Usajili wa mastrika utatikisa

Muktasari:
- Na jambo hilo litamfanya bosi mpya wa masuala ya usajili, mkurugenzi wa michezo wa kikosi hicho cha Emirates, Andrea Berta kutarajia kuwa kwenye shughuli pevu ya kuhakikisha anampata straika, ambaye atakuwa na faida kubwa kwenye mipango ya kocha Mikel Arteta.
LONDON, ENGLAND: NI kitu cha wazi kabisa, Arsenal itakuwa bize kwelikweli kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kusaka straika mpya wa kuja kuwapigia mabao msimu ujao.
Na jambo hilo litamfanya bosi mpya wa masuala ya usajili, mkurugenzi wa michezo wa kikosi hicho cha Emirates, Andrea Berta kutarajia kuwa kwenye shughuli pevu ya kuhakikisha anampata straika, ambaye atakuwa na faida kubwa kwenye mipango ya kocha Mikel Arteta.
Kibarua chake cha kwanza bosi huyo wa usajili huko Arsenal ni kunasa straika, ambaye ataifanya timu hiyo kushinda mataji. Hata hivyo, Berta hataingia tu sokoni kusana Namba 9 mpya.
Wapinzani wao kwenye Ligi Kuu England, Chelsea, Manchester United na Liverpool nao wataingia sokoni kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi kunasa washambuliaji wa kati.
Straika wa Newcastle United, Alexander Isak yupo kwenye rada karibu na kila timu kwenye orodha ya klabu hizo, lakini Newcastle wenyewe wamekuwa na msimamo kwamba supastaa huyo wa Sweden haendi kokote.

Lakini, msimamo wa Newcastle United wa kugoma kumpiga bei Isak kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, inaweza kukwama endapo kama miamba hiyo ya St James’ Park itashindwa kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Na kama Isak atapigwa bei, basi Newcastle itakuwa na uhakika wa kuvuna Pauni 150 milioni.
Vikwazo vya kimatumizi kwenye Ligi Kuu England ndio sababu ya Isak kuendelea kubaki St James’ Park hadi sasa, kutokana na klabu kubwa kutokuwa na pesa za kutosha kulipia ada ya uhamisho ya mchezaji huyo.
Kitu kama hicho kitamhusu pia straika wa zamani wa Manchester City, Julian Alvarez endapo kama kutakuwa timu inayotaka kumrudisha kwenye Ligi Kuu England kutoka Atletico Madrid.
Straika huyo wa Kiargentina anaweza kugharimu zaidi ya Pauni 100 milioni. Kutokana na hilo, klabu nyingi sasa zitatazama uwezekano wa kunasa mastraika wengine kutokana na Isak na Alvarez kuwa ghali sana.

Chanzo kimoja kilifichua: “Isak ni Namba 9 bora duniani na amekuwa akifanya vizuri sana kwa sasa, lakini bei yake ni kubwa sana kwa kuzingatia ishu ya vigezo vya mapato na matumizi ambayo ni tatizo kwa klabu nyingi.”
Straika wa Eintracht Frankfurt, Hugo Ekitike, yule wa Sporting CP, Viktor Gyokeres na Liam Delap wa Ipswich Town, ni miongoni mwa washambuliaji ambao bei zao zipo chini, hivyo klabu nyingi zitapambania kunasa huduma zao.
Mtambo wa mabao wa RB Leipzig, Benjamin Sesko naye anajiandaa kutua kwenye Ligi Kuu England, wakati straika wa Juventus, Dusan Vlahovic anaweza kufikiriwa na miamba ya Emirates endapo kama dili zao za awali zitafeli.

Mastraika wote hao ambao wanajiandaa kubadili timu kwenye dirisha lijalo watazigharimu klabu pesa nyingi. Hiyo ni kwasababu timu nyingi vipaumbele vyao vikuu kwenye dirisha lijalo, hasa kwa Ligi Kuu England ni kusajili mastraika.
Usajili wa straika ni dili zinazohitaji ujanja sana kuzifanya. Kwa mfano, West Ham United imefanya usajili wa mastraika 33 tofauti tangu mwaka 2010. Kingine ni bei zao wanazouzwa mastraika kuwa juu.
Jambo hilo ndilo linalowatisha pia makocha, kuhofia kutumia pesa nyingi kwenye usajili wa straika ambaye atashindwa kuleta matunda kwenye timu, kama ambavyo Arteta wa Arsenal aliamua kutosajili straika kwenye dirisha la Januari.
Makocha wanahitaji kuwa makini kwa sababu wanafahamu wazi usajili mbaya unaweza kuwaweka kwenye hatari ya kuonyeshwa mlango wa kutokea na kupoteza ajira zao. Lakini, ukweli huwezi kushinda kitu kwenye soka kama kocha atashindwa kuwa na uthubutu wa kufanya usajili. Hakuna mataji kwa kocha mwoga, lazima pochi lifunguliwe.
Arsenal inahitaji kufanya uamuzi kama inahitaji kubeba taji, isiogope kutumia pesa kusajili straika ambaye yupo tayari kwa kazi kama alivyo Isak. Man United na Chelsea nazo zipo kwenye boti moja na Arsenal katika kutafuta straika.
Man United imetumia pesa nyingi kwenye usajili wa Namba 9 kwa miaka ya hivi karibuni.
Lakini, kwenye usajili wao hasa huu wa miaka ya karibuni, si Rasmus Hojlund wala Joshua Zirkzee, aliyeonyesha kiwango bora na kumaliza tatizo la kupatikana mabao kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.
Jambo hilo ndilo linaloifanya Man United kuhusishwa na mastraika wengine kama Gyokeres, ambaye aliwahi kuwa chini ya kocha Ruben Amorim huko Sporting CP.

Huduma ya Gyokeres inakuhakikishia mabao, baada ya kufunga mara sita katika mechi nne za mwisho kwenye ligi. Gyokeres alipokuwa chini ya Amorim, alifunga mabao 66 katika mechi 68, lakini shida kwa Man United inaweza kumshindwa kumnasa straika huyo endapo kama itashindwa kukamatia tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Sporting itahitaji Pauni 60 milioni, lakini kama bei yake itakuwa juu ya hapo, straika mwingine ambaye anaweza kugeukiwa ni mkali wa Lille, Jonathan David, ambaye atapatikana bure kabisa sokoni.

Chelsea haina shida, pesa inayo kwa ajili ya kumsajili straika Delap ili kuja kumpa upinzani Nicolas Jackson kama itafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya. Na kama itashindwa kukamatia tiketi ya Ulaya, inaweza kuhamia kwa straika Mfaransa, Jean-Philippe Mateta, ambaye amekuwa na kiwango bora huko Crystal Palace.
Straika mwingine ambaye atakuwa njiani kwenye dirisha lijalo ni nahodha wa England, Harry Kane, ambaye anaweza kuachana na Bayern Munich mwishoni mwa msimu. Shughuli ipo kwa wakurugenzi wa michezo, kuhakikisha wanafanya usajili wa mastraika kwenye dirisha lijalo kwa sababu wapo wa kutosha.
Mabosi kazi iko kwao kama ni Berta wa Arsenal, vigogo wawili wa Chelsea Paul Winstanley na Laurence Stewart au Jason Wilcox wa Man United, kuchangamkia fursa ya kunasa mastraika wa maana sokoni.