NDOTO: Kocha Barcelona akili iko kwenye mataji matatu tu

Muktasari:
- Kocha huyo kutoka Kijerumani amekuwa na msimu mzuri sana tangu amrithi Xavi kama kocha mkuu katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.
BARCELONA, HISPANIA: KOCHA wa Barcelona, Hansi Flick amepuuza wazo la kusaini mkataba wa muda mrefu na Barcelona licha ya kuwekewa ofa mezani na badala yake anataka kuwekeza akili yake kwenye kushinda mataji matatu yaliyo mbele yake msimu huu.
Kocha huyo kutoka Kijerumani amekuwa na msimu mzuri sana tangu amrithi Xavi kama kocha mkuu katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.
Barcelona bado wana nafasi ya kumaliza msimu wakiwa na mataji matatu (treble), la kwanza ni lile la La Liga ambapo wapo kileleni kwa tofauti ya alama nne dhidi ya Real Madrid, pia wamefika fainali ya Copa del Rey, na wanaweza kuchukua Ligi ya Mabingwa ambako wapo robo fainali na mchezo wa mkondo wa kwanza dhidi ya wapinzani wao Borussia Dortmund walifanikiwa kushinda mabao 4-0.
Mafanikio hayo ya Barca yamesababisha mabosi wake kutaka kumpa kocha mkataba mpya wakati ule wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwaka 2026 lakini Flick ameweka wazi kuwa hana mpango wa kusaini mkataba mpya hivi karibuni.
“Nathamini sana na ninafurahia kile nilicho nacho hapa kuanzia wasaidizi wangu katika benchi la ufundi, madaktari na wachezaji wa kiwango cha juu ambao wanapambana kuhakikisha wanakuwa bora kila siku jambo ambalo ni la kipekee sana katika taalama yangu kama kocha.”
“Hiyo ndiyo hali ilivyo sasa, nimebakisha mwaka mmoja katika mkataba wanguna tukifanya vizuri, huenda nikaongeza mwingine. Hivyo ndivyo ninavyofikiria, mimi sio kocha anayefikiria miaka mitatu mbele, nataka kufanya hatua kwa hatua, mwaka baada ya mwaka, najua ni jambo muhimu lakini kwa sasa tunatakiwa kuzingatia na kuwekeza akili zetu katika msimu huu kwani kuna vitu vingi sana vyakufanya.”