talaba SC), Moussa Camara, Naby Camara, Edwin Balua na Joshua Mutale Budo.
Miongoni mwa nyota waliokuwa katika mtihani ni Mnigeria Ibraheem Jabaar aliyejiunga na kikosi hicho akiwa mchezaji huru, baada ya kuachana na Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, kutokana na rekodi za wachezaji raia wa Nigeria waliocheza Simba.
Ibraheem Olalekan Jabaar aliyezaliwa Oktoba 24, 2002, alitambulishwa na Simba rasmi Julai 25, 2026, baada ya kuachana na Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, akicheza pia timu za Olisa FC ya kwao Nigeria na Maccabi Petah Tikva FC ya Israeli.
Nyota huyo ambaye ni chaguo la Kocha Mkuu, Steve Barker aliyefanya naye kazi awali akiwa na Stellenbosch FC, ana kazi ya kuonyesha kipaji chake, kutokana na rekodi za wachezaji wa Nigeria waliochezea Simba, kama Mwanaspoti linavyowaelezea.
AUGUSTINE OKEJEPHA
Nyota huyo alijiunga na Simba Julai 6, 2024, akitokea Rivers United ya kwao Nigeria baada ya kuonyesha kiwango kizuri kilichowavutia mabosi wa timu hiyo, ingawa licha ya matarajio makubwa aliyopewa ila mambo yalienda tofauti na kuondoka.
Kiungo huyo aliitumikia Simba msimu mmoja tu, licha ya kusaini mkataba wa miaka mitatu, ambapo alitua nchini akiwa ndiye mchezaji bora wa Ligi ya Nigeria msimu wa 2023-2024, akiwa na Rivers United, japo wasifu huo haukuweza kumbeba kikosini.
Okejepha aliyezaliwa Aprili 13, 2004, akizichezea Warri Wolves FC, Kano Pillars kisha Rivers United, alishindwa kupenya kikosi cha kwanza cha Simba kilichokuwa kinafundishwa na aliyekuwa Kocha Mkuu, Fadlu Davids na kuondoka Julai 14, 2025.
Akiwa na Rivers msimu wa 2023-2024, Okejepha alicheza mechi 26 za Ligi Kuu ya Nigeria na kuhusika katika mabao manne tu, baada ya kufunga bao moja na kuasisti matatu, ambapo kwa sasa nyota huyo anachezea timu ya Wolayta Dicha SC ya Ethiopia.
NELSON OKWA
Nelson Okwa alijiunga rasmi na Simba Agosti 4, 2022 na kutabiriwa mambo makubwa baada ya kuonyesha kiwango bora katika mechi ya kilele cha 'Simba Day', ambayo kikosi hicho kilishinda mabao 2-0, dhidi ya St George ya Ethiopia mwaka 2022.
Okwa aliyetokea Rivers United ya kwao Nigeria, alifunga bao moja katika mechi hiyo huku lingine likifungwa na Kibu Denis na kubeba matumaini kwa mashabiki wa Simba walioamini atafanya vizuri, ingawa mambo yalikuwa tofauti na matarajio hayo.
Nyota huyo aliyechezea pia Go Round FC ya Nigeria, alishindwa kuwika na kutolewa kwa mkopo kwenda Singida Black Stars zamani Ihefu na Septemba 1, 2024, alipewa rasmi mkono wa kwaheri na baadaye kujiunga na kikosi cha Delhi FC cha India.
VICTOR AKPAN
Akpan ni nyota mwingine aliyetabiriwa makubwa na mashabiki na wadau wengi wa soka nchini kutokana na kiwango chake bora alichokionyesha akiichezea Coastal Union ya mjini Tanga, ambapo hata hivyo, alivyotua tu mambo yalianza kwenda tofauti.
Kiungo huyo mkabaji, alijiunga rasmi na Simba Julai, 2022 kwa mkataba wa miaka miwili, japo aliutumikia nusu kisha baada ya hapo akatolewa kwa mkopo Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na safari yake na kikosi hicho ikaishia hapo.
Nyota huyo alijiunga na Simba kipindi ikiwa na benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Mserbia Zoran Maki ambapo baada ya kushindwa kuonyesha kiwango kilichotegemewa kama ilivyokuwa mwanzoni akiwa Coastal Union aliondoka rasmi Juni 20, 2023.
Akpan aliyeanzia soka la vijana mtaani kwao Nigeria na akaenda kwenye akademi mbalimbali, kisha kujiunga na timu ya Ligi Daraja La Kwanza ya City Stars, alinukuliwa akisema mwaka 2018 alikuja Tanzania kwa lengo la kufanya majaribio na Simba.
Kiungo huyo aliendelea kunukuliwa akisema, baada ya kuja Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 2018, alifanya majaribio na Simba wakati huo ikiwa chini ya Kocha, Mrundi Masoud Djuma Irambona, ingawa alifeli kisha kusajiliwa tena Julai, 2022.
JUNIOR LOKOSA
Junior Sewanu Lokosa aliyezaliwa Agosti 23, 1993, katika mji wa Badagry uliopo mji wa pwani na eneo la Serikali ya Mitaa katika Jimbo la Lagos, Nigeria, ni miongoni mwa washambuliaji walioingia katika mtihani wa jinamizi la kufanya vibaya.
Nyota huyo alitua Tanzania saa 7:45 mchana wa Jumamosi ya Januari 23, 2021 kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kupokelewa na aliyekuwa mkuu wa idara ya uendeshaji ya timu hiyo, Dk. Arnold Kashembe.
Mshambuliaji huyo alisaini mkataba wa miezi sita kwa ajili ya kukichezea kikosi hicho, huku lengo la usajili wake wakati huo ulikuwa ni kuitumikia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo kikosi hicho kilikuwa hatua yake ya makundi.
Lokosa alisajiliwa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika tu na sio vinginevyo kutokana na kikosi hicho kwa wakati huo kilikuwa tayari kina idadi ya wachezaji 10, raia wa kigeni wanaoruhusiwa kusajiliwa kwa kila timu ya Ligi Kuu Bara.
Wasifu wake ulisisimua wengi kwani kabla ya kujiunga Simba akiwa mchezaji huru, alichezea timu ya Esperance ya Tunisia na pia Kano Pillars na First Bank FC, huku akiwahi kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria ya 'Super Eagles'.
Akiwa na Kano Pillars, alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Nigeria mwaka 2018, baada ya kufunga mabao 19, katika mechi 21 tu, huku akifanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya katika timu za Ludogorets ya Bulgaria na Brann ya Norway.
Licha ya wasifu mkubwa kwake, ila tangu ajiunge na Simba wakati huo chini ya Kocha Mkuu, Mfaransa Didier Gomes Da Rosa, alishindwa kumshawishi na baadaye kupewa mkono wa kwaheri, licha ya kubeba matarajio makubwa wakati wa usajili wake.
Nyota huyo amechezea pia, Al Rayyan ya Qatar, Kwara United, Remo Stars FC, Sporting Lagos na Enyimba Aba zote za kwao Nigeria, aliyojiunga nayo Januari 31, 2025, akicheza mshambuliaji wa kati au winga ya kulia ingawa, kwa sasa yupo huru.
IBRAHEEM JABAAR
Jabaar anayecheza nafasi ya kiungo wa kati na wakati mwingine akishambulia kutokea katikati na pembeni, ni miongoni mwa wachezaji wengine raia wa Nigeria waliojiunga na kikosi hicho, ambao wamebeba matumaini makubwa kwa msimu wa 2026-2027.
Nyota huyo ana kazi ya kupigania malengo ya Simba inayotaka ubingwa wa Ligi Kuu ilioukosa kwa misimu mitano mfululizo na kushuhudia ukienda kwa watani zao wakubwa Yanga, kisha kutetea taji la Kombe la CRDB, iliolichukua msimu wa 2025-2026.
Mbali na Jabaar kupambania kutimiza malengo ya kikosi hicho kwa msimu wa 2026-2027, ila ana kazi ya kufanya kuhakikisha anaondokana na jinamizi baya la wachezaji raia wa Nigeria waliofanya vibaya, katika kikosi hicho kwa misimu iliyopita.