Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pemba na kitendawili cha soka, mabingwa washuka kurejea Ligi Kuu kizungumkuti

Muktasari:

  • Super Falcon ni miongoni mwa timu zilizowahi kuandika historia kwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu wa 2011-2012, lakini msimu uliofuata ikashuka daraja na hadi sasa haijarejea Ligi Kuu, huku Jamhuri ilibeba ubingwa mwaka 2003.

KUTWAA ubingwa halafu msimu unaofuata kushuka daraja, kisha kushindwa kurejea tena Ligi Kuu, ndiyo hali inayozikabili baadhi ya timu zinazotokea kisiwani Pemba katika Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).

Super Falcon ni miongoni mwa timu zilizowahi kuandika historia kwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu wa 2011-2012, lakini msimu uliofuata ikashuka daraja na hadi sasa haijarejea Ligi Kuu, huku Jamhuri ilibeba ubingwa mwaka 2003.

Hali hiyo imekuwa ikijirudia kwa timu za Pemba na baada ya kushuka daraja zimekuwa zikishindwa kurejea Ligi Kuu, zikiishia Ligi Daraja la Kwanza, huku Super Falcon ikicheza Ligi Daraja la Pili Pemba.

Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza na wadau wa soka pamoja na baadhi ya viongozi wa timu, wakielezea sababu zinazochangia hali hiyo. Wengi kati yao wametaja sababu kuu mbili ambazo ni kutokuwa na vyanzo vya mapato, kutegemea fedha za mdhamini mkuu pekee, pamoja na matumizi mabaya ya fedha hizo.

Hata hivyo, wadau hao wametoa suluhisho la nini kifanyike ili kuleta mabadiliko ya soka kisiwani Pemba, wakitaja nondo tano.

VIONGOZI WAKWELI

Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Super Falcon, Mohamed Said ‘Shuberi’, anasema timu nyingi za kisiwani humo zinafeli kutokana na kutotambua mahitaji ya mpira.

Akitolea mfano wa timu ya Mwenge, Shuberi anasema kama viongozi wangekuwa wakweli na kumpa mwalimu anachokihitaji, hakuna sababu ya timu hiyo kufanya vibaya.

Pia, kocha huyo anasema kilichoifanya Super Falcon kuwa bora na imara ni ukweli wa uongozi uliokuwepo na kumpa kocha kinachohitajika bila kuchelewa.

“Mpira hautaki ubabaishaji wala hauna mbadala. Ili uwe na timu bora, lazima uondoshe makandokando kwa kiongozi kuwa mfuatiliaji na sio kuagiza kila kitu,” anasema Shuberi.

Kocha huyo amewasihi viongozi wa timu waache kuzitengeneza kama starehe, ila wanapaswa kuzijenga kuwa kama kazi ili wachezaji wapate mahitaji yao.

Shuberi amesema viongozi wa timu hizo wanapaswa kukubaliana na hali ilivyo, kwani mpira wa kisasa unahitaji gharama, ikiwemo jezi, mipira, viatu na usajili wenye viwango utakaotoa ushindani ndani ya ligi.


UMOJA NA MSHIKAMANO

Mtakwimu Mkuu wa Chipukizi United, Suleiman Rajab Othman Rajab, anasema timu zinazoshiriki Ligi Kuu Zanzibar zilipaswa kuwa na umoja wao wa kupanga mikakati ya namna ya kuleta ushindani kwenye ligi na kudumu kwa muda mrefu.

Anaeleza kuwa umoja huo ungetoa mwelekeo wa kuandaa mipango ambayo ingezifanya timu zisishuke hata moja kwa msimu, kwa lengo la kuongeza idadi tofauti na ilivyo kwa sasa.

Katika ligi hiyo yenye jumla ya timu 16 zinazoshiriki, kati ya hizo nne pekee zinatokea kisiwani Pemba, ndizo zinazoiwakilisha kisiwa hicho.

Mtakwimu huyo anasema anatamani Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) liboreshe mambo mawili, ikiwemo udhamini na waamuzi wa michezo, akidai baadhi yao hawachezeshi kulingana na maadili ya kazi yao.

“Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar linapaswa kukaa chini na waamuzi kuchezesha kwa haki bila kuangalia timu wala mmiliki, kwani wasipofanya hivyo hatutafika tunapohitaji,” anasema.

Suleiman anasisitiza kuacha ubaguzi baina ya Pemba na Unguja, kwani mpira hautakiwi kutiwa siasa zenye lengo la kulichafua soka la visiwa hivyo.


WADHAMINI KUACHA UBABISHAJI

Anasema timu nyingi za Pemba bado zinasuasua kwenye udhamini kwa sababu wengi wao sio wa kweli, akifichua unaweza kumtangaza mdhamini hadi kufikia mechi tano wakati hajatoa hata Sh100.

Anaeleza kuwa suala la kumtangaza mtu kwenye mpira ni kubwa sana, lakini wadhamini hawalipi uzito kulingana na fedha wanayoitoa.

Akitolea mfano, msimu uliopita kuna timu (jina kapuni) iliwahi kumtangaza mdhamini (jina kapuni) katika mechi 15 za mzunguko wa kwanza bila kupatiwa fedha, baadaye akajiondoa.


MDAMINI MKUU KUONGEZA DAU

Kwa sasa, mdhamini mkuu wa ligi hiyo ni Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), inayotoa Sh30 milioni kwa kila timu kwa ajili ya maandalizi na fedha hizo zinatolewa kwa awamu.

Msemaji wa New Stone Town, iliyodumu ZPL kwa msimu mmoja pekee, Said Ayoub Kijaji, anasema timu zinazotokea kisiwani Pemba zinashindwa kustahimili kwenye ligi hiyo kwa sababu ya kutokuwa na rasilimali fedha.

Anabainisha timu zinazotokea Pemba zinategemea fedha za mdhamini mkuu pekee kutokana na kukosa vyanzo vingine vya mapato.

Msemaji huyo anasema kwa sababu ya ukata wa fedha, baadhi ya wachezaji wanaamua kutimkia timu zilizo vizuri kiuchumi bila kujali kupata kwao nafasi ya kucheza.

Anasema hayo yote yanatokea kwa timu za Pemba kutokuwa na uwezo wa kuwahudumia wachezaji walioamua kuufanya mchezo wa mpira wa miguu kuwa ajira yao.


NIDHAMU YA FEDHA

Akizungumza na Mwanaspoti, mdau wa soka visiwani hapa, Idrissa Yakout, amesema baadhi ya viongozi wa timu za mpira Pemba hawana uelewa wa mpira wa miguu, ndiyo sababu ya timu hizo kushuka.

Anasema baadhi ya viongozi wa timu hizo wanatumia fedha wanazopewa na mdhamini mkuu wa ligi kwa mahitaji yao binafsi, ikiwemo kufanya mitaji ya biashara, kutumia kwa ajili ya sherehe za harusi na kutatua changamoto zao binafsi na siyo za timu.

Pia, anaeleza viongozi hao hawana mipango ya fedha wanazopata kutoka kwa mdhamini wa ligi hiyo, ndiyo maana timu zinashindwa kujiendesha inavyotakiwa. Msimu uliopita 2025-2026, baadhi ya wachezaji wa Junguni waliosajiliwa dirisha dogo waliondoka kabla ya msimu kumalizika kwa madai ya hali ngumu iliyosababishwa na hali ya kiuchumi.

Mtunza Fedha wa Junguni United, Hamis Kombo Mussa, aliliambia Mwanaspoti kuna baadhi ya viongozi ndani ya klabu hiyo sio waaminifu, ndiyo waliosababisha hali kuwa hivyo.

Anasema fedha zilizopaswa kutumika kwa ajili ya uendeshaji wa timu zilitumika kwa masilahi binafsi ya viongozi, jambo lililochangia kushuka daraja msimu huo. Msimu uliopita 2025-2026, timu mbili kutoka kisiwani Pemba zilishuka daraja, ambazo ni Junguni United na New Stone Town, huku nyingine zilizowahi kufanya hivyo zikishindwa kurejea Ligi Kuu, huku baadhi zikipotea kabisa.

Msimu huu wa 2026-2027 kuna timu nne za Pemba ambazo ni Fufuni, Mwenge, Chipukizi United na Wembe, huku zikionekana kutoanza vizuri katika mechi sita za kwanza, kwani zinashika nafasi tatu za chini.

Fufuni ipo mkiani na pointi mbili, haijashinda mechi yoyote ikiwa imeshuka dimbani mara sita, imeambulia sare mbili na kupoteza nne, huku ikifunga mabao matatu na kuruhusu kumi.

Chipukizi inafuatia kwa kushika nafasi ya 15 baada ya kucheza mechi sita, imeshinda moja, imetoka sare moja na kupoteza nne. Imefunga mabao matatu na kuruhusu tisa. Ina pointi nne. Mwenge ni ya 14 katika msimamo baada ya kucheza mechi sita. Matokeo yake ni kama Chipukizi, lakini zimetofautiana kwa mabao, kwani Mwenge imeruhusu manane, ikifunga matatu. Nayo ina pointi nne.

Wembe yenye pointi tano katika mechi sita ikiwa nafasi ya 11, imeshinda moja, sare mbili na kupoteza tatu. Imefunga mabao matatu na kuruhusu saba.