AKILI ZA KIJIWENI: Yanga ikibeba ndoo inapaswa kushukuru mno!

Muktasari:
- Kwa hapa kijiweni tunaamini huu ni msimu ambao Yanga inauchukua ubingwa kwa staili ya kipekee inayopaswa kuwafanya mashabiki wake kumshukuru Mungu.
KAMA Yanga itachukua taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu inapaswa kushangilia sana pengine kuliko hata misimu mitatu iliyopita.
Kwa hapa kijiweni tunaamini huu ni msimu ambao Yanga inauchukua ubingwa kwa staili ya kipekee inayopaswa kuwafanya mashabiki wake kumshukuru Mungu.
Unajua kwa nini? Yanga ilianza kuongoza ligi na ikaitangulia timu iliyokuwa nafasi ya pili kwa zaidi ya pointi sita na kila mmoja akaamini itachukua ubingwa wa msimu huu kirahisi.
Ghafla mambo yakabadilika, Yanga ikaangusha pointi na watani wao Simba wakapambana hadi wakakaa juu ya msimamo wa Ligi Kuu na ikaonekana mbio za ubingwa zimeanza upya na ile jeuri ya Yanga mtaani ikapungua.
Simba nayo ikajichanganya, Yanga ikarejea juu lakini baadaye Simba ikarejea juu kabla ya Yanga kuchukua usukani ikitumia vyema yale matokeo ya sare ya mabao 2-2 ambayo Simba iliyapata dhidi ya Azam FC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Sasa jamaa wanashinda tu mechi zao mfululizo tena kwa idadi kubwa ya mabao ambayo yanaweza kuwapa faida hata ikitokea wakalingana pointi wakati huo safu yao ya ulinzi ikijitahidi kuhakikisha hairuhusu nyavu zao kutikiswa ili wawe na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Zile presha walizozipitia wakati watani wao wa jadi wamekaa kileleni kipindi fulani, inaonekana hawataki kukutana nazo tena kwa kushinda mfululizo tena katika wakati huu ambao ligi ipo katika hatua za lala salama na zimebaki raundi chache tu.
Wameshaanza kutamba huku mitaani kwa vile wanaona Simba itakuwa na kazi ngumu ya kucheza mfululizo viporo vyake huku ikiwa imechoshwa na mikikimikiki ya Kombe la Shirikisho Afrika hivyo wao wanaweza kujikuta wakitangaza ubingwa mapema.
Wakifanikiwa kuchukua ubingwa waache ti wawe na nyodo maana presha waliyokutana nayo msimu huu ni kiboko.