Prime
Manqoba Mngqithi aitisha ‘njaa ya ukatili’
KOCHA wa Yanga, Manqoba Mngqithi amewataka wachezaji wa kikosi hicho kuongeza njaa ya ukatili katika kutumia nafasi wanazotengeneza, baada ya timu hiyo kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Gaborone United katika mchezo wa kwanza wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Juzi Jumamosi, Yanga ilinusurika kipigo baada ya kusawazisha dakika ya 90+5 kupitia Seleman Mwalimu, kufuatia wenyeji wao kuongoza tangu dakika ya 31.
Licha ya sare hiyo, Manqoba amesema Yanga ilitawala sehemu kubwa ya mchezo, lakini ubora wa eneo la kuchezea pamoja na kushindwa kutumia nafasi walizotengeneza vilipunguza makali ya kikosi chake.
“Hatukucheza kwa ubora mkubwa ambao tunaufahamu. Inawezekana tulitawala mchezo, lakini kuna mambo yalitupunguzia ubora, hasa eneo la kuchezea halikuwa na ubora,” amesema Mngqithi.
Amesema jambo lingine ambalo linapaswa kufanyiwa kazi kabla ya mchezo wa marudiano ni uwezo wa wachezaji kuwa na kiu kubwa ya kumalizia nafasi.
“Nataka wakati wote tuwe na njaa ya ukatili wa kutumia nafasi tunazotengeneza. Hili nalo lilitupa shida, lakini nimependa namna ambavyo wachezaji wangu walionyesha ukomavu wa kuona hatustahili kuwa nyuma.
“Walishambulia kwa nguvu na kwa hesabu mpaka tukapata bao. Kuna mambo tunatakiwa kuyafanyia kazi kwenye mchezo wetu wa marudiano. Hii siyo timu ambayo tunatakiwa kuona kazi itakuwa rahisi, hivyo kuna umakini tutatakiwa kuuongeza.”
Kwa upande wake, Kocha wa Gaborone United, Sean Connor, amesema kikosi chake kilijisalimisha chenyewe baada ya kuamua kurudi nyuma na kuipa Yanga nafasi kubwa ya kutawala kipindi cha pili.
Connor amesema licha ya kupoteza ushindi waliokuwa wameushikilia hadi dakika za mwisho, bado anaamini Gaborone ina nafasi ya kuibuka na matokeo mazuri kwenye mchezo wa marudiano.
“Tulianza vizuri kipindi cha kwanza, hatukuwapa nafasi ya kucheza kwa ubora wao mpaka tulipopata bao la kuongoza. Kipindi cha pili tulifanya kosa kubwa la kuwapa nafasi ya kutawala mchezo zaidi,” amesema Connor.
“Walitushambulia kwa muda mrefu. Tulijaribu kuwazuia, lakini naona ilikuwa ngumu kwao. Tukubaliane wenzetu walikuwa timamu zaidi yetu, walishacheza mechi tano za ligi wakati sisi tumecheza mbili pekee.
“Tuna dakika 90 za marudiano tukiwa ugenini. Kuna sehemu Yanga wanafanya makosa, tutajipanga kuangalia namna ya kuyatumia kuweza kushinda tukiwa Tanzania.”
YANGA ILIVYOTAWALA
Yanga licha ya matokeo hayo, lakini ilicheza vizuri dakika 90 za mchezo huo, ikitawala sehemu kubwa licha ya kuruhusu bao dakika ya 31 kwa shambulizi la faulo.
Hata Yanga hatua ya kusawazisha bao hilo dakika ya 90+5, ilitokana na kuwashambulia zaidi Gaborone United ambao walijikuta wakijichanganya katika kuwadhibiti wageni na bao hilo likarudishwa.
CONNOR ALIWAKAMATA HAPA YANGA
Ukitazama vizuri mechi hiyo ya juzi, kocha wa Gaborone, Sean Connor utampongeza kwa namna alivyoweza kufanya vizuri kuisoma Yanga kwa kujua kwamba nguvu yao ya kutengeneza mashambulizi inatokea pembeni, aliwabana vizuri Albert Kangwanda na Houssein Zakouani ambao ndio walikuwa mpango wa kujengwa kwa mashambulizi.
Mpango huo ulifanikiwa kwa Kangwanda na Zakouani kuonekana hawana madhara lakini hata hivyo hatua ya mpinzani wake kumuingiza Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ilirudisha utulivu wa Yanga na kuja kuongeza nguvu ya kuwashambulia zaidi Gaborone, akihusika katika kujengwa kwa shambulizi lililotengeneza bao la kusawazisha kwa wageni.
MAXI, MUDA FRESHI
Unaweza kumsifia mfungaji wa bao la Yanga, lakini angalia kazi aliyofanya Maxi Nzengeli kwa pasi yake iliyopasua katikati ikimkuta Mudathir Yahya ambaye naye pasi yake ya kisigino kwenda nyuma yake, alijua Mwalimu anaitaka na mshambuliaji huyo kuwahadaa mabeki kwa kuchukua mpira kwa mguu wa kulia, walinzi kuja kushtuka akafunga na mguu wa kushoto.
UPEPO NA DIARA
Bao la Gaborone lilitokana na shambulizi la mpira wa adhabu ndogo nje kidogo ya eneo la hatari likifungwa na mshambuliaji Aubrey Amseb, lakini mabeki wa Yanga wamefichua wakati watu wakiona ni kama makosa ya kipa wa timu hiyo, Djigui Diarra lakini ukweli ni kwamba upepo ulimpa shida kudaka.
Kwa mujibu wa wachezaji hao, kulikuwa na hali ya upepo ambao uliufanya mpira kukatika na kupoteza uelekeo wake na Yanga ikajikuta ikiruhusu bao hilo ambalo liliwalazimisha kuanza hesabu za kusawazisha.
YANGA NAFASI BADO
Yanga licha ya kuwabana vizuri Gaborone United, lakini ilikuwa na shida katika kutumia nafasi ambazo walitengeneza uwanjani, wachezaji wake wakiongozwa na mshambuliaji Peter Shalulile hawakuwa na njaa kubwa ya kumalizia nafasi kama alivyobainisha Manqoba.
Wakati Yanga inarudi nyumbani inatakiwa kuongeza utulivu eneo hili ili mchezo huo wapate matokeo ambayo yatawavusha kwenda hatua ya inayofuata.
GABORONE HATARI HAPA
Kuna mashambulizi ambayo Gaborone waliyafanya kwenye mchezo huo hayakuingia wavuni hasa kwa mipira ya vichwa kwenye zile adhabu wakiwatumia mabeki wake warefu.
Yanga inatakiwa kujipanga na hili kwa kuhakikisha wanaruka vizuri ili kuwabana, mipira mingi ambayo mabeki wa Gaborone waliruka walipiga kwa utulivu, wakiangushwa na shabaha tu.
MANQOBA ‘SUB’ FRESH
Mabadiliko ambayo Yanga iliyafanya kwenye mechi asilimia kubwa yalikuwa na tija kubwa na kwa kiungo Stephanie Aziz KI ameongeza kasi ya kuishambulia Gaborone.
Ukiacha Aziz KI, hatua ya kuingia washambuliaji Cheikh Toure na Seleman Mwalimu iliwalizimisha Gaborone kurudi nyuma na kuwa na hesabu za kuzuia zaidi badala ya kushambulia, wakafanya makosa na Mwalimu kuwafunga.