Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kiungo Simba arejeshwa, sababu yatajwa


SIMBA imeamua kumrudisha mazoezini kiungo, Alassane Kante baada ya mpango wa kumuuza katika dirisha kubwa la usajili kugonga mwamba, huku Kocha Mkuu, Steve Barker akihitaji uwepo wa mchezaji huyo kwenye kikosi chake.


Inaelezwa viongozi wa Simba walikuwa tayari kumuuza Kante ndiyo sababu kuamua kumuondoa kwenye mfumo wakiamini kuna timu itanasa saini yake.

Mwanaspoti limepenyezewa kuwa, kabla ya dirisha kufungwa Agosti 15, 2026, Kante alikuwa na ofa kadhaa kutoka timu za Afrika Kaskazini, lakini JS Kabylie ya Algeria ndiyo ilikuwa siriazi kwenye harakati za kumnasa kiungo huyo raia wa Senegal. Nyingine iliyotajwa ni Raja Casablanca ya Morocco inayofundishwa na Nasredinne Nabi.

Taarifa kutoka Simba zimeeleza kuwa, JS Kabylie iliweka mezani ofa ya Sh450 milioni kwa ajili ya kumnunua Kante, lakini Simba ilikuwa ikihitaji Sh780 milioni ili kumuuza.

Chanzo cha ndani ya Simba kiliambia Mwanaspoti kuwa, uamuzi wa kuweka dau hilo ulitokana na ukweli kwamba Kante bado ana mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo.

“Kulikuwa na ofa kadhaa kutoka nje, lakini JS Kabylie ndiyo iliyokuwa siriazi zaidi. Walifika Sh450 milioni, lakini Simba ilikuwa inataka Sh780 milioni kwa sababu bado ana mwaka mmoja kwenye mkataba. Mpaka dirisha linafungwa hawakufikia makubaliano,” kilisema chanzo hicho.

Baada ya dili hilo kushindikana, Simba imeamua kumrudisha Kante kwenye mazoezi ya timu huku ikisubiri kufanya uamuzi hadi dirisha dogo kama itamuuza au itamvunjia mkataba.

Awali makubaliano ya Simba na Kante baada ya kuvunja mkataba wake na kumtoa kwenye mfumo, alitakiwa kulipwa zaidi ya Sh90 milioni, kiasi ambacho alikuwa akisubiri akabidhiwe aendelee na maisha mengine.

Kinachompa nafasi nyingine ni mahitaji ya Barker, ambaye anahitaji kiungo mwenye uwezo wa kukaa mbele ya mabeki, kukaba na kuvunja mashambulizi ya wapinzani kabla hayajafika kwenye eneo la hatari.

Kante ana sifa hizo na tayari ameshaonyesha uwezo wake kwenye eneo hilo tangu alipojiunga na Simba mwanzoni mwa msimu wa 2025-2026 akitokea CA Bizertin ya Tunisia.

Hata hivyo, changamoto kubwa iliyopo ni namna gani kama atapata nafasi kuonyesha ubora wake kwa Barker ambaye bado anamuhitaji na mipango ya baadhi ya viongozi ambao awali hawakuwa wakimuweka Kante kwenye hesabu za kikosi hicho msimu huu.


TAKWIMU ZAKE

Msimu uliopita, Kante alicheza mechi 24 za Ligi Kuu Bara akitoa asisti mbili na kuisaidia Simba kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo.

Kwenye michuano ya kimataifa, kiungo huyo alicheza mechi tano za makundi, Simba ikimaliza mkiani mwa kundi D ikikusanya pointi tano.


WALIOPO

Kwenye eneo analocheza Kante, Simba imeongeza wachezaji wawili wapya, Kelvin Nashon kutoka Pamba Jiji na Ibraheem Jabaar aliyetokea Stellenbosch ya Afrika Kusini.

Jabaar ndiye aliyeonekana kupata nafasi mapema zaidi, akianza katika mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Kagera Sugar kabla ya kuanza pia dhidi ya Pamba Jiji, ambako alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea faulo mpinzani.

Nashon, kwa upande wake hajaanza katika michezo hiyo mitatu iliyopita, akitokea benchi, jambo linaloacha nafasi ya ushindani katika eneo hilo na kumpa Kante sababu ya kuamini kuwa bado anaweza kupigania nafasi yake.

Hata hivyo, Kante hatakuwa na kazi nyepesi, kwani Barker ndiye atakayefanya uamuzi wa mwisho kuhusu aina ya kiungo anayemtaka kwenye mfumo wake.

Kocha huyo anahitaji kiungo mwenye uwezo wa kukaba, kulinda eneo la mbele ya mabeki na pia kusaidia timu wakati wa kujenga mashambulizi, kitu ambacho Kante amekuwa akifanya katika kikosi cha Simba.

Msimu uliopita, Kante alikuwa akicheza katika eneo hilo pamoja na Yusuph Kagoma, ambaye naye hakuanza katika michezo miwili dhidi ya Pamba Jiji na Singida Black Stars, hali iliyokuwa ikimpa Kante nafasi kubwa ya kuonekana kwenye kikosi.