Tuchel afagilia kiwango cha England
Muktasari:
- England ilifanya mashambulizi ya kutisha tangu mwanzo, huku nahodha Harry Kane na Bukayo Saka wakifunga mabao mawili kila mmoja.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa England, Thomas Tuchel ameisifu timu yake kwa kuonyesha kiwango cha juu baada ya kuichakaza Croatia mabao 7-0 katika mchezo wa Ligi ya Mataifa uliochezwa mwishoni wa wiki jijini Rijeka.
England ilifanya mashambulizi ya kutisha tangu mwanzo, huku nahodha Harry Kane na Bukayo Saka wakifunga mabao mawili kila mmoja.
Jude Bellingham pia alitikisa nyavu na kutoa pasi tatu za mabao, wakati Anthony Gordon na Morgan Rogers wakikamilisha ushindi huo mkubwa ambao umekuwa wa aina yake tangu Tuchel alipoanza kuinoa England.
“Ulikuwa mchezo wa dakika 90 katika kiwango cha juu zaidi kutoka kwa kila mtu. Kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho, waliokuwa kwenye kikosi cha kwanza na wale walioingia benchi, wote walikuwa katika kiwango cha juu. Hongera kwa timu,” amesema Tuchel.
Kocha huyo raia wa Ujerumani alivutiwa zaidi na namna England ilivyodumisha kasi na presha kwa muda wote, hasa dhidi ya safu ya ulinzi ya Croatia.
“Tuliendelea na kasi na kutumia mianya iliyokuwapo. Tulikuwa makini sana katika kutumia nafasi. Pia tuliendelea kuwa na njaa kwenye presha ya mara kwa mara na wakati wa kujilinda.
“Ninapenda mtazamo huu. Kila mara tulicheza kwa unyenyekevu na kuhakikisha tunafanya mambo ya msingi kwa usahihi, ndiyo maana ilikuwa mechi iliyokamilika,” amesema.
Kane pia alifurahishwa na kiwango hicho, huku ushindi huo ukiwa wa pili mfululizo kwa England katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mataifa.
Baada ya kuanza kwa kupoteza dhidi ya mabingwa wa dunia, Hispania, England ilijibu kwa kuifunga Jamhuri ya Czech mabao 2-0 Jumanne kabla ya kuichakaza Croatia.
“Kila mchezaji alikuwa katika kiwango cha juu. Ilikuwa kazi ya ajabu kuanzia mwanzo hadi mwisho.
“Tulizungumza sana kuhusu kucheza dakika 90 kwa kiwango kilekile, kutawala kwa mpira na hata bila mpira. Na ndivyo ilivyokuwa leo.
“Tukiwa huru na tunapotumia nguvu zetu vizuri, ndipo tunapokuwa bora zaidi. Tulicheza kwa kiwango cha Ligi Kuu England na umeona matokeo. Hawakuweza kuendana na kasi yetu wala mbio zetu,” amesema Kane.
England itamaliza mapumziko ya mechi za kimataifa kwa kuikaribisha Jamhuri ya Czech Jumanne, ushindi ukiwaweka katika nafasi nzuri ya kumaliza ndani ya timu mbili za juu zitakazofuzu hatua ya robo fainali.
Kane, ambaye tayari amevunja rekodi ya ufungaji ya England akiwa na mabao 89, pia anatarajiwa kufikisha mechi 125 dhidi ya Czech na kusogea karibu na rekodi ya Peter Shilton ya mechi nyingi za timu hiyo.
“Litakuwa jambo zuri. Ndiyo maana kocha hunitoa mapema, ili kuniweka tayari kwa mchezo unaofuata!” amesema Kane kwa utani.