Straika KMC asaka rekodi mpya Championship
Muktasari:
- Nyota huyo aliyejiunga na kikosi hicho kwa msimu huu wa 2026-2027, amekuwa na mwenendo mzuri wa kufunga ambapo hadi sasa tayari amefunga mabao matatu, akibakisha nane kufikia rekodi yake ya msimu wa 2025-2026, wakati akiichezea Transit Camp.
MSHAMBULIAJI nyota wa KMC FC, Adam Uledi amesema licha ya ushindani mkali uliopo msimu huu wa 2026-2027, katika Ligi ya Championship, ila mojawapo ya malengo yake binafsi ni kukirejesha kikosi hicho Ligi Kuu Bara na kuvunja rekodi ya mabao.
Nyota huyo aliyejiunga na kikosi hicho kwa msimu huu wa 2026-2027, amekuwa na mwenendo mzuri wa kufunga ambapo hadi sasa tayari amefunga mabao matatu, akibakisha nane kufikia rekodi yake ya msimu wa 2025-2026, wakati akiichezea Transit Camp.
Mshambuliaji huyo msimu wa 2025-2026, aliifungia Transit Camp jumla ya mabao 11.
Akizungumza na Mwanaspoti, Uledi amesema kasi nzuri aliyonayo msimu huu inampa matumaini makubwa ya kuifikia rekodi yake na kuivunja ya msimu wa 2025-2026, licha ya ushindani unaoendelea kutoka kwa washambuliaji wenzake wa timu mbalimbali.
“Ushindani wa washambulaji wenzangu unanipa motisha ya kuendelea kupambana zaidi, ila kikubwa ni kuipambania KMC FC ili irudi tena kucheza Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2025-2026, naamini kwa umoja wetu tutafanikiwa,” amesema Uledi.
Mabao hayo matatu aliyoyafunga Uledi, ni sawa na yaliyofungwa na mshambuliaji mwenzake wa KMC FC, Ramadhan Hashim, huku anayeongoza katika mbio hizo ni Abiud Mtambuka wa Mbeya Kwanza na Hamdan Farhan wa Transit Camp wenye manne kila mmoja.