Vita ya EPL kuendelea tane leo

Muktasari:
- Kijumla kutakuwa na mechi nne huku ya mapema zaidi ikiwa ni ile ya vijana wa Pep Guardiola, Manchester City ambao wataumana dhidi ya Crystal Palace ambapo itahitaji matokeo ya ushindi ili kuzidi kuzisogelea nafasi tano za juu na kufuzu Ligi ya Mabingwa.
LONDON, ENGLAND: RAUNDI ya 32 ya Ligi Kuu England inatarajiwa kupigwa leo ambapo timu mbalimbali zitaendelea kupambana kusaka kushinda vita zao.
Kijumla kutakuwa na mechi nne huku ya mapema zaidi ikiwa ni ile ya vijana wa Pep Guardiola, Manchester City ambao wataumana dhidi ya Crystal Palace ambapo itahitaji matokeo ya ushindi ili kuzidi kuzisogelea nafasi tano za juu na kufuzu Ligi ya Mabingwa.
Mchezo huu utapigwa kuanzia saa 8:30 mchana. Man City ina pointi 52 tofauti ya pointi moja dhidi ya Newcastle iliyopo nafasi hiyo ya tano ingawa matajiri hao wa Jiji la Manchester wapo mbele kwa mchezo mmoja wakiwa wamecheza mechi 31 wakati Newcastle ina 32.
Mechi nyingine ya kesho ni kati ya Nottingham Forest na Everton, ambapo Forest inahitaji kuendelea kudumisha ushindi ili kujikita zaidi katika nafasi ya tatu iliyopo sasa.
Licha ya kwamba hata ikipoteza haitaweza kushushwa kwani Chelsea iliyopo nafasi ya nne ina pointi 53 na wao wana pointi 57, watakuwa wameruhusu kukaribiwa zaidi kwani tofauti ya pointi kati yao itabaki moja.
Kwa upande wa Everton, itahitaji pia kushinda ili kujiweka salama zaidi ingawa pointi 35 ilizonazo sasa ni ngumu kuona ikishuka daraja labda ipoteze mechi tano mfululizo. Hii ni kwa sababu Luton Town inayoshika nafasi ya 18, ina pointi 20.
Arsenal itakuwa na kazi aidha ya kurahisisha safari ya ubingwa ya Liverpool ama kuifanya iwe ngumu kutokana na matokeo ambayo itayapata katika mchezo wake dhidi ya Brentford utakaopigwa kwenye dimba la Emirates kuanzia saa 1:30 usiku.
Kimahesabu Liverpool inahitaji kushinda mechi nne bila ya kujali matokeo ya Arsenal ili kutawazwa kuwa mabingwa lakini kama Arsenal ikipoteza mchezo huu, Liverpool itahitaji kushinda tatu na walau sare moja tu.
Liverpool yenye pointi 73 ikiwa itashinda mechi nne zijazo itafikisha pointi 85 wakati Arsenal ikishinda mechi zake saba zote zilizobakia itakuwa na pointi 83 tu.
Southampton ambayo imeshashuka daraja itakuwa nyumbani kuikaribisha Aston Villa, kwenye mchezo utakaopigwa saa 11:00 jioni wakati Leicester City ambayo nayo muda wowote inaweza kutangazwa kushuka daraja itakuwa ugenini kucheza dhidi ya Brighton muda sawa na mechi ya hapo juu.
Leicester itahitaji kushinda ili kufufua matumaini kwani kwa sasa inashika nafasi ya 19 ikiwa na pointi 17 tofauti ya pointi 18 kati yao na Wolves iliyopo nafasi ya 17.
Wikiendi itanoga pia kesho ambapo Chelsea itakuwa nyumbani kuikaribisha Ipswich Town, wakati Wolves ikiwa mwenyeji wa Tottenham inayopambana kujisogeza nafasi za juu kutoka nafasi ya 14 iliyopo sasa.
Vinara Liverpool watawakaribisha wagonga nyundo kutoka London, West Ham katika mchezo ambao majogoo hao wataanza kuhesabu safari za mechi zao nne wanazotakiwa kushinda ili kutangaza ubingwa.
Vijana wa Ruben Amorim, ambao wanaonekana kuwekeza nguvu zaidi katika michuano ya Europa League ikiwa kama njia yao ya kufuzu Ligi ya Mabingwa watakuwa dimbani kuumana mabingwa wa Carabao Cup, Newcastle United mechi itakayopigwa saa 12:30 jioni wakati zile za Liverpool, Chelsea na Tottenham zikianza saa 10:00 jioni. Mchezo wa mwisho wa kesho utakuwa kati ya Bournemouth na Fulham utakaoanza saa 4:00 usiku.