Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ishu ya uwanja kuteka mkutano mkuu Yanga


UKIKUTANA na wanachama wakiwa wamevaa jezi za njano na kijani leo wakielekea maeneo ya Masaki tambua hakuna mechi bali una jambo moja tu la mkutano mkuu wa klabu ya Yanga ambapo ishu ya Uwanja Mpya wa timu hiyo inasubiriwa kwa hamu ili majibu yake yatoke.


Hivi karibuni Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said alisema klabu hiyo itaanza ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo maeneo ya Jangwani na ndani ya mwaka mmoja utakuwa umekamilika ingawa hadi sasa ujenzi wake haujaanza pamoja na kwamba alisema utaanza mara moja.

Yanga watakuwa na mkutano mkuu ambao utabeba ajenda 14 lakini kati ya hizo kuna ajenda tatu zitakazobeba uzito wa mkutano huo utakaofanyika Ukumbi wa The Super Dome, Masaki.

Ajenda za moto ambazo zitabeba usikivu wa mkutano huo ni ile ya kupitia mapendekezo ya uwekezaji ambapo hapa wanachama wa mkutano mkuu watakwenda kufanya maamuzi yatakayotoa hatma ya mchakato wa ujenzi wa uwanja wao mpya ambao unatarajiwa kujengwa.

Kwenye mkutano huo wanachama hao watapewa kwa undani taarifa kutoka serikalini mambo ambayo wanatakiwa kurekebisha kabla ya kuendelea kwa mchakato huo wa ujenzi wa uwanja huo ambayo ni lazima mabadiliko yake tafanywe na mkutano huo.

Ajenda nyingine nzito itakuwa ni ile ya kupitia mapendekezo ya marekebisho ya katiba ya klabu hiyo, ambapo hapa yatakwenda kufanyiwa kazi matakwa ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Mkutano huo utakwenda kubadilisha namna ya upatikanaji wa Makamu wa Rais ambaye anatakiwa kupatikana kwa njia ya kuteuliwa na sio kuchaguliwa kama ambavyo inafanyika sasa.

Mabadiliko hayo yakifanyika, yatamfanya Arafat Haji ambaye ndiye mgombea pekee wa nafasi hiyo, kuwa kiongozi wa mwisho ambaye atatokana na kuchaguliwa ambapo baada yake, Yanga itakuwa na makamu wa kuteuliwa na rais ambaye atatokana na viongozi wa Kamati ya Utendaji watakaochaguliwa. Ajenda nyingine ya tatu nzito ambayo itaubeba mkutano huo ni ile ya uchaguzi mkuu ambapo vita itakuwa kupatikana kwa wajumbe watano wa nafasi za ujumbe wa kamati ya utendaji.

Kwenye mabadiliko hayo pia wanachama wa mkutano mkuu watabariki, mabadiliko ya kuingizwa kutambulika kwa timu zingine kwenye katiba zikiwemo timu ya wanawake ya Yanga Princess, vikosi tofauti vya vijana,kuanzia U9, U 13, U 15, U 17 na U 20.

Mabadiliko mengine  yatakuwa kurekebisha mjumbe kutoka bodi ya wadhamini asiwe sehemu ya wawakilishi wa klabu katika bodi na badala yake aingie makamu wa rais.


HERSI/ARAFAT KIRAHISI

Hapana shaka hakuna wasiwasi juu ya kushinda kwa rais na makamu wake kwani ni wazi injinia Hersi Said hata kama asifanye kampeni atashinda sambamba na Arafat Haji kutokana na kuwa wagombea pekee, wanaotaka kutetea nafasi zao.


PRESHA IPO HAPA

Presha kubwa itakuwa kwa wagombea 16 wa ujumbe ambao wanatakiwa kupatikana watano kwenye kundi hilo, watakaokwenda kuunda kamati ya utendaji kwa wajumbe wa kuchaguliwa huku wakisubiri wawili watakaochaguliwa na rais wa klabu.


BADO WANAUTAKA

Katika wagombea hao 16, wamo wajumbe wanaotaka kutetea viti vyao wakiwemo Alexander Ngai, Rodgers Gumbo, Yanga Makaga, Munir Seleman na Seif Gulamali huku Gerrard Kihinga ambaye alikuwepo kwenye baraza lililopita akiwa mjumbe wa kuteuliwa naye akigombea tena.


WAGOMBEA WAPYA HAWA HAPA

Wagombea wengine ni Injinia Mustapha Himba, Prisca Kishamba, Julius Koyi, Saady Khimji, Freddy Mahembe, Mshindo Hamza Msola, Issa Mangungu, Farid Afif, Mohammed Mwenda na Mzee Mwinyi.

Wagombea hao 16 wamekuwa wakichuana kwenye majukwaa mbele ya wanachama kuuza sera zao ndani ya siku nane za kampeni, zilizoanza Julai 25 mpaka jana Agosti Mosi ilipokuwa mwisho wa kampeni.


MAKOCHA NDANI

Kwenye mkutano huo mpaka jana, kulikuwa kukiwekwa mazingira sawa ya benchi la ufundi jipya la timu hiyo chini ya kocha Msauz Manqoba Mngqithi atakapotambulishwa na wasaidizi wake mbele ya wanachama wa mkutano mkuu huo.

Yanga pia kwenye mkutano huo itaweka wazi bajeti yake mpya ya msimu ujao, kwenye msimu ambao unaonekana utakuwa na ushindani mkubwa huku klabu hiyo itarudi tena kuhitaji kuchukua mataji ya ndani, pia kufanya vizuri kimataifa itakaposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuishia hatua ya makundi msimu uliopita.

Mbali na makocha tetesi zimesema kunawezakana kuwa na mchezaji mmoja au baadhi ambao wamesajiwa kwenye timu hiyo msimu huu.