Dakika 90 zilizobeba mambo mawili
Muktasari:
- Katika mechi hiyo, jambo kubwa linaloweza kutokea ni la kutangazwa kwa kocha mpya wa kikosi hicho atakayechukua nafasi ya Manqoba Mngqithi aliyeondoka Oktoba 24, 2026, baada ya kufikia makubaliano ya pande mbili ya kuvunja mkataba wake.
YANGA inashuka tena kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, jijini, Dar es Salaam kucheza mechi ya raundi ya 10, ya Ligi Kuu Bara, huku ikibeba mambo mawili muhimu yanayoweza kutokea leo kuanzia saa 1:00 usiku.
Katika mechi hiyo, jambo kubwa linaloweza kutokea ni la kutangazwa kwa kocha mpya wa kikosi hicho atakayechukua nafasi ya Manqoba Mngqithi aliyeondoka Oktoba 24, 2026, baada ya kufikia makubaliano ya pande mbili ya kuvunja mkataba wake.
Jambo la pili, ni la kuhakikisha kikosi hicho kinaendeleza mwenendo mzuri katika Ligi Kuu Bara, ili kupunguza gepu la pointi na Simba inayoongoza, baada ya mechi iliyopita kuwafunga maafande wa Mashujaa FC mabao 2-1, Oktoba 27, 2026. Miongoni mwa kocha anayetajwa huenda akatambulishwa leo, ni Mjerumani Sead Ramovic ambaye alijiuzulu, Februari 4, 2025, kwa makubaliano ya pande mbili, ingawa, kwa sasa anatajwa yupo katika hatua za mwisho za kurejea ndani ya kikosi hicho.
Katika mechi tisa iliyocheza Yanga hadi sasa, imeshinda saba, sare moja na kupoteza pia moja, ikiwa nafasi ya pili na pointi 22, huku Kagera iliyocheza 10, ikishinda moja, sare tatu na kupoteza sita, ikishika nafasi ya 15 na pointi sita.
Kagera inakutana na Yanga ikikabiliwa na rekodi ngumu, kwani katika mechi 11, za Ligi Kuu Bara zilizopita, haijashinda yoyote, ikichapwa tisa na kutoka sare mbili, huku mara ya mwisho zilipokutana ilichapwa pia mabao 4-0, Februari 1, 2025.
Katika mechi hiyo ya Februari 1, 2025, mabao ya Yanga yalifungwa na Clement Mzize dakika ya 32, Mudathir Yahya dakika ya 60, Pacome Zouzoua kwa penalti ya dakika ya 78 na aliyekuwa pia mshambuliaji wa timu hiyo, Kennedy Musonda dakika ya 86.
Mara ya mwisho kwa Kagera Sugar kuifunga Yanga katika Ligi Kuu Bara, ilikuwa ni ushindi wa mabao 3-0, Januari 15, 2020, kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini, Dar es Salaam, ambapo kwa wakati huo ilifundishwa na Kocha Mkuu, Mbelgiji Luc Eymael.
Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Eymael tangu ajiunge na Yanga, ambapo mabao ya Kagera yalifungwa na Yusuph Mhilu, Ally Ramadhan ‘Kagawa’ na Peter Mwalyanzi, huku aliyekuwa kiungo wa Yanga, Mohamed Issa ‘Banka’ akionyeshwa kadi nyekundu.
Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Simo Dladla amesema licha ya kuiheshimu Kagera Sugar ila malengo yao ni kuhakikisha wanafanya vizuri na kupata pointi tatu nyumbani, huku akiwataka mashabiki kuendelea kujitokeza kwa wingi ili kuwapa zaidi motisha.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Cedric Kaze amesema anafurahia kukutana na timu aliyowahi kuifundisha misimu ya nyuma, ambapo licha ya kukiri Yanga ina wachezaji wanaoweza kuamua matokeo, ila wamekuja ugenini kutafuta ushindi.
POLISI TZ VS GEITA GOLD
Mechi nyingine ya mapema leo saa 10:00, alasiri, itachezwa kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi, ambapo maafande wa Polisi Tanzania iliyochapwa bao 1-0, dhidi ya Namungo FC, itaikaribisha Geita Gold iliyotoka sare na TRA United ya bao 1-1.
Katika mechi hiyo ya leo ni ya pili msimu huu kwa Polisi Tanzania kucheza kwenye Uwanja wa Ushirika, tangu iliporejea ikitokea Sheikh, Amri, Abeid, Arusha, huku ikitoka sare ya kufungana bao 1-1, dhidi ya Pamba Jiji, Oktoba 23, 2026.
Timu hiyo inayofundishwa na Kocha Mkuu, Mbwana Makata, inaingia katika mechi hiyo ya leo ikisaka ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, tangu mara ya mwisho kwa kikosi hicho cha maafande kilipoichapa Mbeya City mabao 2-0, Septemba 12, 2026.
Kwa upande wa Geita Gold inayofundishwa na Kocha Mkuu, Zubery Katwila, haina mwenendo pia mzuri, kwani imecheza mechi saba mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ushindi, tangu mara ya mwisho ilipoichapa Kagera Sugar mabao 6-2, Agosti 22, 2026.
Katika mechi 10, ilizocheza Polisi imeshinda tatu, sare tatu na kupoteza nne, ikiwa nafasi ya tisa na pointi 12, huku Geita Gold iliyocheza pia 10, ikishinda mbili, sare tatu na kupoteza tano, ikishika nafasi ya 12 na pointi zake tisa.