Polisi Tanzania yazizidi kete Simba, Yanga
Muktasari:
- Baada ya raundi tatu za mwanzo, Polisi Tanzania ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache zaidi, ikiwa imefungwa bao moja pekee katika dakika 270 ilizocheza. Bao hilo ililifungwa na Abdul Suleiman ‘Sopu’ kwa mkwaju wa penalti katika mchezo wa kwanza dhidi ya Azam FC uliomalizika kwa sare ya 1-1.
KOCHA wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata, amefichua kuwa nidhamu ya safu yake ya ulinzi ni miongoni mwa sababu zilizoiwezesha timu hiyo kufanya vizuri katika michezo mitatu ya mwanzo ya Ligi Kuu Bara, huku takwimu zikionyesha imekuwa na ukuta imara kuliko Simba na Yanga.
Baada ya raundi tatu za mwanzo, Polisi Tanzania ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache zaidi, ikiwa imefungwa bao moja pekee katika dakika 270 ilizocheza. Bao hilo ililifungwa na Abdul Suleiman ‘Sopu’ kwa mkwaju wa penalti katika mchezo wa kwanza dhidi ya Azam FC uliomalizika kwa sare ya 1-1.
Takwimu hizo zinaiweka Polisi mbele ya Simba na Yanga katika eneo la ulinzi, licha ya timu hizo mbili kuongoza msimamo wa ligi zikiwa na pointi tisa kila moja. Yanga, ambayo iko kileleni, imeruhusu mabao mawili, sawa na Simba, wakati Polisi Tanzania ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba.
Mwanzo huo umeifanya Polisi Tanzania kuingia kwenye kundi la timu zinazotoa ishara mapema kwamba zinaweza kuwa na ushindani mkubwa msimu huu, hasa kutokana na uwezo wake wa kuzuia wapinzani kupata mabao.
Polisi ilianza msimu kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC, kabla ya kupata ushindi wake wa kwanza kwa kuichapa JKT Tanzania mabao 2-0. Katika mchezo wa tatu, ilipata ushindi mwingine kwa kuifunga Dodoma Jiji bao 1-0 ugenini.
Katika michezo hiyo mitatu, ukuta wa Polisi unaoongozwa na kipa Christopher Nyakanda pamoja na mabeki Denis Mushi, Tangu Kashinje, Joseph Majagi na Oscar Masai, umeonyesha maelewano mazuri na nidhamu katika kutekeleza majukumu yao.
Makata alisema siri kubwa ya uimara huo ni wachezaji wake kufuata maelekezo ya benchi la ufundi na kila mmoja kutambua wajibu wake anapokuwa uwanjani, hasa wakati timu inapokuwa kwenye presha ya mashambulizi.
“Jambo kubwa ambalo nimeliona kwenye timu yangu ni nidhamu. Wachezaji wamekuwa wakifuata maelekezo na kila mmoja amekuwa akijua wajibu wake uwanjani. Hii imetusaidia sana kuwa imara tunapokuwa kwenye kipindi cha kulinda lango letu,” alisema Makata.
Kocha huyo aliwapongeza mabeki wake kwa namna walivyopambana katika kila mchezo, akisema hata pale wapinzani wanapoweka presha kubwa ya mashambulizi, safu yake imeweza kubaki makini na kufanya maamuzi sahihi.
“Tunawapongeza kwa kazi wanayoifanya, lakini hatutaki kubweteka kwa sababu tumeruhusu bao moja katika michezo mitatu. Tunajua ligi ni ndefu na kila mchezo una changamoto zake, hivyo tunahitaji kuendelea kuwa na umakini uleule,” alisema.
Makata alisema pamoja na kuwa na ukuta imara, bado hawajafikia kiwango wanachokihitaji na wanaendelea kufanyia kazi maeneo mbalimbali ya timu ili kuhakikisha mwanzo huo mzuri hauishii kwenye raundi chache za kwanza.
“Ukiwa na ukuta wenye nidhamu unakuwa umejipa nafasi kubwa ya kupata matokeo. Lakini tunahitaji kuendelea kufanya kazi kwa sababu tunataka kuwa bora zaidi. Bao moja tuliloruhusu lilitokana na penalti, lakini hatutaki kuangalia takwimu pekee, tunataka kuona ubora wa timu unaongezeka kila mchezo,” alisema.
Mbali na uimara wa safu ya ulinzi, Polisi Tanzania pia ina faida ya kuwa na washambuliaji wenye uzoefu mkubwa katika Ligi Kuu, akiwamo Habibu Kyombo, aliyewahi kuitumikia Simba ambapo sasa ana bao moja. Mwingine ni Anuary Jabir mwenye mabao mawili. Timu hiyo imefunga mabao manne, lingine likiwekwa kimiani na kiungo Kenny Ally.