Dora: Kassali ndiye aliyeamua mechi dhidi ya Singida
Muktasari:
- Dora alisema pamoja na matokeo hayo, ameridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake huku akimtaja kipa wa Simba, Mahamadou Kassali kuwa mmoja wa walioamua matokeo ya mchezo kwa kuokoa nafasi mbili za wazi ambazo zingebadili mwelekeo wa mchezo huo.
KOCHA msaidizi wa Singida Black Stars, Kapiten Dora, ameisifu Simba baada ya timu yake kupokea kichapo, akisema walitarajia mchezo mgumu kutokana na timu hizo kufahamiana vizuri.
Dora alisema pamoja na matokeo hayo, ameridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake huku akimtaja kipa wa Simba, Mahamadou Kassali kuwa mmoja wa walioamua matokeo ya mchezo kwa kuokoa nafasi mbili za wazi ambazo zingebadili mwelekeo wa mchezo huo.
“Tulijua tangu mwanzo ungekuwa mchezo mgumu kwa sababu tunacheza ligi moja na tunaelewana vizuri lakini nimeridhishwa na kiwango tulichokionyesha. Tulicheza mechi kubwa,” alisema Dora.
Kocha huyo alisema Singida ilitengeneza nafasi kadhaa za kufunga, lakini ubora wa kipa wa Simba uliwafanya washindwe kuzitumia. “Ningependa kutoa pongezi maalumu kwa kipa wa Simba, alifanya kazi kubwa sana, kulikuwa na mipira miwili ambayo ilipaswa kuwa mabao, lakini aliidaka vizuri na kuinyima timu yetu nafasi ya kusawazisha au kubadili mchezo,” alisema.
Licha ya kuondolewa kwenye michuano hiyo, Dora alisema anaona maendeleo makubwa ndani ya kikosi chake ikilinganishwa na walivyoanza mashindano hayo.
“Tulipoanza hapa hali ilikuwa ngumu kidogo, lakini kadri siku zinavyokwenda na mazoezi yanavyoendelea, naona maendeleo makubwa kwa wachezaji. Hilo linatupa imani kubwa kuelekea msimu mpya,” alisema. Kwa mujibu wa Dora, ushiriki wa Singida Black Stars katika Kombe la CECAFA Kagame umeisaidia benchi la ufundi kupata picha ya maeneo yanayohitaji kuboreshwa kabla ya kuanza kwa mashindano ya ndani na Kombe la Shirikisho Afrika.