Man United njia nyeupe kwa Victor Osimhen

Muktasari:
- Hata hivyo, Chelsea imeamua kuachana na dili hilo, jambo linaloipa Man United nafasi kubwa ya kumpata Osimhen ambaye mkataba wake na Napoli unatarajiwa kumalizika 2026.
MANCHESTER United inaonekana kuwa na asilimia kubwa zaidi ya kuipata saini ya mshambuliaji wa Napoli na timu ya taifa ya Nigeria ambaye kwa sasa anaichezea Galatasaray kwa mkopo, Victor Osimhen.
Fundi huyo ambaye msimu huu amecheza mechi 32 za michuano yote na kufunga mabao 28, katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana alikuwa karibu kutua Chelsea, lakini dili lilifeli dakika za mwisho na ikaelezwa matajiri hao wa London wanaweza kurudi mezani mwisho wa msimu huu.
Hata hivyo, Chelsea imeamua kuachana na dili hilo, jambo linaloipa Man United nafasi kubwa ya kumpata Osimhen ambaye mkataba wake na Napoli unatarajiwa kumalizika 2026.
Napoli ipo tayari kumuuza kwa bei pungufu tofauti na ile ambayo ilikuwa ikihitaji katika dirisha lililopita kuanzia Euro 100 milioni.
Matheus Cunha
MANCHESTER United wanataka kumsajili mshambuliaji wa Wolves na timu ya taifa ya Brazil, Matheus Cunha, 25, ambaye ana kipengele kitakachoziruhusu timu zinazomtaka kutoa Pauni 62.5 milioni katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili kumsajili. Mkataba wa sasa wa Cunha unatarajiwa kumalizika 2029 na msimu huu amecheza mechi 29 za michuano yote akifunga mabao 15.
Timo Werner
MABOSI wa Tottenham Hotspur wamesisitiza kwamba hawatamsainisha mkataba wa kudumu mshambuliaji wa RB Leipzig, Timo Werner, mwenye umri wa miaka 29, baada ya mkataba wake wa mkopo kumalizika mwisho wa msimu huu. Spurs haitaki kumsainisha mchezaji huyo mkataba mpya kwa sababu haivutiwi na kiwango alichoonyesha tangu ajiunge nayo.
Kevin de Bruyne
INTER Miami inapambana kufanikiwa ili kumsajili kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya Ublelgiji, Kevin de Bruyne, 33, katika dirisha lijalo lakini inakumbana na upinzani kutoka kwa timu za Saudi Arabia ambazo zinaitaka saini yake. De Bruyne ametangaza kuwa ataondoka mwisho wa msimu huu ikiwa ni baada ya kudumu kwa miaka 10 katika kikosi cha Man City.
Jamie Gittens
WINGA wa Borussia Dortmund, Jamie Gittens amewasilisha barua ya kuomba kuondoka katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo timu kibao kutoka England zinahitaji saini yake. Gittens mwenye umri wa miaka 20 ambaye anaichezea timu ya taifa ya England ya vijana wenye umri chini ya miaka 21 kuna timu kibao za Ligi Kuu Engand zimeonyesha nia ya kumsajili.
Liam Delap
EVERTON na Brighton zimeingia katika vita ya kuwania saini ya mshambuliaji wa Ipswich Town na timu ya taifa ya England kwa vijana wenye umri chini ya miaka 21, Liam Delap, 22. Staa huyu ambaye msimu huu amecheza mechi 33 za michuano yote na kufunga mabao 12, atapatikana kwa kiasi cha Pauni 40 milioni ikiwa timu yake itashuka kutoka Ligi Kuu England.
David de Gea
FIORENTINA ipo katika mazungumzo na wawakilishi wa kipa wake raia wa Hispania, David de Gea, 34, ili kumsainisha staa huyo mkataba mpya wa mwaka mmoja utakaomwezesha kubaki hadi 2026. Benchi la ufundi la Fiorentina linataka kumsainisha mchezaji huyo mkataba mpya baada ya kuvutiwa sana na kiwango alichoonyesha tangu ajiunge msimu huu.
Mark Flekken
BAYER Leverkusen inamevutiwa na kiwango cha kipa wa Brentford, Mark Flekken, 31, na inataka kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Taarifa kutoka Sky Sports zinaeleza Brentford inahitaji kiasi kisichopungua Euro 15 milioni ili kumuuza staa huyo wa kimataifa wa Uholanzi ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2027.