Tuchel amwandalia dawa Jude Bellingham

Muktasari:
- Kiungo huyo wa Real Madrid ambaye alikuwa msaada sana katika ushindi wa mabao 2-0 wa England dhidi ya Albania, amesababisha Tuchel atoe kauli hiyo kwa sababu huwa anafanya vitu vingi kiwanjani na vingine sio vya lazima.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel amepanga kuja na njia mbadala ya kumfanya staa wa timu hiyo Jude Bellingham atunze nguvu zake kwa ajili ya muda muhimu na kudhibiti hisia zake.
Kiungo huyo wa Real Madrid ambaye alikuwa msaada sana katika ushindi wa mabao 2-0 wa England dhidi ya Albania, amesababisha Tuchel atoe kauli hiyo kwa sababu huwa anafanya vitu vingi kiwanjani na vingine sio vya lazima.
“Daima yuko tayari kutoa kila kitu. Lakini tunahitaji kumsaidia ili akae ndani ya muundo, aweze kucheza kama mwanauchumi zaidi na bado awe na athari kubwa, tunahitaji kuhakikisha wachezaji muhimu wanatembea kwa mwelekeo mmoja, wanacheza kwa kasi moja na kusaidiana.”
“Vilevile wacheze kidogo kwa nidhamu zaidi pengine, ili kuhifadhi baadhi ya nguvu kwa ajili ya nyakati muhimu.
“Anapenda (Bellingham) kuzungumza na mwamuzi na waamuzi wa pembeni. Jude ni mchezaji mwenye hisia kubwa awapo kiwanjani na unaona sio tu kwamba anachukia kushindwa, bali ana hamu ya kushinda.
“Nadhani anatakiwa kuhifadhi njaa hii na atajifunza kudhibiti hisia zake kidogo.”
Tuchel ambaye aliwahi kuwaongoza mastaa wakubwa kama Neymar na Kylian Mbappe huko Paris Saint-Germain anaamini Jude anatumia muda mwingi kiwanjani kulalamika na kuongea na waamuzi jambo ambalo linasababisha atumie nguvu nyingi huko ambazo angeweza kuziwekeza kiwanjani na zikasaidia zaidi timu.