Coastal Union kwenye kibarua kigumu mbele ya Simba leo
Muktasari:
- Mechi hiyo ni ya kwanza kwa Simba ikiwa nyumbani baada ya ushindi mechi tatu ugenini, huku Coastal iliyochapwa mbili na sare moja ikisaka ushindi wa kwanza. Timu hizo zinakutana kuanzia saa 1:00 usiku.
MSHIKEMSHIKE wa Ligi Kuu Bara unaingia raundi ya nne leo kwa mechi mbili, huku macho na masikio yakielekezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni jijini Dar es Salaam kushuhudia Simba ikicheza na Coastal Union.
Mechi hiyo ni ya kwanza kwa Simba ikiwa nyumbani baada ya ushindi mechi tatu ugenini, huku Coastal iliyochapwa mbili na sare moja ikisaka ushindi wa kwanza. Timu hizo zinakutana kuanzia saa 1:00 usiku.
Simba yenye mwenendo mzuri tangu msimu huu umeanza katika suala la kusaka pointi ikikusanya zote tisa, kikosi hicho kimeonekana kuwa na rekodi bora dhidi ya wapinzani wake.
Simba imeshinda mechi zote tatu ilizocheza ikianza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagea Sugar, Agosti 16, 2026, kisha ikaichapa Pamba Jiji 2-1, Agosti 19, 2026 na ushindi kama huo mbele ya Singida Black Stars, Agosti 22, 2026. Kwa upande wa Coastal Union inayosaka ushindi wa kwanza msimu huu ilichapwa bao 1-0 na Mashujaa FC, Agosti 15, 2026, ikachapwa 4-1 na Yanga, Agosti 20, 2026, kisha ikatoka sare ya bao 1-1 na TRA United, Agosti 24, 2026.
Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana ilikuwa ni katika mechi ya Kombe la CRDB hatua ya nusu fainali na Simba kushinda mabao 4-0, Juni 20, 2026, kisha kutinga fainali na kuchukua taji hilo kwa kuifunga Azam FC bao 1-0, msimu wa 2025-2026.
Kwa upande wa Ligi Kuu Bara, mara ya mwisho kukutana ilikuwa Mei 21, 2026 ambapo Simba ilishinda mabao 2-1 yaliyofungwa na Libasse Gueye na Anicet Oura, huku bao la Coastal Union likifungwa na Maabad Maulid.
Coastal Union inaingia katika mechi ya leo na kibarua kigumu cha kupata ushindi wa kwanza msimu huu, huku nyingine ni ya kuifunga pia Simba, kwa sababu mara ya mwisho timu hiyo kushinda kwenye Ligi Kuu Bara dhidi ya mpinzani wake huyo iliibuka na ushindi wa bao 1-0, Machi 23, 2014.
Licha ya mwanzo mzuri kwa Simba, lakini moja ya jambo la kuepuka ni mwendelezo wa kadi nyekundu kwa wachezaji baada ya kushuhudia kila mechi wakionyeshwa ambao ni David Kameta ‘Duchu’, Ibraheem Jabaar na Anthony Mligo.
Akizungumzia mechi hiyo, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola alisema licha ya kikosi hicho kuanza vizuri na kupata matokeo waliyokusudia wanaiheshimu Coastal Union bila kujali mwenendo iliioanza nao msimu huu.
“Ni mechi muhimu kwetu kwa sababu ndio ya kwanza nyumbani baada ya kucheza tatu ugenini, tumejipanga vizuri kuanza na ushindi na kuwafurahisha mashabiki zetu watakaojitokeza,” alisema Matola.
Kocha Mkuu wa Coastal Union, Fikiri Elias alisema kupata pointi moja mechi ya mwisho dhidi ya TRA United ilikuwa ni jambo nzuri ili kurejesha morali ya wachezaji, licha ya kukiri ugumu anaoenda kukutana nao mbele ya Simba.
“Wenzetu wameanza vizuri na wana morali ya hali ya juu tofauti na sisi, Simba ni timu inayotengeneza nafasi katika kila maeneo na kutegemea kumiliki zaidi mpira, hivyo, tuko tayari kukabiliana na changamoto hiyo nyingine,” alisema Fikiri.
MASHUJAA v KAGERA SUGAR
Kabla ya Simba dhidi ya Coastal Union, saa 10:00 jioni itapigwa mechi kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, Mashujaa itaikaribisha Kagera Sugar, ambayo tangu msimu umeanza haijaonja ladha ya ushindi.
Timu zote zinakutana zikiwa hazina mwenendo mzuri hadi sasa, ambapo kwa Mashujaa ilianza msimu huu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, kisha kikosi hicho kikachapwa bao 1-0 na Fountain Gate na kipigo kingine cha mabao 2-1 mbele ya Mbeya City.
Kwa upande wa Kagera iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kushuka 2024-2025 ilianza kwa kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Simba, ikatoka sare ya bao 1-1 na Singida Black Stars, kisha kuchapwa na Geita Gold mabao 6-2.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika zilifungana bao 1-1. Pia mara ya mwisho kukutana katika Ligi Kuu, Mei 12, 2025, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba na Mashujaa ilishinda bao 1-0.
Kocha Mkuu wa Mashujaa, Amani Josiah alisema miongoni mwa mambo yaliyowagharimu katika mechi mbili ni makosa binafsi ya wachezaji eneo la kujilinda, jambo ambalo amelifanyia kazi.
Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Juma Kaseja alisema licha ya matokeo waliyopata mechi ya mwisho ya kuchapwa mabao 6-2, alikaa na wachezaji na kuwajenga kisaikolojia, huku akiwataka kupambana na kusahau yaliyopita.