Makamu wa Pili mgeni rasmi Bonanza la Kijini Shangwe
Muktasari:
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika leo Jumamosi Septemba 12, 2026, katika Jimbo la Kijini, Wilaya ya Kaskazini A kisiwani Unguja, likiwaleta pamoja wananchi kwa lengo la kuimarisha umoja na maendeleo.
MWENYEKITI wa Taasisi ya Rise and Restore Foundation ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kijini, Badria Natai amezindua rasmi maandalizi ya tamasha la michezo na kijamii lijulikanalo kama Kijini Shangwe Bonanza 2026.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika leo Jumamosi Septemba 12, 2026, katika Jimbo la Kijini, Wilaya ya Kaskazini A kisiwani Unguja, likiwaleta pamoja wananchi kwa lengo la kuimarisha umoja na maendeleo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwenyekiti huyo alibainisha mgeni rasmi katika bonanza hilo anatarajiwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.
"Tamasha hili litakuwa na washiriki kati ya 3,500 hadi 5,000 kutoka ndani ya jimbo na maeneo jirani watakaohudhuria tukio hili la kihistoria," amesema.
Amesema tamasha hilo limebeba malengo ya kuwaunganisha wananchi, kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi kwa ajili ya kuimarisha afya zao na kutoa fursa kwa wajasiriamali wa jimbo hilo kuonyesha na kuuza bidhaa zao, pamoja na kuwapatia mitaji ya kujiendeleza.
Vilevile, mwenyekiti huyo amesema wananchi hao watapata fursa ya kujiunga na mfuko wa bima ya afya kwa kupatiwa kadi za matibabu hapohapo.
Alieleza, kilele cha bonanza hilo itapigwa mechi ya kirafiki kati ya Jimbo la Kijini dhidi ya Jimbo la Mahonda na litakuwa mwanzo wa utamaduni mpya wa viongozi wa jimbo hilo kuwa karibu na wananchi kwa kushirikiana katika shughuli za maendeleo na kijamii.