Beki chipukizi aula Ligi Kuu Ukraine
Muktasari:
- Nyota huyo mwenye umri wa miaka 19 alikuwa Ukraine kwa mkopo akitokea Azam FC na alipewa nafasi na kuonyesha kiwango bora kilichowashawishi viongozi wa timu hiyo.
BEKI chipukizi wa Tanzania, Ismail Omar amesaini mkataba wa kudumu katika klabu ya Polissya Zhytomyr inayoshiriki Ligi Kuu ya Ukraine baada ya kuvutiwa na kiwango alichoonyesha kwenye klabu hiyo alipokuwa kwa mkopo akitokea Azam FC.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 19 alikuwa Ukraine kwa mkopo akitokea Azam FC na alipewa nafasi na kuonyesha kiwango bora kilichowashawishi viongozi wa timu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya klabu, Ismail ataanza kuitumikia timu ya vijana ya Polissya Zhytomyr U-21 akiendelea kufuatiliwa kwa karibu na benchi la ufundi la timu ya wakubwa kwa lengo la kumpandisha pindi atakapokuwa tayari.
Hatua hiyo inaonekana kuwa fursa kubwa kwa beki huyo, ambaye sasa atapata nafasi ya kuendelea kukua katika mazingira ya soka la Ulaya, akijifunza mbinu, kasi na ushindani unaoweza kumsaidia kufanikisha ndoto ya kucheza katika ligi kubwa zaidi barani humo.
Hilo linaonyesha mafanikio makubwa kwa Azam FC na ni uthibitisho wa kazi inayoendelea kufanywa na klabu hiyo katika kukuza vipaji vya vijana, huku ikizidi kujitengenezea sifa ya kuwa moja ya vituo vinavyozalisha wachezaji wanaoweza kupata nafasi kwenye soka la kimataifa.
Hivi karibuni timu hiyo iliwauza Arafat Masoud 'Konde Boy ENNPI ya Ligi Kuu Misri, Cyprian Kachwele ambaye kwa sasa anakipiga HFX Wanderers FC ya Canada ni miongoni mwa zao la Azam ambalo walianza kukuza vipaji hivyo tangu timu za U-17.