KVZ yatupwa nje CAF ikichapwa 3-0 nyumbani
Muktasari:
- Katika mchezo wa leo, mabao ya Asswehly yote yalifungwa kipindi cha pili kupitia Otto John dakika ya 69 akimalizia mpira wa kona, kisha Mohammed Sola akaongeza la pili dakika ya 75, huku dakika 90+5, Zad Abukhatwa akihitimisha ushindi huo kwa kufunga bao la tatu akitokea benchi.
ASSWEHLY SC imefanikiwa kutinga hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada kuondoka na ushindi wa mabao 3-0 katika ardhi ya Zanzibar katika mchezo wa marudiano dhidi ya KVZ uliochezwa leo Septemba 13, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kisiwani hapa.
Ushindi huo umeifanya Asswehly kuiondosha KVZ kwa jumla ya mabao 4-0, baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Libya wenyeji kushinda 1-0.
Katika mchezo wa leo, mabao ya Asswehly yote yalifungwa kipindi cha pili kupitia Otto John dakika ya 69 akimalizia mpira wa kona, kisha Mohammed Sola akaongeza la pili dakika ya 75, huku dakika 90+5, Zad Abukhatwa akihitimisha ushindi huo kwa kufunga bao la tatu akitokea benchi.
Kipindi cha kwanza, KVZ ilionekana kuanza vizuri wakati ambao Asswehly ikicheza zaidi nyuma na kuruhusu mashambulizi, lakini wenyeji wakashindwa kutumia nafasi hiyo kufunga.
KVZ ilijarabu kupeleka mashambulizi mawili ya hatari kwenye lango la wapinzani wao hao kupitia mshambuliaji Mudrik Gonda na winga Agustino Chalamba 'Kaseke', lakini Asswehly ilikaa imara muda wote wa kipindi cha kwanza ikilinda ushindi wake wa nyumbani.
Baada ya mpango wao wa kipindi cha kwanza kujilinda kufanikiwa, ndipo kipindi cha pili Asswehly ilipobadili mbinu na kufunga mabao hayo yaliyotanua zaidi ushindi wao.
KVZ licha ya kushindwa kupindua matokeo ikiwa nyumbani, lakini winga wa kikosi hicho, Agustino Chalamba 'Kaseke' alionekana kwuasumbua wapinzani wao japo mashambulizi yake hayakuzaa matunda.
Winga huyo alikoseana katika mchezo wa kwanza uliochezwa ugenini baada ya kufiwa na mama yake, hivyo akaachwa kwenye msafara uliokwenda Libya na kuchapwa bao 1-0.
Mbali na Kaseke, winga wa kushoto wa KVZ, Zuberi Abdulla aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Suleiman Kidawa, naye alionekana kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji na kuipa uhai timu hiyo kusogeza mashambulizi mbele akiitumia vizuri spidi alionayo.
KVZ kichapo hicho kinahitimisha safari yao ya kimataifa msimu huu ikiungana na wenzao, KMKM ambao jana Jumamosi wakiwa Libya, walikubali kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Al Ahli Tripoli.
KMKM iliyokuwa ikiiwakilisha Zanzibar katika Kombe la Shirikisho Afrika, imeondolewa hatua ya kwanza ya mashindano hayo kwa jumla ya mabao 7-0, baada ya mchezo wa kwanza nyumbani kufungwa 3-0.