Wanajeshi kuipa makali Yanga
Muktasari:
- Taarifa za ndani kutoka Yanga zimeliambia Mwanaspoti kuwa, timu hiyo inatarajiwa kucheza mchezo huo ikiwa ni sehemu ya programu ya benchi la ufundi kuhakikisha wachezaji wanaendelea kuwa katika hali nzuri ya ushindani kuelekea mchezo mkubwa wa Oktoba 10, 2026 dhidi ya Simba.
WAKATI Dabi ya Kariakoo ikizidi kusogea, Yanga imeanza kusuka mipango ya kuongeza makali ambapo leo Jumamosi itakabiliana na wanajeshi wa JKT Tanzania.
Taarifa za ndani kutoka Yanga zimeliambia Mwanaspoti kuwa, timu hiyo inatarajiwa kucheza mchezo huo ikiwa ni sehemu ya programu ya benchi la ufundi kuhakikisha wachezaji wanaendelea kuwa katika hali nzuri ya ushindani kuelekea mchezo mkubwa wa Oktoba 10, 2026 dhidi ya Simba.
Hata hivyo, hadi sasa muda rasmi wa mchezo huo haujajulikana wala kiwanja, huku wachezaji wa JKT wakiwa wameshapewa ratiba hiyo ya kukutana na Yanga leo kwenye mechi ya kirafiki.
JKT Tanzania nayo iko kwenye ratiba ya maandalizi, ikiwa inajiandaa na safari ya kwenda kukutana na Fountain Gate katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, mechi ikipangwa kuchezwa 9, 2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Kwa Yanga, mchezo dhidi ya JKT Tanzania unaweza kuwa sehemu ya maandalizi muhimu kuelekea Dabi ya Kariakoo inayotarajiwa kuchezwa Oktoba 10, 2026. Huku Benchi la ufundi likitumia muda uliopo kurejesha utimamu wa wachezaji, licha ya kuwapa program maalum wakati wa likizo.
Wakati Yanga ikitafuta mchezo wa kirafiki, Simba nayo imeendelea kujichimbia Afrika Kusini na jana Ijumaa ilikuwa na mechi ya kirafiki dhidi ya Polokwane City, huku leo Jumamosi ikikabiliana na Sekhukhune United, kabla ya kuanza safari ya kurejea Tanzania.
Simba imekuwa Afrika Kusini tangu Septemba 24, 2026 kwa ajili ya maandalizi ya mechi zijazo za mashindano ikiwemo Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga.
Yanga iliyoingia kambini Septemba 30, 2026 ikiendelea kujifua kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, kikosi hicho kilianza programu hizo kikiwa hakijakamilika kwa asilimia 100 kutokana na baadhi ya wachezaji kuwa na majukumu ya timu zao za taifa, lakini wanaendelea kuongeza umakini kuelekea dabi hiyo ya Oktoba 10, 2026.
REKODI ZAO
Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu huu, Yanga inaongoza ikiwa na pointi 18 ambazo pia inazo Simba, lakini tofauti ya mabao inawatenganisha wakongwe hao. Yanga imefunga mabao 16, Simba ikiwa nayo 11, zote zikiruhusu mawili katika mechi sita zilizocheza.
Katika kukutana kwao kwenye ligi, misimu mitatu iliyopita, Yanga imeshinda Dabi ya Kariakoo mara nne, huku mbili zikiwa sare. Simba inaingia katika Dabi ya Oktoba 10 ikisaka ushindi wa kwanza dhidi ya Yanga kwenye ligi kwani haijafanikiwa tangu mara ya mwisho iliposhinda 2-0, Aprili 16, 2023.
Baada ya kumalizika ratiba iliyopo katika kalenda ya Fifa, sasa macho yanaelekezwa Oktoba 10, 2026, ambapo Simba na Yanga zitakutana katika Dabi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu, mchezo huo umepangwa kuchezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku.