Makame ajipa muda kurejesha ufiti
Muktasari:
- Makame ambaye msimu uliopita aliichezea TRA United, alisema anatarajia kurejea uwanjani katika usajili wa dirisha dogo utakaofunguliwa Januari 2027, huku kwa sasa akiendelea na programu maalumu ya mazoezi ya kumrudisha katika kiwango bora cha utimamu wa mwili.
KIUNGO wa kati, Abdulaziz Makame, amesema kwa sasa ameamua kukaa pembeni ili kujipa muda wa kurejesha utimamu wa mwili, baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yakimsumbua msimu uliopita wa 2025-2026.
Makame ambaye msimu uliopita aliichezea TRA United, alisema anatarajia kurejea uwanjani katika usajili wa dirisha dogo utakaofunguliwa Januari 2027, huku kwa sasa akiendelea na programu maalumu ya mazoezi ya kumrudisha katika kiwango bora cha utimamu wa mwili.
“Nimepona, ila nimeona ni vizuri nikae pembeni nifanye mazoezi ya programu maalumu ya kuniweka fiti. Nipo Dar es Salaam, uwanjani mtaniona hadi litakapofunguliwa dirisha dogo la usajili,” alisema Makame.
Akizungumzia ushindani wa Ligi Kuu Tanzania, Makame alisema kiwango cha ushindani kinazidi kuongezeka kila msimu, hivyo mchezaji anatakiwa kuwa katika hali nzuri ya kiafya na kimwili ili kukabiliana na changamoto za ligi.
“Ligi Kuu kila msimu inakuwa ngumu na ya ushindani wa hali ya juu, ndiyo maana mchezaji anatakiwa awe fiti kwa ajili ya kukabiliana na ushindani, hasa kuisaidia timu ambayo inakuwa imekuajiri,” alisema.
Makame, ambaye amewahi kuzichezea Simba na Yanga kwa nyakati tofauti, alisema uzoefu wake katika Ligi Kuu umemfundisha umuhimu wa ushindani wa timu pamoja na ushindani wa namba katika kikosi hicho.
Alisema ushindani huo ni sehemu muhimu inayowafanya wachezaji kuendelea kujituma na kulinda viwango vyao.
Makame, mzaliwa wa Zanzibar, amewahi pia kuzichezea timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara, zikiwemo Namungo, Kagera Sugar na Geita Gold, huku Zanzibar akiwahi kucheza Mafunzo na Taifa Jang’ombe.