Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sophia: Wazazi walisema ‘no’, ‘uppercut’ si mchezo

SOPHIA Pict

Muktasari:

  • Anajivunia kuwa mwanamke, anapenda kuvaa mavazi ya jinsia hiyo na kwa maelezo yake mwenyewe, nyumbani kwake ana “vijora kama vitano hivi”, lakini akipanda ulingoni sura hubadilika anakuwa mpiganaji haswa na siyo bondia anayependa mapambano ya mchongo.

UKIMTAZAMA Sofia Ramadhani Hamisi akiwa nje ya ulingo huenda usiamini kwamba binti huyo ni mmoja wa mabondia wa kike wanaokuja juu kwa kasi katika ndondi za kulipwa nchini Tanzania.

Anajivunia kuwa mwanamke, anapenda kuvaa mavazi ya jinsia hiyo na kwa maelezo yake mwenyewe, nyumbani kwake ana “vijora kama vitano hivi”, lakini akipanda ulingoni sura hubadilika anakuwa mpiganaji haswa na siyo bondia anayependa mapambano ya mchongo.

Kauli hiyo inagusa moja kwa moja dhana ambayo imekuwa ikiwakumba baadhi ya wanamichezo wa kike kwamba michezo haipaswi kuwabadilisha.

“Kujieka kiume kwa wachezaji wengine ni maamuzi yao wenyewe, lakini mimi najieka kike kabisa. Nyumbani kwangu nina nguo nyingi sana za kike, nina vijora vingi sana kama vitano hivi na napenda kuvaa kama mwanamke nikimaliza mazoezi,” anasema.

Lakini, nyuma ya vijora hivyo na maisha yake ya kawaida ya kucheka, kupiga stori na kufurahia maisha, kuna bondia mwenye ndoto kubwa anayatamani mikanda mbalimbali, anayetamani kufika mbali kwenye ndondi za wanawake.

Huyu ni Sofia Ramadhani Hamisi, bondia anayesimamiwa na Zugo Sport Promotion, ambaye safari yake ya kufika ulingoni changamoto nyingi.

Mwanaspoti ilifunga safari kutoka Tabata Mwananchi hadi Gongo la Mboto Ulongoni, Dar es Salaam, ambako Sofia anaendelea na mazoezi ili kuwa bondia mkubwa.

SOPHI 01

SOKA LA MITAANI HADI ULINGONI

Kabla ya kuingia ulingoni, Sofia alikuwa na ndoto ya kuwa mchezaji wa soka, ambapo mapenzi yake katika michezo yalianza tangu akiwa shule mjini Morogoro, mji maarufu kwa kuzalisha vipaji vikubwa nchini kuanzia wanamuziki kama Stamina hadi mabondia kama Twaha Kiduku.

Akiwa shule, Sofia hakuwa mchezaji wa kawaida; alikuwa mchezaji tegemeo na nahodha aliyekuwa akiongoza timu yake ya shule katika mashindano mbalimbali ikiwemo ya Umitashumta.

“Mimi nilikuwa nacheza mpira wa miguu mitaani na shuleni, nilikuwa namba saba na namba 10 winga machachari kweli kweli. Nilikuwa naupenda sana mpira,” anasema Sofia.

Lakini kwanini aliuacha mpira wakati alikuwa na uwezo mkubwa? Sofia anasema kilichofanya aache ni changamoto ya kushikwa mkono kupelekwa sehemu fulani.

“Kule kwenye soka kulikuwa hakuna mdhamini wa kunishika mkono na kuninyanyua.  Unajua soka la wanawake bongo ili ufanikiwe na ufike mbali lazima uwe na mtu wa kukushika mkono, mtu wa kukupeleka sehemu kubwa na kukutambulisha,” anasema Sofia

“Kama huna huyo mtu, basi utaishia kucheza mechi za mitaani (ndondo) bila mafanikio yoyote . Ndio maana nikaamua kuuacha mpira na kuingia upande wa pili wa ngumi ambapo angalau naweza kupambana kwa nguvu zangu mwenyewe.”

Sofia anasema kama angeendelea kubaki kwenye soka la mtaani, hadi leo hii asingejulikana popote pale.

“Ningebaki kule mitaani nisingejulikana kabisa, ningekuwa nacheza tu bila kuonekana kwenye kioo. Lakini huku kwenye ngumi, japo nimeanzo hivi karibuni, sasa hivi naonekana kwenye kioo na watu wengi wananifahamu na kunisikia,” anasema bondia huyo.

SOPHI 02

ILIKUWAJE

Safari ya Sofia kwenye masumbwi ilianza kama utani mwaka 2023. Hakuwa na mtu wa karibu aliyemshawishi, bali mapenzi yalianza baada ya kukaa mbele ya runinga na kutazama mapambano mbalimbali ya ngumi yaliyokuwa yakirushwa na Azam TV.

“Nilikuwa napenda tu kuangalia yale mapambano ya ngumi kwenye TV. Kila yakirushwa nakaa naangalia sana. Kupitia pale, nikajikuta nimeingia kwenye mchezo huu na kuupenda kutoka moyoni,” anasema Sofia.

Katika kipindi hicho alipokuwa akitazama runinga, macho yake yalivutiwa sana na bondia wa kike ambaye alikuwa akifanya vizuri Stumai Muki.

 “Stumai ndiye bondia aliyekuwa ananivutia sana. Nilikuwa namfuatilia sana na ndoto zangu zilikuwa siku moja niwe bondia kama yeye, na pia nicheze.”

Baada ya pale alianza kupambania alichoamini ndipo akajiunga na Zugo Gym 2023 na baadaye miaka miwili baadaye ndoto yake ilitimia ya kucheza na Stumai.

Lilikuwa ni pambano la raundi nane lililopigwa mkoani Lindi, likiwa ni lake la kwanza la raundi nyingi tangu aingie kwenye ndondi za kulipwa, na Sofia anasimulia jinsi presha ilivyokuwa kabla ya kupanda ulingoni. “Presha ilikuwepo kubwa sana kabla ya pambano. Nilikuwa najiuliza: hivi huyu mtu atanipiga? Hivi nitamaliza kweli hizi raundi zote nane? Maana ilikuwa mara yangu ya kwanza kabisa kucheza raundi nyingi kiasi hicho. Lakini namshukuru Mungu, nilipanda ulingoni na kupambana kwa kiwango cha juu sana na kumaliza raundi zile.”

Ingawa alipoteza pambano hilo kwa pointi, Sofia anasema anatamani kurudiana na mpinzani wake.

“Nilipoteza kwa pointi lakini matokeo yaliyotoka hayakuniridhisha kabisa. Nilihisi nimeonewa na ndio maana leo na kesho namtamani sana Stumai, nataka nirudiane naye pambano la marudio ili nithibitishe ubora wangu.”

SOPHI 03

WAZAZI WAKATAA

Sofia anakumbuka jinsi wazazi wake walivyokuwa wakipinga uamuzi wake wa kuingia kwenye ngumi mwanzoni, wakidai kuwa binti wa kike kucheza ngumi ni kupoteza muda tu na ni jambo lisilo na maana.

“Mwanzo walikuwa wananipinga sana na kuongea maneno mengi kwamba naenda kupoteza muda tu. Lakini mimi nililazimisha na kupambana kwa kile ninachokiamini. Mwisho wa siku nilipofika hapa ndipo walipoanza kuamini sasa na sasa hivi wananiombea dua sana nikienda kupigana,” anasema bondia huyo.

Hata hivyo, Sofia anafichua kuwa mama yake hawezi kabisa kutazama pambano lake live kwa sababu ya uoga wa kumuona mwanaye akipigwa usoni. “Mamangu hawezi kabisa kuangalia nikiwa napigana ulingoni live, anaogopa sana. Anasubiri hadi pambano liishe apate matokeo, ndipo anakaa kwenye simu yake kuanza kuangalia video zangu taratibu.”


REKODI ZAKE, STUMAI WA KAWAIDA

Bondia huyo ana mapambano 10 ya kulipwa akishinda matano, sare mawili na kupoteza matatu. Ni rekodi nzuri kwa binti anayeanza ngumi za kulipwa akiwa ana miaka mitatu tu kwenye mchezo huo.

Lakini Sofia anasema kwake rekodi ya kupoteza hakukumfurahisha kwani alitamani kuwa na rekodi safi ya ushindi.

“Kupoteza yale mapambano matatu kuliniumiza sana kwa sababu nilitaka kuweka rekodi safi isiyo na madoa.”

Kuhusu kiwango cha Stumai Muki baada ya kukutana naye ulingoni, Sofia anajibu kwa kujiamini: “Baada ya kupigana naye, niliona ni bondia wa kawaida sana. Sikuona kitu cha ajabu kwake ambacho mimi siwezi kukimudu. Ndio maana nataka pambano lingine haraka sana.”

SOPHI 05

‘UPPERCUT’ INAMTESA

Katika maisha ya ngumi, kila bondia ana ngumi inayomtesa na inayompa mafanikio, lakini kwa Sofia anasema ngumi iliyowahi kumuumiza zaidi na inayompa changamoto kila siku mazoezini ni ngumi aina ya Uppercut au maarufu kama Mbakati, inayopigwa kutoka chini kwenda juu hasa kwenye kidevu au taya.

“Ngumi iliyowahi kuniuma sana na inayofanya niumie hadi leo ni uppercut. Hasa huku mazoezini inanipa tabu sana kutoka kwa mabondia wenzangu. Ili uikwepe, inahitaji umakini mkubwa sana ulingoni kwa sababu ni ngumi ya kushtukiza isiyo na mchezo,” anasema

Anasema mabondia wa kike nchini hakuna mwenye uwezo wa kuitumia hivyo akiwa mazoezini anapambana ili aweze kuwatesa wapinzani wake ulingoni.

“Kwa mabondia wa kike bongo, sijaona binti yeyote anayetumia hii ngumi ya Mbakati vizuri. Mimi nataka niwe binti wa kwanza nchini Tanzania kuitumia hii ngumi kwa weledi mkubwa na kuwaangusha wapinzani wangu ulingoni,” anaeleza.

Kimataifa, Sofia anamfuatilia sana bondia wa kike kutoka nchini Marekani, Claressa Shields, ambaye ana rekodi ya kutokupoteza pambano hata moja katika mapambano yake ya kulipwa.

“Claressa Shields ni bondia wa kipekee Marekani, namfuatilia sana na natamani siku moja niwe kama yeye. Ingawa hajawahi kupoteza na mimi nimeshapoteza mara tatu, bado nina nafasi ya kusafisha rekodi yangu na kuwa kama yeye duniani,” anasema Sophia.


KUHUSU UTUKUTU

Anapinga mtazamo wa jamii kuwa mabondia wote ni watukutu au walioshindwa maisha mtaani, hivyo wakaamua kukimbilia kwenye tasnia hiyo.

Bondia huyo anasema: “Hapana, wale wanaosema mabondia ni watukutu ni waongo. Utukutu ni akili ya mtu mwenyewe na tabia yake mtaani, lakini ngumi sio utukutu kabisa. Ngumi ni mchezo wa akili na nidhamu ya hali ya juu.”

Sofia anasema ukimkuta mtaani ni binti mwenye furaha, anayependa kupiga stori na kucheka na kila mtu.

“Mimi napenda sana stori, napenda kufurahi na watu na sitembei nikiwa nimekaba uso mtaani.”


MAHUSIANO, CHANGAMOTO

Kuhusu maisha yake ya mapenzi, Sofia anaweka wazi kuwa hana mpenzi wala hataki kusikia habari za mahusiano.

“Sihitaji mpenzi kwa sasa kabisa. Akili yangu yote ipo kwenye ngumi, sitaki mambo ya mapenzi yaniharibie malengo yangu,” anasema. Hata hivyo, ana mipango ya kupata familia na watoto huko mbeleni baada ya kustaafu masumbwi. “Kuhusu watoto na familia, hayo nitajua baadaye baada ya kumaliza kazi ya ngumi. Kuhusu idadi ya watoto, hiyo inategemea, naweza kupata hata watoto 10 mbeleni.”

Sofia anakataa tabia ya baadhi ya wanamichezo wa kike kujivika muonekano wa kiume. Yeye anajivunia ukike wake na anapenda kuvaa vizuri anapokuwa nyumbani au nje ya mazoezi .

Anasema: “Kujiweka kiume kwa wachezaji wengine ni uamuzi wao wenyewe, lakini mimi najiweka kike kabisa.

“Nyumbani kwangu nina nguo nyingi sana za kike, nina vijola vingi sana kama vitano hivi  na napenda kuvaa kama mwanamke nikimaliza mazoezi.” Changamoto yake kubwa kwa sasa nchini Tanzania ni uhaba wa mapambano na tabia ya mabondia wa kike kumkimbia ulingoni.

“Changamoto yangu kubwa ni upatikanaji wa mechi. Wakati mwingine unafanya mazoezi sana lakini hupati mechi ya kupigana kwa sababu mabondia wengi wa kike wananiogopa na wanakataa kucheza na mimi.”

Anaongeza kuwa mabondia wengi nchini sasa hivi wamezoea mapambano ya mchongo ambayo hayana ushindani wowote.

“Mabondia wengi wa sasa wanapenda mchongo tu, wanapenda fight za mchongo ambazo wanakuja kupigwa ngumi moja tu ya tumbo au kichwa basi mechi inaisha ili wachukue hela . Lakini mimi sio bondia wa mchongo, mimi ni bondia mkali na mtu wa vita,” anasema bondia huyo.

“Sasa promota akitaka kutupanga, yule opponent akisikia jina langu tu anakataa na kukimbia kwa sababu hawataki vita ya kweli wanataka mapambano mepesi ili washinde.”

SOPHI 06

OMBI LAKE, NJE YA NGUMI

Sofia ametoa ombi kwa mapromota kuandaa mapambano yenye ushindani na kuthamini ngumi za kike kama wanavyofanya kwa wanaume.

Anasema: “Kwenye mapambano mengi, unakuta mabondia wengi wa kiume wanapewa fight lakini kuna wanawake wanaofanya vizuri. Hii inatunyima fursa ya kuonyesha vipaji vyetu na kuingia kwenye kumi bora za Afrika na dunia.”

Nje ya ngumi, anasema: “Mimi sina kazi nyingine nje ya ngumi. Boxing ndio kazi yangu, ndio inayoniendeshea maisha yangu. Nakula, navaa na kuishi kwa kutumia ngumi kwa sababu nipo chini ya menejiment ya Zugo Sport Promotion ambayo inanipatia kila kitu ninachokihitaji.”

Anasema miongoni mwa mabondia wanaomvutia Tanzania ni Hassan Mwakinyo mwenye rekodi mbalimbali za kimataifa.

“Namkubali kwanza kwa sababu anatokea Tanga ambako ni asili yangu, lakini pili ni bondia mzuri ambaye amefungua njia kwa wengine kimataifa.”

Ili kulinda kiwango chake, Sofia anafuata kanuni za lishe na mafunzo anavyopewa na wataalamu wake.

“Kuna vitu vingi nimekatazwa kula ili kuweka mwili wangu sawa na kuwa na nguvu. Nimekatazwa kabisa kula pilipili, kunywa vitu vya baridi, na hizi juice za kemikali. Nazingatia sana hizi sheria ili kuhakikisha mwili wangu unakuwa fiti wakati wote,” anasema.


AWATAJA SHALULILE, ZAKOUANI

Licha ya kuacha soka, Sofia bado ana mahaba mazito na mchezo huo. Yeye ni shabiki lialia wa wananchi, Yanga.

“Mimi naipenda sana Yanga, naipenda mno! Yanga ndio timu yangu na nawapenda wachezaji wote wa Yanga bila ubaguzi,” anasema. Akizungumzia usajili wa msimu huu wa Yanga, Sofia  anawataja wachezaji wapya walioingia na kufanya vizuri kama vile mshambuliaji Peter Shalulile Peter na mawinga Housseine Zakouani na Albert Kangwanda.

“Simba kazi wanayo msimu huu! Yanga yetu imejipanga vizuri sana na wachezaji wapya wanapiga soka la maana,” anasema kwa utani. Moja ya ndoto zake kubwa wakati anacheza soka ilikuwa ni kuja kuichezea timu ya wanawake ya Yanga Princess , lakini anasema: “Mipango si matumizi. Mungu hakupanga nianzie kule, amenileta huku kwenye ngumi na nashukuru sana kwa hapa nilipofika.” Bondia huyo anasema ndani ya miaka 10 ijayo anataka kuwa bondia mwenye mkubwa mwenye mikanda mbalimbali “Mimi natamani kufika mbali na naamini jwa namna ninavyokwenda nitafikia kile ninachotarajia kuwa bondia mkubwa wa kike.”