Prime
Barker aibuka na jipya Simba
KOCHA wa Simba, Steve Barker amesema timu yake inatakiwa kufunga mabao mengi zaidi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kupata ushindi kwenye mechi zake zijazo.
Simba jana ilikuwa mkoani Singida ikivaana na Singida BS kwenye mchezo wa tatu wa Ligi Kuu Bara na awali ilishashinda mechi mbili dhidi ya Kagera Sugar 2-0 na Pamba 2-1.
Simba inawania ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kuukosa kwa misimu mitano mfululizo lakini msimu huu inaonekana kujidhatiti zaidi.
Akizungumza na wachezaji wa timu hiyo juzi, Barker aliwaambia wanatakiwa kuwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga kwenye kila mechi ambazo watacheza, lakini wakati huohuo akiwataka kuhakikisha hawaruhusu mabao langoni kwao.
“Kocha amesisitiza sana suala la kufunga mabao mengi, amesema timu inatengeneza nafasi lakini zinashindwa kutumika, kwenye michezo mingi tunafika langoni hadi mara tisa lakini tunafunga mabao mawili inaonekana ni jambo ambalo halimfurahishi hata kidogo.
“Amesema ili timu ichukue ubingwa ni lazima nafasi nyingi ambazo zinatengenezwa kwenye mchezo zitumike kwa kuwa anaona kuna uwezekano wa kufunya hivyo kwa kuwa mazoezini hali hiyo inaonekana, nafasi nyingi zinazotengenezwa zinatumika,” kilisema chanzo kutoka kambini Simba.
Mbali na kuzungumzia suala hilo, Barker amesema kuwa timu yake itaendelea na mabadiliko kadhaa kwenye kikosi chake ili kuhakikisha inakuwa na balansi nzuri kuanzia kwenye eneo la ulinzi hadi ushambuliaji.
“Kuna wachezaji ambao bado hawajacheza, hilo naelewa, lakini taratibu kila mmoja atapata nafasi kwa wakati husika, lazima kuweka na mabadiliko kwenye kikosi leo anaweza kucheza huyu kesho yule, kila aliyesajiliwa kwenye timu hii ana umuhimu mkubwa hivyo ni suala la muda tu.”
Baada ya mchezo wa jana ambao unakuwa wa tatu kwa Simba ugenini sasa timu hiyo itarejea jijini Dar es Salaam kujiandaa na mechi dhidi ya Coastal Union Agosti 27 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.