Nyuma ya jeuri ya Olivier Giroud kuna Jennifer
Muktasari:
- Giroud, staa wa zamani wa Arsenal, Chelsea na AC Milan, amekuwa kwenye ndoa na Jennifer kwa zaidi ya miaka 15 na hadi sasa wamejaliwa kupata watoto wanne.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Olivier Giroud hivi karibuni wakati akimtakia mkewe Jennifer heri ya kuzaliwa, alimtaja kama mama bora zaidi duniani akionyesha kuthamini mchango wake mkubwa katika familia yao.
Giroud, staa wa zamani wa Arsenal, Chelsea na AC Milan, amekuwa kwenye ndoa na Jennifer kwa zaidi ya miaka 15 na hadi sasa wamejaliwa kupata watoto wanne.
"Heri ya siku ya kuzaliwa kwa Mama bora kuliko wote. Mimi, Jade, Evan, Aaron na Aria tunakupenda kwa moyo wetu wote," aliandika Giroud katika ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 3.4.
Ingawa mashabiki wengi wanayafahamu mafanikio ya Giroud uwanjani, lakini baadhi yao wamekuwa na shauku ya kutaka kujua upande wa pili wa maisha yake hasa uhusiano wake na Jennifer.
Tofauti na mastaa wengi wa soka, Giroud alichelewa kujiunga na mitandao ya kijamii, mathalani Instagram amejiunga Desemba 2021, hivyo kuna vitu vingi kutoka katika familia yake havijulikani ila kwa leo kuna hivi vichache kumuhusu.
Inaripotiwa Giroud na Jennifer walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 2005 wakiwa bado wanafunzi mjini Grenoble nchini Ufaransa, rafiki yao wa karibu ndiye aliyewakutanisha, hatua ambayo imekuja kubadili historia ya maisha yao.
Kwa miaka mingi, Jennifer amekuwa akimfuata mume wake huyo katika miji mbalimbali kuanzia Ulaya hadi Amerika Kaskazini na alienda kucheza soka. Amekuwa naye kuanzia Paris, London, Milan hadi Los Angeles, Marekani.
Lakini mrembo huyu ni nani hasa? Jennifer alisomea masuala ya urembo wa ngozi lakini alilazimika kutoifanyia kazi taaluma yake ili kumsaidia mume wake ambaye alijiunga na Arsenal mwaka 2012 baada ya kufanya vizuri huko kwao Ufaransa.
Akizungumza katika kipindi cha Zone Interdite, Jennifer alisema angeweza kufanyia kazi kile alichosomea lakini kwa mapenzi yake aliamua kumsaidia mume wake, pamoja na kuwalea watoto wao, ingawa hakuwahi kutarajiwa kuishi maisha ya namna hiyo.
“Kamwe sikutarajia kuwa na maisha tuliyonayo kwa sasa, mimi na Giroud tulikutana kwa mara ya kwanza miaka 16 iliyopita, wakati huo bado alikuwa si mchezaji wa kulipwa, sote tulikuwa wanafunzi tu.
"Kwa hiyo nilifikiria kuwa tungekuja kuishi maisha ya kawaida tu - tutapata watoto na kila mmoja ataenda kazini kwake. Nilifikiri tutaishi maisha ya kawaida tukiwa tumezungukwa na familia na marafiki zetu wa huko Grenoble, lakini sivyo ilivyo kwa sasa," alisema Jennifer.
Wawili hao ambao walifunga ndoa mwaka 2011, tayari wamejaliwa kupata watoto wanne ambao ni Jade aliyezaliwa mwaka 2013, Evan aliyezaliwa 2016, Aaron aliyezaliwa 2018 na Aria aliyezaliwa 2020.
Watoto wao wote wamepishana kati ya miaka miwili hadi mitatu ya kuzaliwa na mara kadhaa Giroud huwaposti mtandaoni.
Kama ambavyo mahusiano ya watu wengine hukumbwa na changamoto, ndivyo na kwa wawili hao, mathalani mwaka 2014, ndoa yao ulikumbwa na misukosuko baada ya mchezaji huyo kudaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamitindo Celia Kay.
Hata hivyo, Giroud aliomba msamaha hadharani kwa mke wake pamoja na mashabiki, lakini vilevile alikanusha vikali tuhuma hizo za kuwa na mchepuko. Tangu wakati huo, wawili hao wameendelea kuwa pamoja wakiendeleza maisha yao ya ndoa pamoja na familia yao kwa ujumla.
Ikumbukwe tofauti na wachezaji wengi wa Ufaransa kama Kylian Mbappe, mafanikio ya Giroud katika ulimwengu wa soka yalianza kuonekana akiwa na umri mkubwa kidogo.
Akiwa na umri wa miaka 24, ndipo Giroud alipoanza kuonekana katika timu ya taifa ikiwa ni baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) 2011/12 akiwa na klabu ya Montpellier ambayo kwa sasa imeshuka daraja.
Katika msimu huo, Giroud alifunga mabao 21 kwenye ligi na kutwaa kiatu ch Mfungaji Bora. Mafanikio hayo yalikuja takribani mwaka mmoja baada ya kufunga ndoa na Jennifer, na ndio ilikuwa sababu ya kusajiliwa na Arsenal.
Jennifer anahusishwa kuhusika moja kwa moja katika dili za uhamisho wa mchezaji huyo, inadaiwa kuwa yeye ndiye alikuwa sababu ya kukwama kwa dili la Giroud kujiunga na Everton akitokea Arsenal.
Pia Jennifer ndiye aliyeupiga chini mpango wa kubadilishana wachezaji katika uhamisho wa Pierre-Emerick Aubameyang kutoka Borussia Dortmund kwenda Arsenal mnamo Januari 2018 na Giroud alikuwa sehemu ya mpango huo, na hatimaye Giroud alikuja kutua darajani kuitumikia Chelsea alipocheza kwa misimu mitatu.