EPL ni neema

Muktasari:
- Leeds inarudi Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza tangu 2023 iliposhuka wakati Burnley ikirejea baada ya kukosekana kwa msimu mmoja.
MANCHESTER, ENGLAND: TIMU za Ligi Kuu England, Manchester United, Arsenal na Liverpool ambazo zinapambana kutafuta pesa kwa ajili ya kufanya usajili ili kuboresha vikosi ziko mbioni kupokea mapato makubwa baada ya Burnley na Leeds kurejea Ligi Kuu msimu ujao.
Leeds inarudi Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza tangu 2023 iliposhuka wakati Burnley ikirejea baada ya kukosekana kwa msimu mmoja.
Kupanda daraja kwa timu hizo kumezipa timu nyingine 17 za ligi hiyo kiasi cha pesa ambazo zitaongezeka katika mgawo kabla ya msimu kuanza.
Iko hivi, kila msimu timu tatu ambazo zinashuka daraja kwenda Ligi ya Champioship, Bodi ya Ligi England huzipa pesa kwa ajili ya kuzisaidia kuongeza nguvu na kuhakikisha zinarudi Ligi Kuu England haraka.
Pesa hizo hupewa kwa misimu mitatu zitakayokuwa katika Ligi ya Championship baada ya hapo zitakomaa na kutakiwa kupambana zenyewe ili kupanda.
Vilevile, kiasi cha pesa ambacho hupewa kwa msimu wa kwanza huwa ni asilimia 50 ya pesa zilizovuna zilipokuwa Ligi Kuu msimu mmoja kabla ya kushuka, msimu wapili hupewa asilimia 45 na ule wa tatu huambulia asilimia 20, ingawa kwenye hizo 20 za msimu wa tatu hutolewa kwa timu zilizoshiriki Ligi Kuu kwa misimu miwili au zaidi kabla ya kushuka. Ikiwa timu iliyoshuka daraja ikirudi kabla ya kumalizika misimu mitatu Championship, ile pesa iliyotakiwa walipwe katika msimu uliobaki kama wamecheza mmoja basi miwili iliyobaki huchukuliwa na kugawiwa timu 17 zilizofanikiwa kusalia kwenye ligi katika msimu ambao zimepanda.
Hivyo kwa sasa, baada ya Leeds na Burnley kupanda zikiwa hazijamaliza misimu mitatu Championship, pesa ambazo zimesalia zitatolewa kwa timu 17 ambazo zitabaki kwenye ligi msimu huu.
Inaelezwa Baada ya Burnley na Leeds kupanda kiasi cha Pauni 51 milioni kimehifadhiwa, na sasa zitagawanywa katika timu za Ligi Kuu.
Burnley ilikuwa inatarajiwa kupata Pauni 35 milioni ya kiasi hicho cha pesa wakati Leeds ikiwa ni Pauni 16 milioni.