MAISHA yana kupanda na kushuka. Ukitaka kuamini msemo huo ni halisi, jifunze anachopitia staa wa zamani wa Yanga, Said Bahanuzi, kutoka kumiliki mamilioni ya pesa na sasa kuisaka Sh10,000 kwa jasho.
Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, Bahanuzi ambaye ana asili ya Rwanda, anasimulia maisha yalivyojifunua katika ukurasa mwingine uliobeba uvumilivu, unyenyekevu na imani ya vitu kuja na kuondoka.
“Laiti ingetokea nafasi nyingine au siku zingerudi nyuma za kucheza soka, ningekuwa habari nyingine, ningefanya vitu vya msingi vya kuandaa maisha baada ya soka. Natamani wachezaji wajifunze kutokana na sisi wengine, ingawa tofauti na wajuavyo wengi kutuhusu, hawajui uhalisia wetu,” anasema.
Anasema safari ya kuporomoka kiuchumi ilianza baada ya kupata jeraha la mguu wa kulia na walisema mfupa umekaa pembeni na mguu huo ulianza kujaa maji akiwa na Mtibwa Sugar 2016/17.
Alitumia pesa nyingi kujiuguza pamoja na kutunza familia na watu waliokuwa wanamtegemea, bila kufanya shughuli zingine za kuingiza kipato.
“Kidogo kidogo nikaanza kutumia nguvu hata kupata Sh50,000. Hata ukiomba kwa marafiki inakuwa ngumu kukupa, kwani wanakuwa wanajua haupo kwenye mkondo wa pesa,” anasema Bahanuzi.
“Baadaye ikawa ngumu hata kupata Sh10,000. Kutokana na kuachana na aliyekuwa mke wangu, ilinibidi nimwachie nyumba ambayo niliijenga jijini Dar es Salaam, ili aendelee kulea watoto wangu.”
Anasema baada ya kupigwa na maisha alikwenda kuishi Mwanza. Alianza kwa kulipia chumba cha kuishi chenye choo nje cha gharama ya Sh15,000 katika Kijiji cha Magu. Kutokana na ugumu wa uchumi, wakati mwingine alitumia Sh1,000 kwa ajili ya mlo wa siku.
“Nilikuwa nafanya kazi ya kuuza chakula kwenye hoteli moja hivi, haikuwa kubwa, kwa siku nilikuwa nalipwa Sh4,000, hivyo nilikuwa natumia Sh1,000 kwa matumizi ya mlo wa siku. Wakati mwingine nilikuwa nakunywa eneji tu ili nipate nguvu ya kuendelea kupambana,” anasema mchezaji huyo wa zamani na kuongeza:
“Nilifanya kazi hiyo kuanzia mwaka 2023 hadi 2024, baada ya hapo 2024 hadi 2025 niliuza dagaa. Nilikuwa nazitoa Mwanza kwenda jijini Dar es Salaam, nikapata changamoto ya biashara hiyo nikaachana nayo. Ilinibidi niombe kazi Silent Ocean ya kupandisha na kushusha mizigo kwenye kontena na kwa siku nilikuwa nalipwa Sh10,000, ingawa chakula cha mchana tulikuwa tunapewa bure.”
Anasema alipata changamoto ya kumuuguza mtoto wake, hivyo aliachana na kazi hiyo, lakini alikuwa akipata fursa ya kusaidia mafundi ujenzi wa nyumbani. Alikuwa anakwenda kupambana ili kupata pesa ya kutunza familia.
“Ndiyo maana wanaume wengi wanakufa mapema, wana vitu vingi walivyovibeba kwenye mioyo yao. Mfano, kipindi ambacho Sh1,000 ndiyo ilikuwa inatumika kupata mlo wa siku, ukapigiwa simu ya mahitaji ya watoto, ukatuma ulichonacho bila wao kujua unapita nini, halafu unayemtumia anaona ni pesa kidogo, lazima utaumia,” anasema.
“Mwanamume ni mtu ambaye anatakiwa kutatua maisha ya familia. Huwezi kupiga simu na kuanza kulialia, vinginevyo ndiyo hizo kauli za mwanamuziki Dudubaya anazosema linda mgongo wako, bila kukaza buti wengine wanajiua au wamechanganyikiwa. Kilichonisaidia ni malezi ya msingi ya wazazi wangu. Baba alioa wanawake wanne, mama yangu alikuwa wa mwisho, hivyo tulifunzwa kupambana, kukosa na kupata.”
Anasema ingawa anafanya kazi katika kiwanda kinachojishughulisha na kazi ya kuchakata plastiki na kwa siku anaingiza Sh12,000, wanapewa baada ya wiki mbili.
“Wakati naanza kazi hiyo wengi hawakunijua, lakini kuna jamaa mmoja aliniona akaniuliza, wewe si Bahanuzi? Nikamjibu ndiyo. Akasema umefuata nini hapa? Nikamwambia nafanya kazi hapa, ndipo wengi wakaanza kusema ni wewe, imekuaje staa mkubwa unafanya kazi ya kuchafuka na machupa na ngumu hivi,” anasema Bahanuzi.
“Wapo wengine wanasema ulipata pesa na fursa uliendekeza wanawake, tunasikia kipindi hicho ulikuwa unatoka na wadada maarufu. Nanyamaza kwani siwezi kumjibu kila mtu, hawajui maisha yangu nyuma ya pazia. Najua umaarufu usipokuwa na pesa sawa na mtu mwenye kipara kujitwisha gunia la misumari kichwani.”
Anasema kwa sasa amepanga chumba cha Sh25,000, umeme kwa mwezi Sh6,000 Mlandizi, huku pesa anayoipata anajibana aweze kuwasaidia watoto wake na kumuuguza mama yake mzazi anayeumwa.
“Nafanya kazi kiwandani usiku, mchana nikipata kazi ya saidia fundi naenda nafanya. Watu wengi wananiuliza umewezaje kukubaliana na hali na kuanza moja? Mimi ni mwanamume, najua Mungu anaweza akakupa vitu na akaviondoa akapewa mwingine, najua anaweza akanishusha na kunipandisha,” anasema na kuongeza;
“Wachezaji wa sasa ambao wanapata pesa ndefu kuliko sisi, basi waandae maisha yao baada ya kazi, umaarufu wanaoupata kama watafuja pesa, wajue unawasubiri kuwatesa. Sisi wengine huku hata ukipanda daladala watu wanaanza kusema wachezaji kwa umalaya, kwa sasa nimezoea nachukulia kawaida nanyamaza tu.”
Anasema pesa ndefu ya mpira wa miguu ni dau la usajili alilolipata wakati anajiunga na Yanga msimu wa 2012-2014 na alipewa Sh12 milioni na mshahara ulikuwa Sh600,000, na baada ya kumalizika kwa mkataba huo na kuongeza mwingine 2014 hadi 2016, aliahidiwa kupewa Sh30 milioni na mshahara Sh1 milioni.
“Walinitangulizia Sh3 milioni kati ya Sh30 milioni, baadaye wakanivunjia mkataba, hivyo sikupata chochote. Licha ya kuwa na umaarufu unaweza ukaona sikuwa na pesa ambazo jamii ilikuwa inanitazama nazo,” anasema.
Anasimulia jinsi ambavyo dili la kutakiwa na TP Mazembe lilivyoyeyuka, kutokana na Yanga kuhitaji pesa ndefu, zilizokuwa haziendani na uhalisia wa uzoefu na jina lake.
“Wakati nipo Yanga, uongozi wa TP Mazembe ulinifuata, lakini walihitaji milioni 600. Kiukweli ilinishtua sana kwani wao walinisajili kwa milioni 12, nikitokea Mtibwa Sugar. Ni kweli nilikuwa na kipaji, lakini sikucheza kwa muda mrefu wa kuhitaji kiasi kile,” anasema na anaongeza:
“Yanga kipindi hicho walikuwa wagumu kuwaachia mastaa wao kwenda kujaribu maisha nje, badala yake walikuwa wanainua vikwazo, kama vilivyonipata. Zilikuja timu nyingi kutoka Misri na China, lakini ziligonga mwamba.”
Anakiri kwamba Ligi Kuu Bara ina ushindani wa hali ya juu, unaovutia wageni kuja kucheza kwa wingi hapa nchini.
“Ingawa kipindi nacheza kulikuwepo mapro wenye viwango vya juu kama Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite, Didier Kavumbagu, kwa Simba alikuwepo Emmanuel Okwi, marehemu Patrick Mutesa Mafisango. Kwa sasa, ukiacha waliondoka, waliyopo ni Aziz Ki, Peter Shalulile, Djigui Diarra, Maxi Nzengeli, Clatous Chama, Libasse Gueye, Anicet Oura, Rushine De Reuck na wengine wengi ambao wanafanya vizuri,” anasema mkongwe huyo.
Anawapa pongezi kwa kuwa na muendelezo wa viwango vyao ambao amecheza nao ni Simon Msuva, Mbwana Samatta, Jonas Mkude, Himid Mao, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliyekuwa amekuja nyuma yao.
“Ukiachana na hao, lakini bado kuna wazawa ambao sasa hivi wanafanya vizuri kama Feisal Salum ‘Fei Toto’, Ibrahi Bacca, kabla ya Clement Mzize kuumia alikuwa kwenye kiwango bora, Idd Nado, Bakari Mwamnyeto ingawa anasemwa sana, lakini bado hajayumba uwanjani, Dickson Kibabage, Dickson Job, Zuberi Foba na wengine wengi,” anasema.