Prime
Mnyama na Yanga, Lilongwe kulishangaza kuliko Gaborone
KILOMITA 1,800 kutoka Lilongwe hadi Gaborone. Wikiendi hii iliyoisha zilichezwa mechi mbili za kushangaza. Yanga walikuwa Gaborone wakati Simba walikuwa katika ardhi ya Kamuzu Banda pale Lilongwe. Mechi zao zilishangaza sana.
Mechi ya Gaborone ilikuwa imeshikwa na Yanga. Halafu wakaishia kutoka sare. Mechi ya Lilongwe ilikuwa imeshikwa na wenyeji, Mighty Wanderers halafu Simba wakashinda. Yanga walifungwa bao la kushangaza kidogo. Waliokuwemo uwanjani wanadai upepo mkali ulitingisha lile shuti ambalo Djigui Diarra alifungwa akiwa amesimama hapo hapo. Hata hivyo, mechi nzima ilikuwa imekamatwa na Yanga.
Walionyesha ukubwa wao katika Uwanja wa Taifa wa Gaborone. Ni kitu kilichonishangaza kidogo. Bingwa wa Tanzania amekuwa ana nguvu nyingi kuliko bingwa wa Botswana. Tofauti imeendelea kuwa kubwa.
Muda mwingi Waswana walikuwa wamekaa mbele ya kipa wao. Yanga walikuwa wakipiga msako mwingi katika dakika zote za mechi. Kipindi cha kwanza na hata baadaye katika kipindi cha pili walikuwa wameshindwa tu kumfikia Peter Shalulile.
Kipindi cha pili akaingia Aziz Ki kwa ajili ya kurahisisha mambo kule mbele, lakini bahati mbaya akapishana na Shalulile. Selemani Mwalimu akaingia na kwenda kuikomboa mechi katika dakika za jioni za mechi. Mwalimu alikuwa ameibwa na Yanga usiku pale Zanzibar na alifunga bao katika muda uleule ambao alikuwa ameibwa pale Unguja. Usiku sana. Lilikuwa bao muhimu la ugenini ambalo siku hizi CAF wamelifuta.
Kwa nilivyoona hata kama Yanga wangefungwa Gaborone bado wangekuwa na nafasi kubwa ya kupita katika pambano la Jumamosi ijayo pale Temeke. Mpira una maajabu yake, lakini Yanga ana mabao mengi pale Temeke kama akiwa makini.
Kwa kinachoonekana kwa sasa Aziz bado ni mchezaji muhimu katika kurahisisha mechi. Inabidi awepo pale kwa ajili ya kupiga pasi za mwisho. Kuna wachezaji wengi wapambanaji pale Yanga, lakini Aziz anafanya mambo rahisi zaidi.
Inayonishangaza ni mechi ya Simba. Kwanza kabisa nilidhani bingwa wa Botswana angekuwa bora zaidi kuliko bingwa wa Malawi. Kitu cha kushangaza Might Wanderers walionekana imara zaidi kuliko Gaborone United.
Najiuliza kama Gaborone United angecheza na Simba halafu Mighty Wanderers wangecheza na Yanga mechi zingekuwa kama zilivyokuwa? Ni kweli kwamba Simba walicheza na timu bora au walikuwa dhaifu? Ni kweli kwamba Yanga walikuwa bora au walicheza na timu dhaifu?
Vyovyote ilivyo ilikuwa mechi ngumu kwa Simba ingawa walishinda. Kuna wachezaji wengi wa Mighty Wanderers waliwavuruga Simba. Kuna rasta wao mmoja pale katikati alikuwa akinikumbusha Thaaban Scara Kamusoko. Yule staa wa zamani wa Yanga kutoka Zimbabwe.
Simba wana bahati zao katika michuano hii. Hata bao lenyewe walilofunga lilitokana na kosa dogo la wazi la beki mmoja wa Wanderers. Pamoja na kosa hilo bado ashukuriwe pia Aniceth Oura. Namna alivyotulia kabla ya kufunga. Wachezaji wangapi wanapoteza nafasi za wazi kama ile?
Lakini pia kwa namna ambavyo Mighty Wanderers walicheza vizuri, basi Simba walihitaji nafasi chache za kuua mechi. Ile ilikuwa nafasi ya dhahabu iliyoanguka katika miguu ya Oura. Angekosa tusingemsamehe. Pamoja na ubora wa wenyeji Simba walimkosa mchezaji anayeitwa Libasse Gueye. Ndiye kinara wa mashambulizi ya Simba. Alipata kadi nyekundu msimu uliopita katika mashindano haya haya.
Katika mechi muhimu ugenini ambayo Mourice Abraham anaanza halafu Clatous Chota Chama anaanzia benchi, ni wazi kwamba zama za Chama zimeanza kuelekea mwisho Msimbazi. Kocha Steve Barker sio kwamba hamuamini Chama, hapana, naona anaanza kuhisi ana mechi zake.
Mchezaji bora huwa anacheza mechi zote. Kubwa na ndogo. Zenye kasi na zisizo na kasi. Lakini kila siku umuhimu wa Chama unapungua Msimbazi. Mechi nyingi amekuwa akitolewa na mashabiki hawalalamiki. Hii hakuanza lakini mashabiki hawakulalamika.
Uzuri ni kwamba Simba yenyewe ina timu nzuri. Hawana hofu sana na kukosekana kwa Chama uwanjani. Hawana hofu sana kwa sababu kina Libasse wapo na wanaweza kuamua mechi kama alivyofanya Oura. Vipi marudiano pale Uwanja wa Uhuru? Kama mechi zikichezwa katika viwango vilevile, basi Simba watakuwa na kazi ngumu uwanjani. Inabidi wapandishe kiwango chao kwa haraka zaidi.
Watakuwa nyumbani na mara nyingi Simba wamekuwa wakijua namna ya kutumia vizuri uwanja wa nyumbani.
Sitegemei Simba itupwe nje baada ya kuongoza bao moja kule Lilongwe. Ushindi wowote utaipitisha Simba. Sare yoyote itaipitisha Simba. Lakini wanahitaji kupambana zaidi kuliko mechi iliyopita. Na kama Libasse atakuwepo ina maana kasi ya mashambulizi Simba itaongezeka zaidi.
Kwa ujumla wa timu zote. Sidhani kama shabiki yeyote aliyepo Misri, Algeria au Morocco anatazamia timu ya Tanzania kati ya Simba na Yanga iondolewe katika hatua za awali kabisa za michuano hii.
Bajeti tulizonazo na viwango ambavyo tumejiwekea inaonyesha kwamba hizi timu za Malawi, Zambia, Ethiopia, Kenya, Rwanda na nyingi nyinginezo za ukanda huu zinapaswa kupisha utawala wa hizi timu mbili za Tanzania, Simba na Yanga, bila ya kumsahau kijana wao Azam.
Kutolewa mapema ni aibu. Tumesajili wachezaji wa bei mbaya. Tumeleta makocha kutoka Afrika Kusini. Tunalipa mishahara mikubwa. Ni aibu kutolewa na timu kutoka kanda hizi zinazotuzunguka. Kama tunaifikiria nusu fainali nadhani Simba watatazama kiwango chao katika pambano dhidi ya Wanderers na kugundua kwamba hakikubaliki.