Mtihani wa Simba kwa Singida Black Stars
Muktasari:
- Mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, utapigwa kwenye Uwanja wa Airtel mkoani Singida kuanzia saa 12:00 jioni, huku Simba ikilenga ushindi utakaoiwezesha kufikisha pointi tisa na kupanda kileleni mwa msimamo.
SIMBA inakutana na mtihani mwingine wa mapema katika Ligi Kuu Bara itakapovaana na Singida Black Stars leo Jumamosi, huku takwimu za misimu minne iliyopita zikiipa timu hiyo ya Msimbazi kiburi cha kutamba mbele ya wapinzani wao.
Mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, utapigwa kwenye Uwanja wa Airtel mkoani Singida kuanzia saa 12:00 jioni, huku Simba ikilenga ushindi utakaoiwezesha kufikisha pointi tisa na kupanda kileleni mwa msimamo.
Simba kwa sasa imekusanya pointi sita, sawa na Yanga, lakini ushindi leo utaiwezesha kufikisha pointi tisa na kuipita Yanga, ambayo itashuka nafasi kutoka kileleni ikisubiri kucheza Agosti 24, 2026.
Kabla ya mchezo huo, Simba imeanza msimu kwa ushindi katika mechi mbili, Agosti 16, 2026 iliifunga Kagera Sugar mabao 2-0, kabla ya kuichapa Pamba Jiji mabao 2-1, Agosti 19, 2026. Zote ikicheza ugenini kama itakavyokuwa leo.
Singida Black Stars nayo imeanza msimu kwa ushindi na sare, ikiifunga Fountain Gate mabao 3-0 ilipocheza nyumbani, kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar ugenini, hivyo imekusanya pointi nne.
BARKER ATOA TAHADHARI
Kocha wa Simba, Steve Barker, ametambua ugumu wa mchezo huo akisema wanahitaji kutumia nafasi hiyo kupata pointi tatu na kuendelea kujenga msingi mzuri wa malengo yao ya msimu.
“Haitakuwa mechi rahisi, lakini tunahitaji kupata matokeo ya ushindi yatakayotupa pointi tatu,” amesema Barker.
Nahodha msaidizi wa Simba, Rushine De Reuck, ambaye msimu uliopita alifunga mabao manne, amesema ushindi walioupata katika mechi mbili za mwanzo unapaswa kuwapa nguvu ya kuendelea kupambana kwa ajili ya malengo ya msimu.
“Tunahitaji kuamini ushindi tulioanza nao ili kuhakikisha tunajiimarisha kupambania malengo ya msimu huu,” amesema.
SIMBA YATAWALA TAKWIMU
Katika mechi nane zilizopita kati ya timu hizo misimu minne, Simba imekuwa na rekodi nzuri zaidi, ikishinda mara saba na kutoka sare moja.
Singida Black Stars haijapata ushindi katika mechi hizo, ingawa rekodi hiyo haiwezi kuifanya Simba kuwa na uhakika wa ushindi kutokana na ushindani unaoonekana kila zinapokutana.
Msimu uliopita wa 2025-2026, Simba iliifunga Singida Black Stars mara mbili, ikishinda 2-1 ugenini, Machi 11, 2026, kabla ya kupata ushindi wa 2-0 nyumbani.
Msimu wa 2024-2025, Simba ilishinda 1-0 ugenini, Desemba 28, 2024 na 1-0 nyumbani ambapo ilikuwa Mei 28, 2025.
Msimu wa 2023-24, Simba ilishinda 2-1 ugenini ambapo mechi ilichezwa Oktoba 8, 2023 na 3-1 nyumbani, Machi 12, 2023.
Katika msimu wa 2022-2023, Singida Black Stars iliizuia Simba kwa sare ya bao 1-1, Novemba 9, 2022, lakini Simba ikashinda 3-1 katika mchezo wa pili.
GEITA, KAGERA KUMALIZANA
Katika mchezo mwingine wa ligi utakaochezwa leo saa 2:30 usiku, Geita Gold itaingia uwanjani kuvaana na Kagera Sugar, hili ni pambano la timu zilizorejea Ligi Kuu baada ya kushuka daraja msimu wa 2024-2025.
Geita Gold imeanza msimu kwa ushindi na kipigo, ikiifunga Mbeya City bao 1-0 kabla ya kupoteza kwa bao kama hilo dhidi ya Namungo. Kocha wa timu hiyo, Zuber Katwila, amesema ushindi ni muhimu kutokana na ugumu wa msimu, akitahadharisha kuwa hakuna mchezo mwepesi.
“Ushindi kwetu ni muhimu, msimu ni mgumu hivyo hakuna mechi nyepesi,” amesema Katwila.
Kwa upande wake, kocha wa Kagera Sugar, Juma Kaseja, amesema wamejiandaa kupambana kwa ajili ya pointi tatu, huku akitambua ubora wa Geita Gold.
“Itakuwa mechi ngumu, lakini tumeajipanga kuhakikisha tunapambania pointi tatu. Natambua Geita Gold ni timu yenye ushindani mkubwa, utakaofanya mechi iwe yenye mvuto zaidi,” amesema Kaseja.
Kagera ambayo leo itakuwa ugenini, mechi zake mbili za kwanza imeanza kwa kipigo, kisha sare zote ikiwa nyumbani ikifungwa 2-0 na Simba, kisha sare ya 1-1 dhidi ya Singida Black Stars.
REKODI ZA GEITA NA KAGERA
Katika mikutano yao ya misimu ya hivi karibuni, timu hizo zimekuwa na matokeo yenye ushindani.
Msimu wa 2021-2022, Kagera Sugar ilipoteza 1-2 nyumbani dhidi ya Geita Gold, Novemba 20, 2021, kabla ya Geita Gold kushinda 1-0 katika mchezo wa pili Mei 7, 2022.
Msimu wa 2022-2023, timu hizo zilitoka sare ya 1-1 Septemba 6, 2022, huku mchezo wa pili ukimalizika kwa sare ya mabao 2-2, Desemba 25, 2022. Msimu wa 2023-2024, Kagera Sugar ilishinda 1-0, Septemba 17, 2023, kabla ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa pili Februari 28, 2024.
Msimu wa 2024-2025, timu hizo hazikukutana katika Ligi Kuu baada ya ratiba ya msimu huo, huku zote zikishuka daraja.