Vita ya mabingwa KVZ, KMKM
Muktasari:
- Mechi hiyo itachezwa kesho, Jumapili saa 10:00 jioni kwenye uwanja wa Mao Zedong huku macho yote yakiwa kwa wababe hao.
MABINGWA watetezi wa Ngao ya jamii Zanzibar, KMKM na bingwa wa Ligi Kuu Zanzibar, KVZ watafungua pazia la kuanza kwa ligi hiyo.
Mechi hiyo itachezwa kesho, Jumapili saa 10:00 jioni kwenye uwanja wa Mao Zedong huku macho yote yakiwa kwa wababe hao.
Wakati KMKM, inachua ngao hiyo msimu uliyopita ilikuwa ikinolewa na Hababuu Ali ambaye kwasasa ndiye Kocha Mkuu wa KVZ.
Kwa maana hiyo, Kocha huyo anakibarua cha kupindua meza kwa mahasimu wake kuondoka na Ngao hiyo mbele ya wapinzani wake.
Katika msimu uliopita, Timu ya KMKM ilitwaa ubingwa baada ya kupata ushindi kwa kuifunga Mlandege mikwaju ya penati 5-3 baada ya dakika 90 kutoka bila kufungana(0-0).
Akizunguzia kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa KVZ, Hababuu Ali amesema timu hiyo inajipanga kuchukua ngao ya Jamii na huo utakuwa mwanzo mzuri upande wao.
Amesema, Hamu na shauku yake kubwa kutwaa taji hilo mbele ya wapinzani wake aliochukua nao kipindi wakiwa pamoja na sasa anahitaji kuvunja rikodi yake. “Mechi ya kesho itakuwa ngumu sana kwasababu ndio inayofungua Ligi Kuu Zanzibar inayoanza rasmi Agosti 29, lakini nataka nianze vizuri kwa kutwaa ubingwa wa ngao hiyo,” amesema
Ameeleza kuwa hiyo ni hatua kubwa upande wao kupata nafasi hiyo na watahakikisha wanaitumia inavyotakiwa kwa kuibuka na ushindi.
Pia, Shirikisho la soka Zanzibar(ZFF), limesema msimu huu litauza tiketi kwa kutumia mfumo wa kisasa wa N-Card na si mkononi kama ilivyozoeleka na mfumo huo utaaza kufanya kazi katika mchezo wa kesho.
Taarifa hiyo imetolewa juzi Agosti 19, 2026 na Ofisa Habari wa ZFF, Mohamed Kabwanga wakati akizungumza na waandishi wa Habari katika Makao Makuu ya Ofisi hizo yaliyopo Mbuyu Mnene.
Amesema kiingilio cha mchezo huo kitakuwa Sh2,000 na na tiketi zitauzwa kwa mfumo wa N-Card.
Naye, Ofisa Masoko kutoka N-Card, Mohamed Yusuf amesema tiketi zinapatikana Ofisi za ZFF, Mbuyu Mnene, TTCL Posta, Kijangwani na viwanja vya Mao siku ya mchezo na kusisitiza kuwa tiketi zinapatikana kwa urahisi na ufanisi mkubwa kupitia mfumo huo.