Real Madrid, Saliba ngoma yawekwa kando

Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa Real Madrid itasubiri hadi dirisha la majira ya kiangazi mwakani ambapo inaamini itampata kwa ada ndogo ya uhamisho kwani mkataba wake utakuwa umebakiza mwaka mmoja kabla ya kumalizika.
REAL Madrid wanapanga kusubiri kwa muda katika harakati za kumsajili beki wa kati wa Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, William Saliba, mwenye umri wa miaka 24.
Kwa mujibu wa taarifa Real Madrid itasubiri hadi dirisha la majira ya kiangazi mwakani ambapo inaamini itampata kwa ada ndogo ya uhamisho kwani mkataba wake utakuwa umebakiza mwaka mmoja kabla ya kumalizika.
Real Madrid imekuwa ikihusishwa na staa huyo tangu dirisha la majira ya kiangazi mwaka juzi, lakini changamoto kubwa imekuwa ni Saliba mwenyewe mara zote ambazo wamefanya naye mazungumzo kusisitiza kuendelea kubakia Arsenal. Mkataba wa staa huyo unatarajiwa kumalizika 2027. Msimu huu amecheza mechi 42 za michuano yote.
Rasmus Hojlund
MANCHESTER United wapo tayari kusikiliza ofa kutoka timu zinazoitaka huduma ya mshambuliaji raia wa Denmark, Rasmus Hojlund, 22, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Mabosi wa Manchester United wapo tayari kumuuza mchezaji huyo kwa kiasi kisichopungua Pauni 52 milioni. Mkataba wa sasa wa staa huyo unatarajiwa kumalizika 2028.
Morgan Gibbs-White
MANCHESTER City imeambiwa kuwa italazimika kulipa Pauni 100 milioni ili kuipata saini ya kiungo wa Nottingham Forest na timu ya taifa ya England, Morgan Gibbs-White kaitka dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Morgan ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2027 na msimu huu amecheza mechi 30 za michuano yote.
Mathys Tel
TTOTTENHAM Hotspur inatafakari kumsainisha mkataba wa kudumu mshambuliaji wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa, Mathys Tel, 19, mwisho wa msimu huu. Katika mkataba wa mkopo kuna kipengele kinachoiruhusu Spurs kulipa Euro 50 hadi 55 milioni, lakini haitaki kutoa kwani inaamini ni kikubwa sana.
Lionel Messi
INTER Miami iko katika hatua za mwisho kufikia makubaliano na wawakilishi wa mshambuliaji tegemeo, Lionel Messi kwa ajili ya kumsainisha mkataba mpya wakati ule wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwisho wa mwaka huu. Messi mwenye umri wa miaka 37, msimu huu amecheza mechi tisa za michuano yote na kufunga mabao manane.
Matheus Cunha
MANCHESTER United, Newcastle United, Arsenal, Aston Villa, Nottingham Forest na Tottenham Hotspur ziko katika vita ya kuwania saini ya mshambuliaji wa Wolves na timu ya taifa ya Brazil, Matheus Cunha, 25. Timu nyingi zimevutiwa na kiwango alichoonyesha tangu msimu uliopita. Mkataba wake unamalizika 2029. Msimu huu amecheza mechi 29 na kufunga mabao 15.
Yahia Fofana
NEWCASTLE United, Wolves na Brentford zinapambana kuiwania saini ya kipa wa Angers na timu ya taifa ya Ivory Coast, Yahia Fofana, 24, ambaye anauzwa kwa kiasi kisichopungua Pauni 15 milioni. Fofana ni miongoni mwa makipa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Angers na mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwakani.
Hugo Larsson
EENTRACH Frankfurt imesisitiza inahitaji kiasi cha pesa kisichopungua Pauni 50 milioni kutoka kwa timu inayoitaka saini ya kiungo wake na timu ya taifa ya Sweden, Hugo Larsson, 20, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Timu kibao ikiwemo Manchester City zinahitaji huduma ya staa huyo lakini changamoto ni fedha za mauzo kuwa kubwa.