Baleba apewa somo la Carrick kuibeba Man United
Muktasari:
- Miaka 20 iliyopita, Carrick alijiunga na Manchester United akitokea Tottenham kwa ada ya Pauni18.6 milioni, akiwa kiungo wa chini aliyekuwa akifanya kazi kubwa katika eneo la kiungo.
MANCHESTER, England. KIUNGO Carlos Baleba ana kila sababu ya kumtazama kocha wake mpya, Michael Carrick, kama chanzo cha msukumo katika harakati za kuisaidia Manchester United kurejea kwenye kilele cha soka la England.
Miaka 20 iliyopita, Carrick alijiunga na Manchester United akitokea Tottenham kwa ada ya Pauni18.6 milioni, akiwa kiungo wa chini aliyekuwa akifanya kazi kubwa katika eneo la kiungo.
Sasa, miaka miwili baada ya kuanza kwake kama kocha wa United, usajili mkubwa zaidi wa Carrick katika dirisha hili la majira ya kiangazi umekuwa mwingine wa aina hiyo, Baleba (22), ambaye amesajiliwa kutoka Brighton kwa ada ya awali ya Pauni65 milioni.
United walionyesha nia ya kumsajili kiungo huyo wa Cameroon tangu mwaka jana, jambo linaloibua swali kwa nini walilazimika kusubiri hadi wiki ya mwisho ya dirisha la usajili.
Hata hivyo, sasa Carrick amekamilisha maboresho ya safu yake ya kiungo baada ya pia kuwasajili Youri Tielemans na Andrey Santos.
Mwisho wa msimu uliopita, United pia walimhakikishia kiungo wa England, Kobbie Mainoo (21), mkataba mpya utakaomuweka klabuni hapo hadi 2031.
Tangu Carrick alipowasili Old Trafford mwaka 2006, hakuna mchezaji wa nafasi yake aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika kubadili mwenendo wa United kama alivyofanya yeye.
Wakati huo, Sir Alex Ferguson alihitaji kuimarisha safu yake ya kiungo baada ya United kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa misimu mitatu mfululizo.
Carrick alikuwa kipande cha mwisho cha fumbo hilo na United walitwaa ubingwa katika msimu wake wa kwanza.
Pamoja na Owen Hargreaves, ambaye alijiunga na United msimu uliofuata, Carrick alikuwa mhimili muhimu katika mafanikio ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara tano katika misimu saba ya mwisho ya Ferguson, sambamba na kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008, kabla ya kocha huyo kustaafu mwaka 2013.
Baada ya Carrick na Hargreaves, United wamefanya usajili mkubwa katika eneo la kiungo, wakiwemo Marouane Fellaini, Paul Pogba, Fred, Casemiro na Manuel Ugarte.
Lakini hakuna aliyefanikiwa kuirudisha United kwenye kiwango cha zamani cha kutawala Ligi Kuu.
Pogba alikuwa mchezaji aliyemvutia Baleba tangu akiwa mdogo, lakini United watakuwa na matumaini kwamba historia yake haitafanana na ya Mfaransa huyo, ambaye kipindi chake cha pili Old Trafford kiligubikwa na matatizo na mvutano wa kutaka kuondoka.
BALEBA SULUHISHO LA TATIZO LA NAMBA SITA
Usajili wa Baleba unaweza pia kuwa ishara kwamba Andrey Santos, aliyesajiliwa kutoka Chelsea kwa Pauni50 milioni, hawezi kutoa majibu yote katika nafasi ya kiungo mkabaji, namba sita.
Santos hana nguvu za kimwili kama Baleba, huku hitaji la United la kupata kiungo maalumu wa ulinzi likiwafanya mwezi uliopita kuulizia tena uwezekano wa kumsajili Aurelien Tchouameni kutoka Real Madrid.
Hata hivyo, Baleba amekuwa chaguo la gharama nafuu zaidi kwa upande wa ada na mshahara, huku pia akiwa na uzoefu wa miaka mitatu katika Ligi Kuu England.
Mkurugenzi wa soka wa United, Jason Wilcox, alisema: “Dhamira ya Carlos kujiunga na Manchester United na imani yake kwamba tutafikia malengo yetu ya pamoja vinamfanya kuwa usajili bora kwetu.”
Baleba alivutiwa na maono ya United kuhusu maendeleo yake na namna alivyohakikishiwa kuwa klabu hiyo inamhitaji.
Kiungo huyo aliwahi kufanya mazungumzo mafupi na Carrick na pia kuzungumza kwa kina na Matheus Cunha baada ya United kuifunga Brighton 3-0 katika mchezo wa mwisho wa msimu uliopita.
Ingawa Brighton ilikuwa imefuzu kushiriki Conference League, Baleba alikuwa na malengo makubwa zaidi.
Atapata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa akiwa United na anaamini anafaa katika kikosi hicho baada ya kuzoea kasi na ushindani wa Ligi Kuu England katika misimu yake mitatu iliyopita.
Usajili wa Baleba umekamilisha ujenzi upya wa kikosi cha United kuelekea msimu mpya.
FERNANDES ANA KIKOSI CHA UBINGWA
Mustakabali wa Bruno Fernandes umekuwa ukijadiliwa kwa miezi kadhaa, lakini wiki hii nahodha huyo wa United alitwaa tuzo ya PFA ya Mchezaji Bora wa Mwaka, akiwa mchezaji wa kwanza wa klabu hiyo kushinda tuzo hiyo tangu Wayne Rooney mwaka 2010.
Licha ya kuwa na tuzo nyingi binafsi, Fernandes amekuwa akipata wakati mgumu katika kushinda mataji ya timu.
Katika takribani miaka saba akiwa United, ameshinda mataji mawili pekee, huku timu hiyo pia ikipoteza fainali mbili za mashindano ya Ulaya katika kipindi hicho.
Sasa hana tena sababu ya kulalamika kwamba kikosi hakina ubora wa kutosha.
Ingawa United bado wanaonekana kutokuwa imara kwenye safu ya ulinzi, wana mabeki tisa wa kikosi cha kwanza walio fiti, huku ujio wa Baleba ukiongeza uwiano na nguvu katika timu.
Fernandes alikuwa karibu na Casemiro ambaye alikuwa akicheza nafasi hiyo kabla ya kuondoka United msimu huu.
Baleba huenda hana uzoefu na hadhi ya Casemiro, ambaye ameshinda Ligi ya Mabingwa mara tano, lakini ana kasi, nguvu na uwezo mkubwa zaidi wa kufanya kazi katika maeneo mbalimbali ya uwanja.
Fernandes atatimiza miaka 32 Septemba na mkataba wake wa sasa unamalizika mwakani.
United wanatarajiwa kutumia kipengele cha kuongeza mkataba wake kwa mwaka mmoja hadi 2028, isipokuwa kama watampa mkataba mpya kabla ya hapo.
Klabu hiyo imeweka mwaka 2028, ambao utakuwa kumbukumbu ya miaka 150 tangu kuanzishwa kwake, kama lengo la kumaliza kusubiri kwa muda mrefu kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
Kutwaa taji la 21 la Ligi Kuu katika historia ya United hakutakuwa tu zawadi nzuri ya kuhitimisha kipindi cha Fernandes klabuni hapo, bali pia kungeimarisha zaidi nafasi yake miongoni mwa magwiji wa klabu hiyo.
Hata kabla ya kipigo cha kushangaza cha mabao 2-0 dhidi ya Hull Jumamosi iliyopita, ambacho kilifanya United kuanza msimu vibaya, ilikuwa wazi kwamba huenda msimu huu ukawa mapema mno kwao kutarajia ubingwa.
Hata hivyo, United hawapaswi kupata shida kumshawishi Fernandes kusaini mkataba mpya.
Kiungo huyo anaweza kuwa na nguvu zaidi kwenye mazungumzo ya mshahara, hasa kutokana na kurejea kwa Marcus Rashford, ambaye ndiye mchezaji anayelipwa zaidi klabuni hapo licha ya kucheza mchezo wake wa mwisho wa kuanza kikosi cha United Desemba 2024.
United wamekuwa wazi kwamba wanataka muundo wao wa mishahara kuhakikisha mchezaji wao bora ndiye anayelipwa zaidi. Tuzo ya PFA aliyotwaa Fernandes imeongeza uzito wa hoja hiyo.
Na katika harakati zake za kutaka kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Fernandes anaweza pia kupata msukumo kutoka kwa Carrick mchezaji ambaye aliwahi kusaidia United kuvuka kipindi kigumu na kurejea kileleni mwa England.