CAF yaipa Simba sharti zito, ikiibakiza Uhuru CAFCL
Muktasari:
- Hata hivyo, CAF imewapa Simba sharti la kuingiza mashabiki 6,000 tu katika Uwanja huo ambao kikawaida unaingiza mashabiki 23,000.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kwamba baada ya timu ya ukaguzi ya CAF kuukagua Uwanja huo, imewapa ruhusa ya kuutumia.
Hata hivyo, CAF imewapa Simba sharti la kuingiza mashabiki 6,000 tu katika Uwanja huo ambao kikawaida unaingiza mashabiki 23,000.
"Uwanja wa Uhuru tumeruhusiwa Simba Sports kuutumia kwa ajili ya michuano yetu ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Sisi tuliweka wazi dhamira yetu ya kucheza mechi zetu katika Uwanja wa Uhuru.
"CAF walikuja wakaukagua uwanja, wakatoa mapendekezo yao na taarifa ambayo tumepokea ni kwamba wameruhusu Simba tuutumie uwanja huo na yale mapendekezo na yale mapendekezo ambayo walielekeza yafanyika yamefanyika.
"Lakini wameweka ukomo wa idadi ya mashabiki ambao wanapaswa kuingia uwanjani. Ni mashabiki 6,000 pekee kutokana na miundombinu ya Uwanja wa Uhuru," amesema Ahmed Ally.
Mbali na Simba, timu nyingine ambayo itautumia Uwanja huo ni Singida Black Stars inayoshiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza amesema kwamba hadi sasa wana matumaini ya zaidi ya asilimia 90 kuutumia Uwanja wa Uhuru kwa mechi zao za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
"Tuliwaandikia mamlaka husika kuomba kuutumia Uwanja wa Uhuru na kwa sasa tunasuhiria majibu yao. Lakini tuna matumaini makubwa ya kucheza mechi zetu hapo kwa vile tumeshathibitishiwa na Meneja wa Uwanja, Ndugu Gordon Nsajigwa kwamba unakidhi kutumika kwa mechi za hatua ya makundi.
"Kwa hiyo tuna matumaini ya zaidi ya asilimia 90 kucheza mechi zetu hapo," amesema Massanza.
Simba ipo katika kundi C la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na timu za RS Berkane ya Morocco, Orlando Pirates ya Afrika Kusini na Colombe Sportive ya Cameroon.
Singida Black Stars ipo katika kundi C la Kombe la Shirikisho Afrika na timu za CR Belouizdad ya Algeria, AS Maniema ya DR Congo na Red Arrows ya Zambia.
Hata hivyo, timu za Yanga na Azam FC zitatumia Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.