Basata yamuweka Harmonize kwenye uangalizi kwa mwezi mmoja
Muktasari:
- Basata imesema hatua hiyo inampa msanii huyo fursa ya kuendelea na shughuli zake za sanaa, huku ikisisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua nyingine endapo atashindwa kutekeleza masharti yaliyowekwa wakati wa kipindi cha uangalizi.
Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limempa mwezi mmoja wa uangalizi msanii wa muziki Rajab Abdul, ‘Harmonize’, baada ya kufika na kutekeleza masharti aliyowekewa kufuatia hatua iliyochukuliwa dhidi yake.
Basata imesema hatua hiyo inampa msanii huyo fursa ya kuendelea na shughuli zake za sanaa, huku ikisisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua nyingine endapo atashindwa kutekeleza masharti yaliyowekwa wakati wa kipindi cha uangalizi.
Uamuzi huo umefanyika siku kadhaa baada ya Basata kumsimamisha Harmonize kujihusisha na shughuli za sanaa baada ya kudaiwa kukiuka maadili kupitia video ya wimbo wake unaoitwa “Kudos.”
Kwa mujibu wa Basata, video hiyo ilikiuka maadili na kuvunja heshima ya mtazamaji, hatua iliyotajwa kuwa ni kinyume na Kanuni ya 20(a) ya baraza hilo.
Kutokana na kosa hilo, Harmonize alitozwa faini ya Sh5 milioni na kupewa masharti ya kuondoa au kushusha video hiyo katika mitandao yote ya kijamii. Shughuli zake za sanaa zilisitishwa hadi atakapolipa faini hiyo na kutekeleza masharti aliyopewa.